***************************
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
ameiagiza Wizara ya Maji ifuatilie utendaji wa Mamlaka zilizopewa
dhamana ya kusimamia miradi ya maji katika maeneo mbalimbali nchini na
ihakikishe kwamba bili wanazotozwa wananchi zinakuwa na uhalisia na si
kuwaumiza.
Ametoa agizo hilo baada ya kuibuka
wimbi la malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu upandaji wa bili za maji
ambao hauna uhalisia kwa sababu Serikali ndiyo inayotoa fedha za miradi
hiyo nchini.”Serikali haitakubali wala haitoruhusu mwananchi anatozwa
gharama kubwa za maji.”
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Alhamisi, Septemba 12, 2019) Bungeni jijini Dodoma katika kipindi cha
maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu wakati akijibu swali la
Mbungewa Viti Maalumu, Mariam Kisangi, aliyetaka kujua kauli ya Serikali
kuhusu suala hilo.
“Yako maeneo ambayo mamlaka
zilizopewa dhamana ya kusimamia miradi ya maji kumejitokeza wimbi la
mabadiliko ya kuhusu kupanda kwa bei za bili, mfano wilayani Maswa
mkoani Simuyu bei imeongezeka kutoka sh. 5,000 hadi 28,000 kwa mwezi.”
“Bei hizo hazina uhalisia na
hakuna sababu ya mamlaka kuzoza bei kubwa kiasi hicho na kuwafanya
wananchi washindwe kumudu kulipia bili zao, wakati Serikali ndio imetoa
fedha za kugharamamia uanzwishwaji wa miradi hiyo na haijadai
kurudishiwa fedha hizo.”
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Maji
kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) ifuatilie bei za
bili wanazotozwa wananchi ili kujiridhishwa kwamba zinazingatia uwezo
wa wananchi wengi kuzilipa hasa wale wa vijijini.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu
amewaagiza Wakuu wa Mikoa, Wilaya, Wakurugenzi wa Halmashauri, Maafisa
Kilimo na Maafisa Biashara kote nchini wasimamie katika masoko yote na
wajirishe iwapo vipimo vinavyotumika ni sahihi kwani lumbesa
haikubaliki.
Ametoa agizo hilo wakati
akijibu swali la Mbungewa Jimbo la Mlalo, Rashid Shangazi aliyetaka
kupata kauli ya Serikali kuhusu hatua zilizochukuliwa katika kudhibiti
unyonyaji wanaofanyiwa wakulima kupitia ufungaji wa mazao unaozidi
viwango.
Waziri Mkuu amesema wanunuzi
wa mazao mbalimbali lazima wafuate sharia, kanuni na taratibu za
manunuzi ya mazao husika. “Maafisa Kilimo wasimamie biashara hiyo na
waendeshe operesheni kwenye maeneo ya masoko ili kujirishana vipimo
vinavyotumika.”
Amesema ni muhimu zaidi
kutumia mizani ambayo haina utata ili kuwawezesha wakulima kuweza
kunufaika kutokana na kilimo na kwamba suala la waununuzi kutumia vipimo
visivyosahihi kama lumbesa halikubaliki.
Akijibuswali la Mbunge wa Sumve,
Richard Ndasa aliyetaka kupata kauli ya Serikali kuhusu kuhusu suala la
ununuzi wa zao la pamba, Waziri Mkuu amesema Serikali imelifanyia kazi
suala hilo na tayari zaidi ya tani 200,000 zimeshanunuliwa ambayo ni
sawa na asilimia 80.
Waziri Mkuu amewahakikishia wakulima wa zao la pamba kwamba pamba yote iliyosailia majumbani itanunuliwa.
No comments:
Post a Comment