Friday, September 27, 2019

Shaka: Tunashiriki uchaguzi kwa kujiamini na tutashinda



Watendaji wa chama hakuna kulala 

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Chama cha Mapinduzi ( CCM) Mkoa wa Morogoro kimejianda vyema na kusema kipo tayari kushiriki uchaguzi wa serikali za Mitaa, Vijiji na Vitongoji kwani ndio kitovu cha kushika hatamu za utawala wa dola hivyo kitaheshimu sheria na matakwa ya demokrasia.

Kimesema Uchaguzi huo licha ya kuwa ni muhimu na kipimo cha kuaminiwa kwa vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu mwaka 2020,CCM na serikali zake hakina sababu za kushindwa .

Hayo yameelezwa jana na Katibu wa CCM mkoa Morogoro Shaka Hamdu Shaka wakati akitoa tathimini ya zoezi la uchukuaji fomu za kuomba kuteuliwa na chama kugombea nafasi ya vitongoji alipokuwa akizungumza na viongozi wa kata, matawi na mashina morogoro mjini na kuwataka kuendelea kujipanga, kufuata, kanuni, taratibu za kisheria na kikatiba zilizowekwa na Serikali.

Shaka alisema kila kiongozi wa CCM ana wajibu wa msingi kuhakikisha chama kinapitisha wagombea wenye weledi na sifa, wanaokubalika kwenye jamii na watakaokuwa tayari kuwatumikia wananchi. 

Alisema wakati uchaguzi huo ukifanyika Novemba mwaka huu, serikali za CCM zimejitahidi vya kutosha kuimarisha huduma za kiwajibu kwa jamii, kuinua uchumi na kushughulikia kero sugu na kuzitatua. 

"Nawapongeza sana makatibu wa wilaya, kata na matawi hamasa na mwitikio kwa wanaccm umekuwa mkubwa katika kuchukua fomu za vitongoji ndani ya chama tunaendelea kusisitizana kuwa Uchaguzi huu ni muhimu kwa mustakabali wa chama. Mtendaji yeyote wa chama atakayezembea atahesabiwa ni msaliti na amekihujumu chama. Usaliti na hujuma si sifa njema bali dhambi isiosameheka" Alisema shaka

Aidha amewakumbusha watendaji hao wa chama muda wote kuzingatia maelekezo ya kikanuni na kisheria kuhusu usimamizi na kufuata taratibu, miongozo na kanuni za chama na Serikali ili kutimiza dhana ya demokrasia kivitendo.

"Viongozi wa kata, matawi chama na jumuiya sambamba na viongozi wa chama ngazi za vijiji, mitaa na vitongoji lazima msimame pamoja zisimame pamoja na mfanye kazi usiku na mchana bila kuchoka wote kwa umoja wenu na mshikamano mjitume kama wafanyavyo siafu ili tushinde vizuri ili kulinda heshima ya Rais Magufuli mbele ya macho ya dunia" Alisisitiza Shaka .

Alisema CCM inajua kina sifa za kushinda kwakuwa siku zote kimekuwa mstari wa mbele kuheshimu na kufuata taratibu lakini mahasimu wao kisiasa alidai wanajiandaa kwa ulalamishi na uzushi wa kutengeneza baada kupotezea muelekee na kupoteza dira kisiasa.

Katibu huyo aliwaeleza watendaji wake kazi na dhamana ya kuwatumikia wananachi kimepewa CCM hivyo kuwaachia wengine hatua hiyo itahesabika ni makosa kisiasa kiufundi na kihistoria

"Tunashiriki uchaguzi kwa kujiamini tutashinda kwa haki usawa na amani. CCM mkoa wa morogoro Tunaahidi kufuata taratibu zote za kikanuni na kikatiba. Tutakaposhindwa tutaheshimu matokeo na wenzetu pia wawe waungwana wa kutii matakwa na uamuzi wa wananchi "Alisema Shaka 

Source Majira, mtanzania

No comments:

Post a Comment