Mkuu
wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo baada ya kukagua mtambo wa kuponda kokoto
zitakazotumika kwenye ujenzi wa vihenge katika eneo la maalum la viwanda la
Kanondo.
Mkuu
wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amesifu ujenzi wa vihenge vya kuhifadhia
chakula unaoendelea kujengwa katika eneo maalum lililotengwa na Manispaa ya
Sumbawanga kwaajili ya uwekezaji wa viwanda pamoja na maghala lililopo Kanondo
katika Kata ya Ntendo na hivyo kuwataka wamiliki wengine walionunua viwanja
katika eneo hilo kuhakikisha wanawekeza ili kuongeza ajira.
Amesema
kuwa ujenzi huo wa vihenge ni mkubwa na unagemewa kutoa ajira mbalimbali na
hivyo kuwataka wananchi wa mji wa sumbawanga na maeneo mengi ya Mkoa
kutoa kuchangamkia fursa ya ajira katika ujenzi utakaogharimu karibu shilingi
bilioni 15 na hivyo kuwataka Wakala wa Taifa wa hifadhi ya Chakula (NFRA)
Sumbawanga kuhakikisha wanasimamia vizuri kwa msaada na ushauri kutoka Wakala wa
Majengo Tanzania wakihakikisha mkandarasi hafanyi makosa.
“Tulichelewa
kuanza huu ujenzi lakini tulitaka huu ujenzi wa vihenge uje katika eneo hili la
viwanda la Kanondo, Hii kazi naona mmeanza vizuri pamoja na kuchelewa tangu
mwezi wa saba, tunategemea mwezi wa saba mwakani hivi vihenge sita viwe
vimekamilika pamoja na ghala lake moja na uwezo wa vihenge pamoja na ghala ni
kuhifadhi tani 26,000 na vikikamilika NFRA watakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani
59,500 hii ni mara mbili ya uwezo tulionao sasa hivi, hivyo tunawahamasisha
wakulima walime mahindi kwa wingi, uhakika wa soko upo,” Alisisitiza.
Wakati
akitoa taarifa ya ujenzi huo Meneja wa NFRA kanda ya Sumbwanga Abdillah
Nyangasa alisema kuwa NFRA wana maghala katika maeneo matatu ndani ya mkoa wa
Rukwa moja likiwa Halmasharu ya Wilaya ya Sumbawanga katika mji mdogo wa Laela
na mawili yakiwa katika Manispaa ya Sumbawanga katika eneo la Mazwi pamoja na
eneo la Kanondo.
“Kwa
upande wa Mazwi tuna maghala yenye uwezo wa kuhifadhi tani 18,500 ambapo hali
yake mengi ni machakavu yanahitaji ukarabati pia mazwi hapo hapo tuna ghala la
tani 4000 ambalo nalo ni chakavu na lilitakiwa kufanyiwa ukarabati kama mradi
huu ungefanyika pale lakini hapo mazwi kuna maghala mawili ya tani 3000 na
kufanya tani 6000 ambayo hayo hayahitaji ukarabati na ndipotulimohifadhia
mahindi, lakini kuna ghala la Laela ambalo lina uwezo wa kuhafadhi tani 5000
hili linahitaji ukarabati kidogo kwa ndani, lakini pia kuna mradi huu mpya wa
kanondo,” Alisema.
Kwa
upande wake Mkurugenzi wa manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisema kuwa
Eneo hilo la Viwanda na maghala lina viwanja 103 na viwanja 43 tayari
vimeshauzwa na kuongeza kuwa ujio wa ujenzi wa vihenge hivyo utasaidia kuongeza
thamani ya eneo hilo kwasababu ilikuwa inaonekana miundombinu bado haijafika
lakini kutokana na ujenzi wa vihenge hivyo halmashauri imefanikisha kufikisha
umeme na maji katika eneo hilo na kuongeza kuwa Manispaa inamradi mkubwa wa
maji unaotarajiwa kusambaza maji katika eneo hilo.
“Tunawaomba
wananchi wa Sumbawanga na wawekezaji kutoka nje kuja kuwekeza kwani sasa eneo
letu lipo hai na limeanza kufanyiwa kazi, waje wawekeze viwanda mbalimbali,
hata wafanyabiashara wetu wa pale mjini lakini mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa
kuongeza tunategemea nasi Manispaa kuchukua viwanja viwili ambapo tutajenga
sehemu kwaajili ya wafanyabiashara wadogowadogo walipo pale mjini waweze
kuhamia hapa,” Alimalizia.
Ujenzi
huo wa vihenge vipya vya kisasa unaojengwa na mkandarasi Elerai Construction
Company Limited kwa ufadhili wa Serikali ya Poland wenye thamani ya Shilingi
bilioni 13.6 unatarajiwa kumalizika mwezi July, 2020 na kuongeza uwezo wa
kuhifadhi chakula kutoka tani 33,500 za sasa hadi kufikia tani 59,500 na hivyo
kuongeza ununuzi wa zao la mahindi wa NFRA kutoka kwa wakulima.
No comments:
Post a Comment