Wednesday, October 2, 2019

TUSIRUHUSU MFUMO MPYA UNUNUZI WA KOROSHO-MAJALIWA

WAZIRI MKUU amewaagiza Wakuu wa Mikoa yote inayolima korosho nchini wahakikishe wanasimamia vizuri zao hilo na wasiruhusu kuingizwa kwa mfumo mpya wa ununuzi ambao haujaeleweka kwa wadau na wanunuzi.
“Mabadiliko  ya mifumo yalitolewa na baadhi ya viongozi ambao sio waaminifu, Serikali iko macho itawachukulia hatua viongozi wa vyama vya ushirika wasiokuwa waaminifu. Tunataka mfumo wenye manufaa ndio utumike.”
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 2, 2019) wakati akizungumza na wananchi wa mkoa wa Mtwara baada ya kukagua ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inayojengwa katika eneo la Mitengo, wilayani Mtwara.
Waziri Mkuu amesema msimu wa korosho kwa mwaka huu unatarajiwa kutangazwa hivi karibuni, hivyo ni lazima kwa wakuu wa mikoa inayolima korosho wakajiandaa vizuri ili kuepusha migogoro isiyokuwa ya lazima.
Waziri Mkuu ameendelea kuwasisitiza wafanyabiashara kutojihusisha na ununuzi wa korosho kwa njia ya kangomba.”Kangomba imepigwa marufuku, watakaojihusisha moto utawawakia huko huko . Tunataka wakulima wenyewe ndio wanufaike”
Pia, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wakulima wa zao la korosho kuendelea kujiimarisha na wahakikishe wanajiwekea akiba kwa ajili ya ununuzi wa pembejeo kwa sababu. “Serikali  itaendelea kusimamia zao hili ili wakulima wapate tija.”
Mapema, Waziri Mkuu ametembelea ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini na kukagua kazi ujenzi inayoendelea hospitalini hapo, ambapo amesema itakapomalizika itawapunguzia wananchi safari ya kwenda Muhimbili kufuata huduma.
Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli imejikita katika kuboresha huduma mbalimbali za wananchi zikiwemo za afya, hivyo wananchi wa Kanda ya Kusini watapata matibabu ya kibingwa karibu na maeneo yao.
“Hakuna mashaka wala wasiwasi wa kupata huduma bora za afya kuanzia sasa na kuendelea kwa sababu Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeendelea kuwezesha utaratibu mzuri wa kupata huduma za afya nchini.”
Ujenzi wa hospitali hiyo ya Rufaa ya Kanda ya Kusini unatarajiwa kukamilika Agosti 2020 na kwa sasa inajengwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa gharama ya zaidi ya sh. bilioni 15 na tayari Serikali imeshatoa zaidi y ash. bilioni sita.
Kwa upande wake, Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu alisema Serikali imetenga zaidi ya sh. Bilioni 15 kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za afya
Alisema historia ya mradi wa ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini inayojengwa Mkoani Mtwara ilianzia kwenye kikao cha Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi cha Mkoa cha tarehe 16 Januari 1979. Halmashauri Kuu ilijadili na kuazimia kuishawishi Serikali kujenga hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Kusini itakayohudumia Mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma.
Waziri Ummy aliongeza kuwa hospitali hiyo inajengwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza  ilianza mwaka wa fedha 2005/2006 kwa kazi ya upimaji wa mipaka na mwinuko wa ardhi kupitia kampuni ya Beacon Consult Ltd kwa gharama ya sh. 26,000,000 na ilikamilika ndani ya siku 30 za mkataba. Kwa sasa ujenzi huo upo katika awamu ya nne.
Awali,Waziri Mkuu alitembelea kiwanda cha kubangua korosho cha Yalin kilichopo katika eneo la Msijute mkoani Mtwara na kukagua kazi ya ubanguaji pamoja na kuzungumza na watumishi wa kiwanda hicho ambao waliishukuru Serikali kwa kuhamasisha ujenzi wa viwanda.

No comments:

Post a Comment