Friday, October 4, 2019

Dkt Mollel atoa Mwito kwa wauzaji na wasambazaji wa Viuatilifu nchini


Na Innocent Natai, TPRI-Arusha

Kaimu Mkurugenzi mkuu wa Taasisi ya Utafiti wa Viuatilifu vya kudhibiti visumbufu katika Ukanda wa Tropiki (Tropical Pesticides Research Institute-TPRI) Dkt Margaret Mollel amewataka wauzaji na wasambazaji wa viuatilifu nchini kuepuka uuzaji wa viuatilifu ambavyo vinaingizwa kwa njia za panya ambavyo havijakaguliwa na kusajiliwa na taasisi hiyo.

Akizungumza wakati wa ufunguzi wa warsha ya siku tatu inayofanyikia katika taasisi hiyo mkoani Arusha, ikiwa kutanisha  watafiti wanaofanya majaribio ya kuhakiki viuatilifu kabla ya kuvisajili kutoka katika vituo vya kilimo hapa nchini kutoka SUA pamoja na TPRI kadhalika wataalamu waliobobea katika maeneo hayo ili kuondoa changamoto ya uandaaji wa ripoti.

Dkt Mollel ametoa mwito kwa wafanyabiashara wa viuatilifu kuacha Kufanya biashara bila kibali, Kuuza/kusambaza viuatilifu visivyosajiliwa, Kuuza /kusambaza viuatilifu visivyo na vibandiko (lebo), Kuuza viuatilifu vilivyoisha muda wa matumizi, na Uhamishaji wa viuatilifu (Repacking/Decanting)

Kuuza viuatilifu kwenye eneo ambalo halijakaguliwa na Mkaguzi wa Viuatilifu, Kuuza viuatilifu kwa kutembeza mitaani, Kuuza viuatilifu kwenye masoko,  minadani na kutandaza barabarani/vijiweni kwani hayo makosa yote yanaweza kuwasababishia wakulima hasara kwa kununua viuatilifu ambavyo havikidhi haja yao na wakati mwingine kuleta madhara katika mazao, mazingira na hata kwa binadamu.

Aidha amewaasa pia wakulima kuacha kununua viuatilifu  ambavyo vinaingizwa hapa nchini kinyume na sheria vikiwa havijafanyiwa utafiti na kusajiliwa na TPRI  kwa kisingizio cha kupunguza gharama kutokana na wahalifu hao kuuza kwa bei rahisi.

“Tunataka viuatilifu vilivyo bora hapa nchini, wachukue viuatilifu vyenye nembo ya TPRI ambavyo tumeshakwisha kuvifanyia utafiti, kuvikagua na kuhakiki kuwa havina madhara tuna wataalamu waliobobea ambao wanapima viuatilifu kabla ya kuvisajili kwa ajili ya kutumika hapa nchini hivyo mmavyo nunua kwa bei rahisi havina ubora uliokusudiwa utanunua vingi na bado hautaweza kuuwa visumbufu “ Alisema Dkt Mollel

Pia amesema kuwa watakao kutwa wakiuza au kuvisambaza viuatilifu ambavyo havija fanyiwa utafiti, kukaguliwa na kusajiliwa na TPRI (ambavyo havina nembo ya TPRI) na makosa hayo mengine watachukuliwa hatua kali za kisheria ikiwemo Faini: Kati ya Shilingi milioni 10 hadi milioni 100 kwa makampuni makubwa, mtu binafsi faini Kati ya Shilingi milioni  2 hadi milioni 10 au kifungo miaka mitatu au vyote, kwa mkosaji sugu adhabu zilizotajwa hapo juu pamoja na kunyang’anywa kibali cha kufanya biashara ya viuatilifu.

Aidha akizungumzia warsha hiyo inayofanyikia katika taasisi hiyo ikiwakutanisha  watafiti wanaofanya majaribio ya kuhakiki viuatilifu  kabla ya kuvisajili kutoka katika vituo vya kilimo hapa nchini, SUA, TPRI na wataalamu waliobobea katika maeneo ya viuatilifu.

Amesema kuwa warsha hiyo imeandaliwa maalumu kwa ajili ya kuondoa changamoto iliyokuwepo katika uandaaji wa ripoti za utafiti ili kukaa pamoja na kuwekeana utaratibu na mwongozo wa namna gani wataandaa ripoti zilizo katika mfumo mmoja pia kwa kufuata miongozo iliyowekwa kwa nchi za jumuia ya Afrika Mashariki.

“Baada ya warsha hii watatoka na mfumo mmoja katika uandaaji wa ripoti, na sio kwamba hapo nyuma walikuwa wanafanya vibaya hapana walikuwa wanafanya vizuri” Aliongeza Dkt Mollel

Ametoa wito kwa washiriki wote wa warsha hiyo elimu watakayo ipata waipeleke kwa wengine ambao hawajafanikiwa kushiriki na pia watoke na azimio moja zuri kwas ababu itarahisisha katika vikao vya kupitisha viuatilifu kabla ya usajili.

MWISHO

No comments:

Post a Comment