Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi akiangalia moja ya Majalada katika ofisi ya Ardhi
ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero jana. Kulia kwa Lukuvi ni Mkuu wa
Wilaya ya Mvomero Mwl Mohamed Utaly na kulia ni Kaimu Kamishna Msaidizi
wa Ardhi Kanda maalum ya Morogoro Erick Makundi.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi akiangalia moja ya Majalada katika ofisi ya Ardhi
ya Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero jana.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya
Makazi William Lukuvi akizungumza na viongozi wa wilaya ya Mvomero
pamoja na watendaji wa sekta ya ardhi wakati wa ziara yake ya kutatua
migogoro ya ardhi mkoa wa Morogoro. Wa pili kulia ni Mkuu wa wilaya ya
Mvomero Mwl Mohamed Utaly
(PICHA ZOTE NA WIZARA YA ARDHI)
………………….
Na Munir Shemweta, WANMM MVOMERO
Raisi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt John Pombe Magufuli amebatilisha pendekezo la kufutwa shamba lenye
ukubwa wa ekari 1000 lililopo Kidunda wilayani Mvomero mkoani Morogoro
linalomilikiwa na Cecilia George Rusimbi.
Uamuzi wa Dkt Mafuli kubatilisha
ufutaji shamba hilo unatokana na kubainika kuwa pendekezo
lililowasilishwa la kufutwa shamba hilo kwa madai ya kutoendelezwa
kutokuwa za kweli na ulilenga kumdhulumu mmiliki wake.
Akitangaza uamuzi huo wa Raisi jana
wilayani Mvomero, Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William
Lukuvi alisema, baada ya kufuatilia mashamba yaliyopendekezwa kufutwa
Dkt Magufuli alibaini taarifa alizopelekewa za kufuta shamba Cecilia
hazikuwa sahihi na hivyo kuamua kubatilisha pendekezo lililowasilishwa
kwake na kumpatia haki yake mmiliki.
Kufuatia hali hiyo Waziri Lukuvi
aliwaonya Aaafisa ardhi nchini kuhakikisha wakati wa kufanya zoezi la
ukaguzi/Upekuzi wa mashamba yasiyoendelezwa wanazingatia haki pamoja na
kufuata sheria badala ya kufanya kazi hiyo kwa upendeleo au kumuonea
mtu.
Hata hivyo, Waziri wa Ardhi alisema,
utendaji kazi katika wilaya ya Mvomero umekuwa wa hovyo na usiozingatia
maadili jambo linalopelekea wilaya hiyo kuongoza katika mkoa wa Morogoro
kuwa na migogoro mingi ya ardhi sambamba na malalamiko mengi ya
wananchi dhidi ya ofisi ya ardhi.
‘’Baadhi ya watumishi katika ofisi ya
halmashauri ya wilaya ya Mvomero mnajifanya ni Maafisa ardhi au Wapima
wakati hamkuajiriwa kwa nafasi hiyo, mnasaini nyaraka za ardhi na
kuwaumiza wananchi’’ alisema Lukuvi
Kwa upande wake Cecilia George Rusimbi
alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe
Magufuli kwa uamuzi wake wa kubatilisha ufutaji sahamba lake na
kuuelezea uamuzi huo kuwa umezingatia haki na kusikia kilio chake
ambapo alisema umempa faraja baada ya kuhangaika sana kuhusiana na
shamba hilo.
‘’ Nimemiliki shamba tangu mwaka 1987
na kuhangaikia hati kwa muda mrefu na nimeshangazwa kuelezwa kuwa shamba
langu liko katika mpango wa kufutwa kutokana na kutoendelezwa, hii
imenifanya kuishi kwa wasiwasi’’ alisema Cecilia.
Waziri Lukuvi ameagiza shamba hilo la
kilimo cha Michikichi, Mitiki na Bamboo kupangwa upya na mmiliki wake
kupatiwa hati kulingana na upimaji utakaofanywa na kumtaka kuliendeleza
kwa mujibu wa sheria.
Sambamba na sakata la shamba la
Cecilia, Lukuvi aliagiza kupunguzwa ukubwa wa Shamba Sangasanga na
Lubango lililodaiwa kuwa na ukubwa wa ekari 1,103 wakati uhalisia wa
shamba hilo ni ekari 500 na kuagiza mmiliki wake kurudisha hati ili
apatiwe hati ilinayolingana na uhalisia wake na ekari 603.5
zilizoongezwa zitabaki kuwa ardhi ya akiba.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Mvomero Mwl
Mohamed Utaly alieleza kuwa wilaya yake ina tatizo kubwa la migogoro ya
ardhi pamoja na jitihada kubwa inayofanywa na ofisi yake kukabiliana na
tatizo hilo na kuongeza kuwa mingine inachochewa na uhamasishaji
unaowafanya wananchi kukata tamaa.
Katika hatua nyingine Waziri wa Ardhi
Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi alitembelea ofisi ya Ardhi
katika halmashauri ya Mvomero na kubaini ‘madudu’ katika ofisi hiyo
ambapo alibaini baadhi ya majalada ya wananchi waliomba kumilikishwa
ardhi tangu mwaka 2012 katika halmashauri hiyo kushindwa kupatiwa hati
huku.
Hali hiyo ilimfanya Waziri Lukuvi
kumuagiza Kaimu Kamishana Msaidizi wa Ardhi Kanda Maalum ya Morogoro
Erick Makundi kuhakikisha wale wote walioomba hati na kutumiza vigezo
vya kupatiwa hati wanapatiwa kufikia mwezi ujao Desemba 2019. Pia
ameagiza kufuatiliwa majalada 300 ambayo wamiliki wake wamekamilisha
taratibu za kupatiwa hati lakini hawajapatiwa.
Sambamba na hilo Lukuvi aliagiza
wafanyakazi wa ofisi ya ardhi katika halmashauri hiyo wanaojitolea
kutosaini nyaraka zozote za ardhi kwa kuwa baadhi yao wamekuwa
wakishiriki kutoza tozo kwa gharama za juu za shilingi 50,000 wakati
gharama halisi ni 20,000.
No comments:
Post a Comment