WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi uratibu
mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja nchini kuwekeza
kwa kuwaunganisha na Taasisi na Wizara husika ili waweze kuwekeza mitaji
yao kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Ametoa
agizo hilo jana (Alhamisi, Oktoba 24, 2019) baada ya kugundua uwepo wa
wafanyabiashara wengi wa Urusi wanakusudia kuja Tanzania kwa ajili ya
kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa
Kitanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.
“Tayari
miadi imekwishawekwa ya kuwakaribiasha wawekezaji wa Urusi kuja
Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa
wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa wafanyabiashara hao
wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo.” Waziri
Mkuu alisisitiza.
Alisema
Mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na
Urusi uliomalizika jana Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri
zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.
Akizungumza
baada kumalizika mkutano huo kwenye ukumbi wa Olympic Park wa Sochi
nchini Urusi, Waziri Mkuu alisema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza
bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza
kwa faida ya pande zote mbili.
Waziri
Mkuu aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo
kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, Ujenzi wa
miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za
mafunzo nchini humo.
Alisema
kwa upande wake Tanzania imejinadi vizuri ikIngozwa na yeye mwenyewe
kwani alifanya mazungumzo na viongozi wa makampuni zaidi ya manane ya
Urusi ili kuyashawishi yawekeze nchini na yote yalikubali kufika
Tanzania mapema iwezekanavyo.
“Viongozi
wa makapuni yote niliyopata nafasi ya kuzungumza nao wamesema wako
tayari kuja nchini ili waweze kufanya mazungumzo na Serikali pamoja na
wafanyabiashara wazalendo ambao wako tayari kuungana na wafanyabiashara
hao katika kuwekeza nchini Tanzania.”
Waziri
Mkuu alisema viongozi hao walimueleza maeneo ambayo wao wanaamini kuwa
wanafanya vizuri na wangependa kupata kibali cha kuwekeza Tanzania baada
ya mazungumzo yao na Serikali. Pia walieleza ni kwa namna gani Taifa
litanufaika na uwekezaji wao.
Alisema,
tayari wafanyabiashara binafsi 18 wa Tanzania walijitokeza kushiriki
katika Mkutano huo na walifanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahabarisha
wenzao wa Urusi kuhusu mazingira mazuri ya kuwekeza yaliyopo nchini hasa
baada ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John
Pombe Magufuli kuondoa kero, kanuni na taratibu ziliokuwa zikiyafanya
mazingira ya uwekezaji kuwa magumu.
Awali,
akizungumza kwenye Mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka
mataifa ya Afrika na Urusi, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Tanzania ni
nchi sahihi kwa uwekezaji kwa wanaotaka kuwekeza barani Afrika kwani
imedhamiria kukuza uchumi wake na kufikia wa kati ifikapo 2025 kwa
kupitia sekta ya viwanda. Pia ni nchi yenye amani na utulivu.
“Nchi
yetu imejaliwa kuwa na maliasili nyingi ambazo vilele ni malighafi kwa
viwanda kama vile mazao ya kilimo, misitu, bahari, maziwa, madini na
mbuga za wanyama ambazo ni kivutio cha watalii,” alifafanua Waziri Mkuu.
Leo
Oktoba 25, 2019 Mheshimiwa Majaliwa ataondoka nchini Urusi kwenda nchi
ya Azerbaijan ambako pia atamwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli
katika Mkutano wa Nchi zisizofungamana na upande wowote. Mkutano huo
ni wa siku mbili.
No comments:
Post a Comment