Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (katikati waliokaa) Katika Picha ya pamoja na Watumishi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga pamoja na viongozi wengine.
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo akitoa pongezi zake kwa Madiwani na Watumishi Halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga katika baraza la madiwani lililofanyika katika mji
wa Laela.
Madiwani wa kwanza kushiriki
katika baraza la madiwani la kwanza kufanyika katika mji wa Laela ambapo
ndio makao makuu mapya ya halmashauri ya Wilaya hiyo.
…………….
Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo amewapongeza madiwani pamoja na watumishi wa halmashauri ya
Wilaya ya Sumbawanga kwa kuweza kutekeleza agizo la Rais Dkt. John Pombe
Magufuli alilolitoa tarehe 6, Oktoba 2019 alipokuwa katika ziara yake
ya siku 3 ambapo aliiagiza halmashauri hiyo kuhamia Laela pamoja na
halmashauri nyingine nchini kuhamia katika maeneo yao ya kiutawala.
Amesema kuwa ni watumishi 16 tu
kati ya watumishi 165 wa makao makuu ya halmashauri wanaotumia mifumo ya
watumishi (LAWSON), mfumo wa mapato LGRCIS), Mfumo wa malipo wa EPICOR,
TASAF na Kitengo cha Uchaguzi ndio waliobaki mjini wakisubiri
miundombinu hiyo kukamilika katika makao mapya ya halmashauri hiyo
katika Mamlaka ya mji mdogo wa Laela.
“Nitoe maelekezo kwa Mkurugenzi wa
Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga kushirikiana na Wadau wengine
(Mfano TTCL) ahakikishe anaunganisha Makao Makuu Mapya ya Halmashauri
Laela kwenye Mkongo wa Taifa. Hii itawezesha Mifumo mingine inayotumia
Mtandao wa mawasiliano kuweza kufanya kazi kutokea hapa hapa Laela.
Ninamuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha Watumishi ambao bado
hawajahamia Laela wawe wamehamia ifikapo tarehe 1 Januari, 2020.”
Alisema.
Aidha, ameitaka menejimenti ya
halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau kufanya tathmini juu ya
kuwafikia wananchi waliopo mbali na Laela kama vile kutoka katika vijiji
vya mfinga, Mwadui, Kalumbaleza wanaokwenda kupata huduma Laela ambao
wanatoka umbali wa zaidi ya kilometa 150.
Ameyasema hayo katika kikao cha
baraza la madiwani la kwanza kufanyika katika makao makuu hayo mapya ya
halmashauri hiyo tarehe 21.11.2019, kikao kilichohudhuriwa na viongozi
wa vyama mbalimbali vya siasa, madiwani pamoja na watumishi wa
halmashauri.
Awali akitoa taarifa ya maandalizi
ya kuhamia katika makao hayo mapya Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt.
Khalfan Haule alisema kuwa kitengo cha uchaguzi kimebaki mjini kutokana
na kukosekana kwa eneo kubwa la kuhifadhia vifaa vya uchaguzi lakini
mara tu uchaguzi utakapopita kitengo hicho kitahamia katika mji wa
Laela.
“Kwahiyo Wakimaliza uchaguzi
wakiandaa ile taarifa tutahakikisha nao wanahamia haa Laela, Watu wa
Fedha na watu wa Utumishi wanawasiliana na watu wa TTCL ili mokongo ule
wa taifa uweze kupatikana hapa Laela na zile huduma zao ziweze kuhamia
hapa Laela, kwa ujumla shughuli zinaenda vizuri na wananchi wanaendelea
kuhudumiwa vizuri hapa Laela,” Alisema.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti
wa Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Apolinari Macheta alisema kuwa
watumishi wa halmashauri hiyo walikuwa wakishiriki usafi wa Jumamosi ya
mwisho wa mwezi katika eneo ambalo halikuwa la kwao na pia walikuwa
wakichangia maendeleo katika maeneo ambao sio ya kwao.
“Tulichelewa sana na ni maamuzi
ambayo yangefanyika hata huko nyuma tungeweza kuwa parefu zaidi lakini
tunakushukuru sana kwa namna mji wetu wa Laela ulivyo hautofautiani na
mji wa sumbawanga na hata kama ni changamoto ni za kawaida haziwezi
kufanana na za wengine kwakweli tunaonekana tuko mjini.” Alisema.
Wakati akitoa neno la Shukurani
mbunge wa jimbo la Kwela Mh. Ignus Malocha alisema kuwa yeye ndio wa
kwanza kutangulia kwani ofisi yake ilikuwa ya kwanza kabla ya Mkurugenzi
kuhamia katika mji huo baada ya wiki mbili tu tangu Rais Dkt. John
Pombe Magufuli kutoa agizo hilo, hivyo alimshukuru mkuu wa mkoa kwa
kusimamia zoezi hilo la utekelezaji wa agizo la Rais.
No comments:
Post a Comment