Thursday, November 28, 2019

PROF.MBARAWA- UJENZI MIRADI YA MAJI KUTOTUMIA WAKANDARASI

Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa katikati Mwenye miwani, akizungumza na Madiwani na Viongozi wa ngazi mbalimbali ofisini kwa Mkuu wa Wilaya (hawapo pichani) wakati akipokea taarifa ya utekelezaji wa miradi ya maji Wilayani humo kabla ya kuanza ziara kukagua miradi ya Maji.
Waziri wa Maji Makame Mbarawa na msafara walioongozana wakishuka mlima kutoka mradi wa Maji wa Luhundwa ambako huko amekagua utekelezaji wa mradi huo, ambao baada ya kukamilika wananchi wa maeneo hayo watapata huduma ya maji Safi.
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa katikati akisisitiza Jambo baada ya kufika katika moja wa mitaro ya kupitisha mabomba ya maji kuelekea katika mradi wa maji wa Luhundwa ambao bado unaendelea na utekelezaji wake ili wananchi wanaozunguka mradi huo waweze kupata huduma ya maji
Mbunge wa Jimbo la Mpwapwa George Lubeleje mwenye suti nyeusi katikati akizungumza na wananchi wananchi waozunguka mradi wa Maji wa Bumila baada ya kuhakikishiwa huduma ya maji na Waziri wa Maji na mkandarasi tayari kashapewa fedha kukamilisha mradi huo.
 
foleni ya madumu na msimamizi wa kituo Cha maji katika mradi wa Maji wa Bumila ambao unafanya kazi kwa dharura ili kupunguza makali ya adha ya maji katika eneo hilo ambapo hata hivyo mkandarasi kashalipwa fedha kukamilisha mradi huo ili kupanua zaidi huduma ya maji katika eneo hilo.
………………
Na.Alex Sonna,Mpwapwa
Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, amesema wamekusudia kuanzia Sasa kuanzisha utaratibu wa kutokutumia wakandarasi au kutoa tenda katika miradi ya maji inayotekelezwa maeneo mbalimbali hapa nchini na badala yake watatumia wataalamu wa ndani ya Mamlaka za maji kukamilisha miradi hiyo.

Waziri Mbarawa ametoa kauli hiyo  Wilayani Mpwapwa wakati wa ziara yake Wilayani Mpwapwa kukagua  utekelezaji wa miradi ya Maji, ambapo amesema wamefikia hatua hiyo baada ya wakandarasi wengi kuchukua fedha na kutokukamilisha miradi hiyo, amesema serikali imewekeza fedha nyingi Sana lakini matokeo yake hayaonakani.

Na kubainisha kuwa miradi mingi wanapewa wakandarasi ambao hawana uwezo au kupeana tenda kindugu na kutekeleza miradi chini ya kiwango.

“Serikali za awamu zote zilizopita ilitenga fedha nyingi Sana kwa ajiri ya miradi ya maji lakini matokeo yake hayaonekani wote tunajiuliza fedha zinakwenda wapi wakati maji hayatoki na fedha hazirudishwi na majibu yake kila mtu anayo”

“Kwahiyo tumeamua kuja na utaratibu huu wakuto kuwatumia wakandarasi na badala yake tutatumia wataalamu wa ndani ya Mamlaka zetu za maji na mfano tumefanya hivyo Mkoa wa Katavi na matokeo tumepata” amesema Waziri Mbarawa.

Katika Ziara hiyo Wilayani Mpwapwa ametembelea miradi ya maji Luhundwa na Bumila kuona utekelezaji wake wake na akiwa katika mradi wa Maji wa Bumila, Waziri wa Mbarawa amewahakikishia wananchi wa Kata hiyo kuwa hivi karibuni wataanza kupata huduma ya maji Safi.
Kwani mradi huo ulikwama kutokana na mkandarasi kutolipwa fedha lakini kwa Sasa mkandarasi huyo kashalipwa fedha na mradi huo utakamilika ndani ya mda mfupi na wataanza kupata huduma ya maji.
“Tunajua mkandarasi wa mradi huu alisimama lakini tumeshamlipa fedha zake na atakuja kukamilisha mradi huu, pia nishukuru Chama Cha Mapinduzi waliweka pumpu ya dharura na mkawa mnapata huduma ya maji, Sasa tutapanua zaidi na kuongeza vituo zaidi ili mpate huduma ya maji kikamilifu naomba muiamini serikali yenu” amesema.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa Jabir Shekimweri akitoa taarifa ya Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt Binilith Mahenge, amesema licha ya miradi mingi kutokukamilika lakini bado huduma ya maji inazidi kuimarika kwani mwaka 2015 ni asilimia 43 tu ndio walikuwa wakipata huduma ya maji na Sasa ni asilimia 57 kwa miji midogo na Wilaya.
Wakati kwa miji mikubwa upatikanaji wa maji ilikuwa, ni  asilimia 65 na Sasa ni asilimia 82, na wamejipanga angalau kufikia mwaka 2025 kwa miji midogo ifikie asilimia 80 na miji mikubwa wafikie asilimia 95.
Aliongeza kuwa ” kwa Wilaya ya Mpwapwa Kuna miradi 10, inayotekelezwa mpaka Sasa, Saba (7)mipya na mitatu(3) ya ukarabati yote ikiwa na thamani ya shilingi bilioni 4.17, huku changamoto ikiwa ni fedha kutofika kwa wakati maeneo husika” amesema DC Shekimweri.

Kutokana na hali ya kutofika kwa wakati kwa fedha za utekelezaji wa miradi hiyo Mkuu huyo wa Wilaya amemuomba Waziri kuhimiza watendaji wa Mamlaka za maji na usafi wa mazingira Vijijini RUWASA makao makuu kupeleka fedha kwa wakati ili miradi hiyo ikamilike kwa wakati wananchi waweze kupata huduma ya maji Safi.

Amesema changamoto hiyo ya fedha kutofika kwa wakati imekuwa chanzo kikubwa kwa miradi mingi kutokamilika kwa wakati katika Wilaya hiyo huku wananchi wakiendelea kupata adha ya maji.

Baadhi ya Wananchi wa wanaozungua mradi wa Maji wa  Bumila wameishukuru serikali kwa kuleta fedha za mradi huo kwani shida ya maji katika eneo hilo ni kubwa sana wamesema angalau Sasa adha ya maji itapungua kwa kiasi kikubwa Sana kwani hiyo ilikuwa kero kubwa Sana kwao

No comments:

Post a Comment