Friday, September 13, 2019

WASIMAMIZI WA UCHAGUZI SERIKALI ZA MITAA SIMIYU WAAPISHWA, WAASWA KUZINGATIA SHERIA, KANUNI NA MIONGOZO KUEPUSHA MALALAMIKO

Msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, katika Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi, Eng. Wilbert Siogopi Makala akila kiapo mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio(kushoto), zoezi ambalo limefanyika Septemba 12, 2019 Mjini Bariadi na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini,(kushoto walioketi) akiwa katika picha ya pamoja na Wasimamizi wa chaguzi wa Serikali za Mitaa baada ya wasimimizi hao kuapishwa ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio(kushoto), zoezi ambalo limefanyika Septemba 12, 2019 Mjini Bariadi na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
Bi . Amina Mbwambo msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima akizungumza kwa niaba ya wenzake  mara baada ya kuapishwa ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio(kushoto), zoezi ambalo limefanyika Septemba 12, 2019 Mjini Bariadi na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio(kushoto) akizungumza na wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mara baada ya kuwaapisha Septemba 12, 2019 Mjini Bariadi na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Bariadi, Bw. Melkizedeck Humbe akitoa neno kwa wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ambao waliapiswa Septemba 12, 2019  Mjini Bariadi na   Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio na kushuhudiwa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini.
********************************

Na Stella Kalinga, Simiyu RS
Wasimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa utakaofanyika Novemba 24, 2019 kutoka katika Halmashauri sita za Mkoa wa Simiyu wameapishwa Septemba 12, 2019 Mjini Bariadi, ambapo Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bw. Jumanne Sagini amewataka wazingatie sheria, kanuni, taratibu na miongozo katika uchaguzi huo ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima.
Sagini amesema wasimamizi hao  wanapaswa kutambua kuwa wamepewa jukumu zito ambalo linahitaji umakini wa hali ya juu na utulivu wa akili, hivyo ni vema wakasoma na kuzipitia tena sheria, kanuni na miongozo ya uchaguzi wa Serikali za Mitaa walizopewa ili wazielewe na waweze kufanya kazi bila kubabaika.
“Kumbukeni kuwa Uchaguzi huu unaweka msingi na maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 hivyo ni imani yangu kuwa kila mmoja wenu atakahakikisha anazingatia sheria, kanuni,miongozo na taratibu zilizotolewa ili kuepusha malalamiko yasiyo ya lazima; matarajio yangu ni kwamba mtaishi viapo mlivyoapa leo” alisema Sagini.
Aidha, Sagini amewataka wasimamizi hao kujiepusha na ushabiki wa kisiasa kwa kuwa wao kama wasimamizi ni waamuzi, hivyo hawapaswi kwa namna yoyote kujihusisha na masuala ya ushabiki wa vyama vya kisiasa, ili waaminiwe kuwa wanaweza kutoa haki; watakaobainika kujihusisha na itikadi za kisiasa watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Akizungumza mara baada ya kuwaapisha wasimamizi hao, Hakimu Mkazi Mfawidhi Mwandamizi wa Mahakama ya Wilaya ya Bariadi, Mhe. Mary Mrio amewataka wasimamizi hao kuishi viapo vyao na kuhakikisha wanafanya majukumu yao kwa uadilifu na kwa mujibu wa sheria kwa sababu watakapokiuka sheria , kanuni na taratibu wataiingiza serikali kwenye gharama.
Kwa upande wao wasimamizi wa uchaguzi wa Serikali za Mitaa mkoani Simiyu mwaka 2019 wamesema watahakikisha wanatekeleza wajibu na majukumu waliyopewa kwa mujibu wa sheria, kanuni, taratibu na miongozo kama walivyoelekezwa.
“Tunashukuru kwa kuaminiwa katika jukumu hili nyeti la Kitaifa, tunaamini kama tulivyoelekezwa kama wasimamizi tutasimamia yale tunayopaswa tutafanye kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na tutaviishi viapo vyetu tulivyoapa siku ya leo na kutimiza wajibu wetu kama watumishi wa Umma” alisema Wilbert Siogopi msimamizi wa Uchaguzi Halmashauri ya Wilaya ya Bariadi.
“Tunaahidi kwamba tutakitekeleza kiapo tulichoapa leo, tunafahamu kuwa kazi hii ngumu lakini kama mlivyotuasa tukiamua kwa dhati kabisa tukapitia sheria, kanuni, taratibu na miongozo ya uchaguzi tutafanya kazi inayotarajiwa” alisema Bi . Amina Mbwambo msimamizi wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa katika Halmashauri ya Wilaya ya Itilima.
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 24, 2019 nchini kote ambapo katika Mkoa wa Simiyu utahusisha  Vijiji 470, Mitaa 92 na Vitongoji 2652.

No comments:

Post a Comment