*****************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ameiomba Serikali ya Japan ikubali kutoa mafunzo zaidi kwa Madaktari
Bingwa wa upasuaji (Nephrologist Surgeon Specialist) na Madaktari
Bingwa (Nephrologist Physician Specialist) wa magonjwa ya figo na moyo
kutoka Tanzania ili kukidhi mahitaji makubwa ya madaktari hao nchini.
Waziri Mkuu amewasilisha ombi
hilo jana jioni (Septemba, 02, 2019) wakati alipozungumza na Mshauri
Maalum wa Masuala ya Afya wa Taasisi ya Tokushukai General Incorporated
Association iliyo chini ya Serikali ya Japan, Bw. Akio Egawa kwenye
uwanja wa ndege wa Narita nchini Japan akiwa njiani kurejea nyumbani.
Waziri Mkuu alisema hivi sasa
Tanzania ni kimbilio kwa nchi jirani katika tiba ya moyo na figo, hivyo
Madaktari Bingwa wa Upasuaji na Madaktari Bingwa wa magonjwa hayo
wanahitajika sana.
Alisema baada ya hospitali ya
Benjamini Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma kufanikiwa kupandikiza figo kwa
wagonjwa saba chini ya ufadhili wa Taasisi hiyo, nchi jirani pia
zinategemea kupata huduma hiyo nchini Tanzania, hivyo madaktari na vifaa
tiba zaidi vinahitajika Ili kujenga uwezo wa kuwahudumia wagonjwa wa
ndani na nje.
Waziri Mkuu aliishukuru
Serikali ya Japan kupitia Taasisi hiyo kwa misaada yake ambayo kwa
kiwango kikubwa imefanikisha kuanzishwa kwa tiba ya upandikizaji
figo katika hospitali ya Benjamin Mkapa ya Chuo Kikuu cha Dodoma.
“Nashauri uandaliwe utaratibu
wa kubadilishana watalaam ili Watanzania waende Japan kutibu wagonjwa na
Wajapan waje nchini kufanya kazi kwenye hospitali zetu lengo likiwa ni
kubadilishana ujuzi na kuongeza uzoefu.”
Pia, Waziri Mkuu alimkaribisha
nchini Tanzania Bw. Egawa ili aweze kuona mwenyewe maeneo mengine
ambayo Taasisi anayoiongoza inaweza kusaidia ili kuifanya nchi yetu
kuwa na uwezo mkubwa katika tiba ya uapandikizaji wa figo Barani Afrika.
Waziri Mkuu alisema amefurahi
kufahamu kuwa Bw. Egawa ameishi Tanzania kwa miaka mitatu akifanya kazi
kwenye ubalozi wa Japan uliopo Dar es Salaam, hivyo anaifahamu vizuri
Tanzania na anajua umuhimu na mahitaji ya huduma za afya nchini na
anafahamu mikakati Serikali kuhusu kuboresha huduma za afya.
Kwa upande wake, Bw. Egawa
alimwahidi Waziri Mkuu kuwa Taasisi yake iko tayari kuunga mkono juhudi
za Serikali ya Tanzania inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli kwa
kuendelea kusaidia hospitali ya Benjamin Mkapa ili kuiimarisha na
kuiwezesha kufanya vizuri zaidi katika huduma ya tiba ya figo na moyo.
Alisema taasisi yake iko tayari kuendelea kutoa ushirikiano na Serikali
ya Tanzania.
No comments:
Post a Comment