Katibu Mkuu ofisi ya Rais Tawala
za mikoa na serikali za mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph
Nyamhanga,akizungumza katika kongamano la majadiliano Wiki ya asasi za
kiraia (Azaki) linaloendelea jijini Dodoma
Katibu Mkuu wa Shirikisho la watu
wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata) Jonas Lubago,akiongea wakati wa
kongamano la majadiliano Wiki ya asasi za kiraia (Azaki) linaloendelea
jijini Dodoma
……………………
Na Alex Sonna
Wakurugenzi wa Halmashauri na
Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kutoa elimu ya ujasiriamali
kwa vikundi vya watu wenye ulemavu ili wanufaike na mikopo inayotolewa
na Halmashauri hizo.
Agizo hilo limetolewa leo na
Katibu Mkuu,Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga katika kongamano la asasi za kiraia
(AZAKI) linaloendelea Jijini Dodoma.
Amesema watu wenye ulemavu
wamekuwa hawatumii fursa ya mikopo inayotolewa na Halmashauri kutokana
na wengi wao kutokuwa na elimu ya ujasiriamali.
“Matokeo yake wanaishia kuishi
maisha ya utegemezi na kuomba omba mitaani, ninajua kabisa watu wenye
ulemavu hawawezi kupata mikopo kwenye taasisi za kifedha ikiwemo mabenki
kutokana na hali yao, ndio maana serikali kwa kuliona hilo iliamua
kutenga asilimia 2 kati ya 10 ya mapato ya ndani ya Halmashauri zote
nchini kwa ajili ya kutoa mikopo kwa makundi maalum yakiwemo ya watu
wenye ulemavu,” amesema.
Ameeleza watu wengi wenye
ulemavu bado hawajajitokeza vya kutosha kutumia fursa ya mikopo kwa
ajili ya kujiimarisha kiuchumi hivyo wakurugenzi na maafisa hao
wanatakiwa kutoa elimu ili waweze kujitokeza.
Amebainisha katika mwaka wa
fedha 2018/19 Halmashauri nchini zilitenga jumla ya Sh. Bilioni 54.08
kwa ajili ya mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye
ulemavu lakini mpaka kufikia Juni 30, mwaka huu kiasi cha fedha
kilichokuwa kimetolewa ni Sh.Bilioni 42.06 ambapo vikundi vya watu
wenye ulemavu walipata kiasi cha fedha Sh.Bilioni 3.87.
“Kwa mwaka wa fedha 2019/20
serikali imetenga kiasi cha fedha Sh.Bilioni 62.22 ambapo wanawake na
vijana wametengewa Sh.Bilioni 24.9 na watu wenye ulemavu wametengewa
Sh.Bilioni 12.4,”amesema.
Naye, Katibu Mkuu wa
Shirikisho la watu wenye ulemavu Tanzania (Shivyawata), Jonas Lubago
amesema watu wengi wenye ulemavu hawana uelewa wa mikopo inayotolewa na
Halmashauri nchini na ndiyo maana hawajitokezi kukopa.
Ameomba serikali kuangalia
uwezekano wa kuwakopesha watu wenye ulemavu wakiwa mtu mmoja mmoja maana
wengi wanashindwa kutumia fursa ya mikopo kwa kukosa watu wa kujiunga
nao kwenye vikundi.
No comments:
Post a Comment