Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 12 Septemba 2019 wakati wa mkutano wa kumi na sita wa Bunge la miswada Jijini Dodoma.(Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa
Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali bungeni leo tarehe 12 Septemba 2019 wakati
wa mkutano wa kumi na sita wa Bunge la miswada Jijini Dodoma.
Na
Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Dodoma
Upatikanaji
wa mbegu bora zikiwemo za mahindi ngano, maharage, mpunga, soya, alizeti,
mtama, ufuta, viazi mviringo na mbegu za mazao ya bustani kwa msimu wa 2018/19
ulifikia tani 49,040 kati ya hizo tani 38,507 sawa na asilimia 78.6
zilizalishwa nchini na tani 8,361 sawa na asilimia 17 ziliagizwa nje ya nchi na tani 2,171 sawa na asilimia 4.4 ni
bakaa ya msimu wa 2017/2018.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe ameyasema hayo leo tarehe 12 Septemba 2019 wakati akijibu swali la Mbunge
wa Kasulu Mjini Mhe Daniel Nsanzugwanko mkakati wa serikali katika kutatua
uhaba mkubwa wa mbegu hasa za mahindi na maharage
ambayo ni mazao ya chakula na namna ambavyo serikali itajikita katika
uzalishaji wa mbegu.
Alisema kuwa Mikakati ya Serikali
ya kuongeza uzalishaji wa mbegu ni pamoja na kuwezesha Wakala
wa Mbegu za Kilimo (ASA) kuongeza uzalishaji wa mbegu bora katika mashamba ya
Mwele, Dabaga, Mbozi, Msimba, Bugaga na Arusha; kutumia Taasisi za Utafiti wa
Kilimo kuzalisha mbegu mama, msingi na zilizothibitishwa ubora na kukodisha
maeneo katika mashamba ya ASA kwa kampuni binafsi za mbegu ili kuongeza
uzalishaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali ikiwemo mahindi na maharage.
Aidha, mikakati mingine ni kuongeza
eneo la umwagiliaji katika mashamba ya mbegu ya Msimba, Arusha, Dabaga na mashamba ya Vituo vya Utafiti kutoka hekta 200 hadi
600;
kushirikisha taasisi za umma
kama Jeshi la Magereza na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kuzalisha mbegu bora
pamoja na vikundi vya wakulima wadogo
kuzalisha mbegu za Daraja la Kuazimiwa ubora.
Mhe Bashe
alisema kuwa shamba la mbegu la
Bugaga lililopo katika Wilaya ya Kasulu lina ukubwa wa hekta 200. Shamba hilo
linamilikiwa na ASA na kwa sasa linatumika kuzalishia mbegu bora za mahindi,
maharage na alizeti. Aidha, shamba hilo linatumika kuzalisha miche bora ya
michikichi, miche ya matunda ya machungwa na maembe.
Pia
serikali imeanza kuchimba kisima cha maji katika shamba hilo ili kuwezesha
uzalishaji wa mbegu kwa kipiti chote cha mwaka. Vilevile, ASA imejenga kitalu
nyumba cha kukuzia miche ya chikichi pamoja na kuandaa bustani ya kukuzia miche
hiyo ya michikichi na miche ya matunda.
Aliongeza
kuwa Mkakati wa Serikali ni kuongeza
uzalishaji wa mbegu ambapo Serikali katika mwaka wa fedha 2019/20 imetenga
takribani shilingi bilioni 13 kwa
ajili ya utafiti wa mbegu kupitia Taasisi ya Utafiti wa Mbegu-TARI na
uzalishaji wa mbegu kupitia Wakala wa Mbegu za Kilimo –ASA kwa ajili ya kuzalisha
mbegu kwa njia ya umwagiliaji ili kuongeza uzalishaji mara tatu hadi nne zaidi
ya sasa. "Aidha, nitumie fursa hii kuzisihi halmashauri kutotumia maeneo
yaliyotengwa kwa tafiti za kilimo kwa shughuli zingine ikiwemo kujenga stendi
za mabasi" Alikaririwa Mhe Bashe
Kadhalika,
Wizara ya Kilimo itaamua kuyaachia maeneo hayo kwa shughuli zingingine baada ya
kujiridhisha kwamba maeneo hayo hayana tija kwa shughuli hizo za kilimo.
Naye Naibu waziri wa Kilimo Mhe Omary Mgumba (Mb) akijibu swali la mbunge wa viti maalum Zaynab kuhusu serikali kutafuta
soko la zao la nazi alisema kuwa Soko la kudumu la zao la nazi lipo nchini kwa
sababu kiasi cha nazi kinachozalishwa bado hakikidhi mahitaji ya soko la ndani
ya nchi kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya zao hilo ikiwemo ulaji wa madafu
na watumiaji wa nazi.
Aidha, mafuta mwali yanayotokana na nazi yanaendelea kupata umaarufu
kutokana na uhitaji wake kuwa mkubwa ndani na nje ya nchi, ambayo lita moja
inafika hadi Shilingi 40,000/=. Bidhaa kama fagio, mbao, kamba na samani
zinazotokana na mti wa mnazi na uwezo wa zao hilo kutunza mazingira huongeza
thamani ya zao la minazi.
Alisema kuwa Katika kuimarisha soko la zao la nazi
nchini msimu wa mwaka 2018/2019 wakulima wapatao 74 katika mikoa ya Lindi na
Mtwara wamefundishwa namna ya kukamua mafuta mwali.
Vilevile, kikundi cha wanachama 50 katika Wilaya ya
Bagamoyo kimepewa mashine yenye uwezo wa kukamua lita 500 za mafuta mwali kwa
mwaka. Aidha, Serikali inaendelea kuimarisha masoko ya mazao yote ya kilimo
likiwemo zao la nazi kwa kuwaunganisha
wakulima na wanunuzi kupitia vyama vya ushirika, masoko ya moja kwa moja na
viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya
zao la nazi.
Mhe Mgumba amesema, Serikali inaendelea kutoa elimu
kwa wazalishaji wa zao la nazi kuendelea kupanda mbegu bora zenye ukinzani
dhidi ya magonjwa na zenye tija kubwa.
Tanzania ni nchi ya kumi duniani kwa uzalishaji wa nazi ikiongozwa na nchi ya
Indonesia na kwa Afrika ni nchi ya kwanza ambapo huzalisha wastani wa tani
530,000 za nazi kwa mwaka ikifuatiwa na Ghana ambayo huzalisha wastani wa tani 366,183.
Aidha, Serikali inaendelea kuhamasisha kilimo cha
minazi nchini ambapo imeanzisha shamba lenye ukubwa wa hekta 54 katika kituo
kidogo cha utafiti cha Chambezi Wilaya ya Bagamoyo ili kuzalisha miche
bora ya minazi yenye ukinzani dhidi ya
ugonjwa wa kunyong’onyea kwa minazi (Coconut Lethal Disease) na
kuisambaza kwa wakulima kwa gharama nafuu.
Aliongeza kuwa Serikali inahamasisha kilimo cha minazi
katika maeneo mapya ili kuongeza uzalishaji wa nazi nchini ambapo msimu wa
2018/2019 ilizalisha na kusambaza jumla ya mbegu 11,000 kwa wakulima katika
mikoa ya Rukwa na Mwanza. Aidha, Serikali inafanya mazungumzo na Jumuiya ya Asia
- Pasific Coconut Community (APCC) ambayo hutunza “germplasm” ya minazi
kuwezesha upatikanaji wa mbegu bora za minazi zenye kuongeza tija kwa wakulima.
MWISHO
No comments:
Post a Comment