Na Jovina Bujulu, MAELEZO, Dar es Salaam
Serikali ya Awamu ya Tano
inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli imeendelea kujidhihirisha jinsi
inavyofanya kazi kwa ufanisi na weledi kwa kuhakikisha inatekeleza
mipango yake kwa kasi inavyotakiwa.
Hatua hiyo inapelekea utendaji wa
kazi za Serikali kuwa bora na zenye tija kwa wananchi siku hadi siku na
zenye nia ya kuleta mabadiliko katika utekelezwaji wa miradi mbalimbali
ambayo hutumia pesa nyingi za umma inayoendana na thamani ya pesa.
Kwa kuzingatia kuwa fedha
zitumikazo katika utekelezaji wa miradi ya Serikali kwa kiasi kikubwa
hutumika kupitia mfumo wa ununuzi wa umma. Ili kuleta tija kwa taifa,
Serikali imeamua kuimarisha eneo hilo kwa kuanzisha Mfumo wa Ununuzi kwa
njia ya Kielektroniki (TANePS) ambao unasimamiwa na Mamlaka ya
Kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA) chini ya Wizara ya Fedha na Mipango.
Ili uwe endelevu, mfumo
umetayarishwa kwa mujibu wa Sheria ya Ununuziwa Umma ya Mwaka 2011na
Kanuni za Ununuzi wa Umma chini ya Tangazo la Serikali Na. 446 la Mwaka
2013. Sehemu ya XI ya Kanuni hizo inabainisha utaratibu wa mfumo wa
manunuzi kwa njia ya mtandao kwa mujibu wa Kanuni ya 343,mambo
yatakayotekelezwa kwa mfumo ni pamoja na usajili wa watumiaji, mchakato
wa zabuni, ununuzi wa bidhaa, mnada wa mtandaoni, malipo ya ada
mbalimbali pamoja na usimamizi wa mikataba mbalimbali.
Akizungumza mfumo huo hivi
karibuni Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James alisema
kuwa mfumo umeanzishwa ili kuiwezesha Serikali kupata thamani halisi ya
fedha zinazotumika kupitia ununuzi wa bidhaa, huduma na kazi za ujenzi.
Mfumo wa ununuzi umeanza kutumika
tayari kuanzia mwezi Machi 2018 kwa mujibu wa Kanuni ya 342(1) ambapo
baadhi ya taasisi za umma zimeunganishwa baada ya kukamilisha taratibu
muhimu ikiwemo mafunzo kwa watumiaji wa mfumo huo na mfumo huo upo wazi
kwa wafanyabiashara kujisajili.
Akielezea baadhi ya faida za mfumo
huo, Katibu Mkuu James alisema kuwa ni pamoja na kurahisisha ushiriki
wa wazabuni kwenye michakato ya ununuzi na hivyo kuongeza ushindani na
ufanisi na kupunguza muda unaotumika katika mchakato wa zabuni.
“Mfumo huu utaongeza uwazi na
kupunguza vitendo vya rushwa ikiwa ni pamoja na kuongeza kiwango cha
uwajibikaji kutokana na urahisi wa uhakiki wa michakato ya zabuni
inayoendeshwa, kupunguza gharama za ununuzi kutokana na uokoaji wa
muda, pamoja na kupunguza muda wa kuandaa vikao na tathmini yake pamoja
na kuimarika kwa utunzaji wa kumbukumbu za ununuzi.” alisisitiza Katibu
Mkuu James.
Inakadiriwa kwamba kuanzishwa kwa
mfumo huu kutaokoa wastani wa shilingi bilioni 34 katika miaka mitano ya
kwanza, hali ambayo itaipunguzia Serikali mzigo mkubwa uliokuwa
unatokana na matumizi yasiyo na tija ambayo yalikuwa kwenye mfumo wa
kawaida.
Kwa kuzingatia manufaa ya mfumo
huo, Serikali imeagiza PPRA kuhakikisha kuwa ifikapo tarehe 31, Desemba,
mwaka huu ihakikishe kwamba taasisi zote za nunuzi nchini ziwe
zimeungwa katika mfumo huo.
“ Natoa wito kwa wazabuni, taasisi
binafsi na za umma na wananchi kwa ujumla kuungana na Serikali kwa
kutoa ushirikiano wa kutosha ili kufanikisha azma ya Serikali ya kuwa
na mfumo wenye tija kwa taifa” alisema James.
Kwa upande wake Afisa Mtendaji
Mkuu wa Mamlaka ya kudhibiti Ununuzi wa Umma (PPRA), Mhandisi Leonard
Kapongo alisema baada ya kupatiwa maelekezo hayo Mamlaka ilianza kutoa
mafunzo kuhusiana na matumizi ya mfumo wa TANePS kwa maafisa wa ununuzi
na TEHAMA wa taasisi za Umma.
“Mpaka sasa Mamlaka imefanikiwa
kuunganisha taasisi 418, huku wataalamu waliopatiwa mafunzo kutoka
taasisi nunuzi ikifikia 1,600 ambapo mara baada ya kupatiwa mafunzo
taasisi zao huunganishwa kwenye mfumo na kuendelea kutekeleza michakato
yote ya ununuzi inayofuata” alisema Mhandisi Kapongo.
Mhandisi Kapongo alitoa rai kwa
wakuu wa taasisi kuhakikisha kwamba wanatumia mfumo huo kwani ni takwa
la Sheria ya Ununuzi na Kanuni zake, na kwamba PPRA watafuatilia kwa
karibu kuhakikisha matumizi sahihi ya mfumo huo.
Watoa huduma mbalimbali, wazabuni
na makandarasi wameshauriwa kuchangamkia fursa ya kushiriki kwenye
michakato ya zabuni kwa kujisajili TANePS kupitia tovuti ya mfumo ambayo
ni, www.taneps.go.tz ambapo watapata maelekezo mbalimbali ya namna ya kujisajili.
Akizungumzia faida ya mfumo huo
kwa wazabuni, Mhandisi Kapongo alisema kuwa ni mfumo uliorahisishwa sana
kwa vile hawatahitaji tena kutumia makabrasha au kusafiri kwa ajili ya
kuwasilisha zabuni zao.
“Mambo yote hayo yatafanyika kwa
njia ya mtandao, yakihusisha kutangazwa kwa mipango ya ununuzi ya mwaka,
matangazo mahsusi ya zabuni na Wazabuni waliosajiliwa kuweza kupakua
nyaraka za zabuni na kuziwasilisha kwa taasisi nunuzi kwa njia ya
mtandao na majibu ya washindi wa zabuni yatatangazwa kwenye mtandao wa
mfumo” alisema Mhandisi Kapongo.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya PPRA,
Balozi Dkt, Marten Lumbanga ameunga mkono mfumo huo na kuongeza kuwa
utarahisisha kazi na kuweka uwazi kwa mapato ya Serikali yanayoingia
kupitia ununuzi kwa taasisi za umma.
No comments:
Post a Comment