Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango akisisitiza kuhusu umuhimu wa Taasisi na Mashirika ya umma
kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli la kuhakikisha kuwa
zinawakilisha gawio lao ndani ya siku 60 zilizotolewa.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa
Shirika la Reli Tanzania Bw. Masanja Kadogosa ikiwa ni utekelezaji wa
agizo la Rais Dkt. John Pombe Magufuli alilotoa wakati akipokea gawio
kutoka kwa Taasisi na Mashirika ya Umma Novemba 24, 2019 Jijini Dodoma.
Waziri wa Fedha na Mipango Dkt.
Philip Mpango akipokea mfano wa hundi kutoka kwa Watendaji wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC).
Watendaji wakuu wa Taasisi na
Mashirika ya Umma wakionesha mfano wa hundi zao leo ambazo ni jumla ya
shilingi bilioni 2.75, wakati wa hafla ya kuwasilisha gawio kwa
Serikali ikiwa ni utekelezaji wa agizo la Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo Jijini Dodoma.
………………….
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Saa chache baada ya Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kutoa siku 60 kwa Taasisi, Kampuni ambazo Serikali ina
hisa chache na Mashirika ya Umma 187 ambayo hayajatoa gawio au mchango
kwa Serikali tayari Taasisi nne zimetekeleza agizo hilo leo.
Akizungumza leo, jijini Dodoma,
wakati akipokea gawio na michango kutoka Shirika la Posta, Shirika la
Reli (TRC), Self Microfinance Fund, na Kituo cha Uwekezaji Tanzania
(TIC), ambapo jumla ya fedha zilizowasilishwa ni shilingi bilioni 2.75,
Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Philip Mpango alisema kuwa baada ya
agizo la Rais alilolitoa jana, hakutakuwa na mzaha kwa Taasisi, Kampuni
na Mashirika ambayo hayatekeleza agizo hilo ndani ya siku 59 zilizobaki.
“Nitasimamia kikamilifu agizo hili
la Mheshimiwa Rais, itakapofika siku ya 60 nitatembeza panga bila uoga
wala kupepesa macho kwa Taasisi, Kampuni na Mashirika ambayo hayatakuwa
yametekeleza agizo hili, hatutanii katika hili” alisema Waziri Mipango.
Aidha, Waziri Mpango alizishukuru
Taasisi hizo kwa kutekeleza agizo la Rais na kuongeza kuwa angependa
kuona Mashirika yaliyobaki yakitekeleza agizo hilo kwa wakati, kwa kuwa
fedha hizi si zake wala za Rais bali ni kwa ajili ya kutekeleza miradi
ya maendeleo kwa faida ya watanzania wote.
Naye, Msajili wa Hazina, Athumani
Mbutuka alisema kuwa alitekeleza agizo la Rais Magufuli la kumtaka
kuzijulisha Taasisi, Kampuni na Mashirika 187 ambayo hayakuwa yametoa
gawio na michango kufanya hivyo ndani ya siku 60, ambapo Taasisi za TRC,
TIC, Shirika la Posta na Self Microfinance Fund wamekuwa wa kwanza
kutekeleza agizo hilo.
Rais Dkt. John Pombe Magufuli jana
alipokea gawio na michango kutoka kwa Taasisi, Kampuni na Mashirika 79
ambayo yalitoa jumla ya shilingi trilioni 1.05, ambapo Mamlaka ya
Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Mamlaka
ya Hifadhi za Taifa (TANAPA), Mamlaka ya Hifadhi ya Bonde la Ngorongoro,
Wakala wa Huduma za Misitu na Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM)
yalikabidhiwa cheti kwa kufanya vizuri. Aidha, TPA iliyotoa gawio la
shilingi bilioni 169 na TPC iliyotoa shilingi bilioni 14 yalipewa tuzo
kwa kutoa gawio kubwa zaidi.
No comments:
Post a Comment