Monday, September 30, 2019

Dkt.Kalemani : Msisubiri nguzo Lipieni Muunganishiwe Umeme

Moja ya kibanda cha biashara kilichofungiwa na kuwashwa umeme na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani, katika kijiji cha Dodoma, wilayani Chato mkoani Geita.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani,( kulia)akimpongeza kijana mwenye duka( aliyevaa t-shirt nyeupe) mara baada ya kuwasha umeme katika duka lake.
Baadhi ya wanakijiji cha wakimsikiliza Waziri wa Nishati , Dkt. Medard Kalemani wakati akifanya harambee ya kuchangia ujenzi wa zahanati ya kijiji hicho.
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani( katikati) akipiga makofi mara baada ya kuweka jiwe la msingi katika zahanati ya kijiji cha Nyisanze wilayani Chato Mkoani Geita.
Wasanii wa kikundi cha Zakia wakitumbuiza wakati wa kuwashiwa umeme katika kijiji cha Dodoma wilayani Chato Mkoani Geita.
*******************************
Zuena Msuya, Geita
Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani amewaambia wananchi wanaoishi vijijini waache kulalamika badala yake walipie gharama ya umeme ili waunganishwe na huduma hiyo kwa kuwa itafika kote nchini.
Dkt. Kalemani alisema wanavijiji wasisubiri nguzo kuwafikia katika maeneo yao ndipo wakalipie, bali walipie sasa na kusuka nyaya katika nyumba zao kwa kuwa umeme utaunganishwa katika kila kaya bila kubagua aina ya nyumba.
Aliyasema hayo, Septemba 29,2019 katika kijiji cha Dodoma wilayani Chato, Mkoani Geita, alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya usambazaji umeme vijijini na kuwasha umeme katika kijiji hicho.
Kuhusu suala la wananchi kusubiri nguzo zifike katika maeneo yao ndipo wakalipie,Dkt. Kalemani alieleza kuwa kwa kufanya hivyo ni kuchelewesha zoezi la kuwaunganishia wananchi huduma ya umeme, kwa kuwa lengo kupitisha miundombinu katika makazi ya watu ni kuwaunganisha umeme wananchi wengi wa vijijini.
Dkt. Kalemani alieleza kuwa vijiji vingi nchini vimepitiwa na miundombinu ya mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini, lakini wananchi wamekuwa na mwamko mdogo wa kulipia shilingi 27,000, pia wamekuwa wakilalamika kuwa hawajapata umeme.
“ Ndugu zangu mnalalamika sana kuhusu umeme, mkiulizwa kama mmelipia mnasema bado, mnasubiri nguzo, suala la nguzo haliwahusu ninyi wanavijiji, kinachowahusu ni kutandaza nyaya katika majumba yenu na kulipia gharama,sasa kama mmefanya hivyo na kukosa umeme ndiyo malalamike”, alisisitiza Dkt. Kalemani.
Aidha aliendelea kuwakumbusha wananchi kuwa huduma ya umeme wanayofungiwa, mbali na kuwapatia mwanga pia waitumie fursa hiyo kujiongezea kipato kwa kuanzisha viwanda vidogo na biashara mbalimbali.
Alisisitiza kuwa mwananchi asikubali kulipia gharama zaidi ya shilingi elfu 27,000/= na kwamba ni vifaa kama nguzo, nyaya, mashine ya LUKU pamoja na transifoma hutolewa bure kwa wananchi wote walio vijijini na waliopitiwa na Mradi wa Usambazaji Umeme Vijijini( REA).
Katika hatua nyingine, Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani ambaye pia ni Mbunge wa Chato, aliweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Zahati ya Kijiji cha Nyisanze wilayani Chato mkoani Geita ambayo pindi itakapokamilika itawapunguzia adha ya kutembea umbali mrefu wananchi wa kijiji hicho na maeneo jirani kwenda kufuata huduma za afya.
Ujenzi wa Zahanati hiyo umefikia hatua ya kupaua, ambapo pamoja na mambo mengine aliendesha harambee ya kuchangia fedha pamoja na vifaa mbalimbali kama vile Nondo, Matofali, na Mifuko ya Saruji inayohitajika ili kukamilisha ujenzi huo.
Hata hivyo katika harambee hiyo, aliweza kupata vifaa vyote vinavyohitajika katika kumalizia ujenzi wa zahanati hiyo kutoka kwa wageni mbalimbali waliohudhuria mkutano huo pamoja na wananchi, zahanati hiyo inatarajiwa kukamilika hivi karibuni.

No comments:

Post a Comment