Thursday, September 26, 2019

SERIKALI YADHAMIRIA KUKIFUFUA KIWANDA CHA MPONDE -MHE MGUMBA





Mhe. Naibu waziri wa Kilimo Omary Mgumba amesema kuwa serikali imedhamiria kukifufu kwa haraka kiwanda cha Mponde alisema hayo alipofanya ziara ya kikazi katika Halmashauri ya Wilaya ya Bumbuli, mkoani Tanga ili kukagua maendeleo ya kilimo na kuskiliza changamoto za wakulima  mkoani humo.

Mgumba alisema kuwa Serikali itahakikisha kiwanda cha Mponde kinafufuliwa muda si mrefu baada ya taratibu za kisheria za ununuzi wa mitambo na vipuri vya kiwanda hicho utakapokamilika, hivyo wananchi wawe na amani.

Pia alisema kuwa, kiwanda hicho sasa ni mali ya serikali na mwekezaji ameshapatikana na ataanza ukarabati wa kiwanda muda si mrefu. Mifuko ya PSSSF na WCF itaendesha mradi wa kiwanda hicho wa zaidi ya shilingi bilioni 4.7 na wote watachangia asilimia 50 kila mmoja.

Vile vile alisema, Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) inatakiwa kufika Bumbuli ili kuweza kuwaelimisha wakulima kuhusu aina mikopo inayotolewa na benki hiyo ili kuwapatia mitaji ya kilimo cha chai, wakulima wasiache kulima chai kwa sababu bado ina soko kubwa sana duniani na pia waanzishe vyama vya ushirika ili waweze kuwa na nguvu ya pamoja katika shughuli zao za kilimo cha zao la chai.

Hayo yote ni kutokana na maelekezo aliyoyatoa Waziri Mkuu, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb.) siku ya tarehe 1/11/2018 alipotembelea kiwanda hicho cha chai cha Mponde.Kiwanda hicho kilifungwa kutokana na uchakavu wa mitambo, wakulima kutopata pembejeo na kupungua uzalishaji wa zao la chai kutokana na baadhi ya wakulima kukata tamaa kwa kukosa soko la uhakika.

Kuhusu elekezo la ufufuaji wa mashamba ya chai ya wakulima wadogo yaliyotelekezwa, Mhe. Naibu Waziri alijulishwa kuwa uhamashaji wa kufufua mashamba umefanyika katika Kata zote 14 zinazolima chai, hekta 562 zimeshafufuliwa kati ya hekta 800 sawa na 70.25% ya lengo. 

Kuhusu agizo la uundaji wa vyama vya ushirika vya msingi vya kilimo na masoko (AMCOS) kwa ajili ya zao la chai, Mhe. Naibu Waziri alijulishwa kuwa, jumla ya Kata 12 kati ya 14 zilihamasishwa kuunda ushirika na vyama vya ushirika 4 kati ya 8 vinavyojishughulisha na zao moja la kahawa vimeunganishwa na zao la pili la chai na jitihada za kuunganisha vyama vilivyobaki inaendelea.

Kuhusu agizo la mwisho la kuhusu kufanyika kwa tathmini ya awali ya gharama za ununuzi wa mashine, ukarabati wa mitambo na miundombinu ya kiwanda kwa ujumla, tathimini imeshafanyika na gharama za awali za kufufua kiwanda zimekadiriwa kuwa shilingi bilioni 2.7.

Katika ziara hiyo, Naibu Waziri huyo alikutana na wakulima wadogo wadogo wa zao la chai katika Kijiji cha Kweminyasa. Wakulima hao waliwasilisha baadhi ya changamoto zinazowakabili katika kilimo cha chai zikiwemo za uwepo wa viutalifu feki, ukosefu wa fedha za kununulia mbolea na pia uhaba wa soko la uhakika la majani mabichi ya chai kutokana na kufungwa kwa Kiwanda cha Chai Mponde kwa takribani miaka sita toka mwaka 2013.

No comments:

Post a Comment