*************
WAZIRI MKUU,
Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na viongozi wa Kampuni
ya Toshiba nchini Japani, ambapo amewashawishi waje nchini na wafungue
ofisi kubwa na waanzishe viwanda vya bidhaa za elektroniki watakavyoona
vinafaa hapa nchini.
Waziri Mkuu
ameyasema hayo leo (Jumanne, Agosti 27, 2019) baada ya kutembelea
Makumbusho ya Sayansi ya Kampuni ya Toshiba na kiwanda cha kutengeneza
mitambo ya kuzalisha umeme cha Tsurumi kinachomilikiwa na Kampuni hiyo.
Akizungumza
na viongozi wa kampuni ya Toshiba, Waziri Mkuu amewashawishi waje nchini
na wafungue viwanda vya kutengeneza bidhaa mbalimbali za kielektroniki
kama vile redio, televisheni, pasi na viwanda vingine watakavyoona wao
vinafaa kujengwa nchini.
Waziri Mkuu
amewahakikisha viongozi hao kwamba hawatojuta kuwekeza nchini Tanzania
kutokana na sera nzuri na mazingira mazuri ya uwekezaji na biashara
pamoja na soko la uhakika wa bidhaa zitakazozalishwa kwa kuwa Tanzania
imezungukwa na nchi nyingi.
“Wawekezaji
wote wanaokuja kuwekeza Tanzania wakiwemo na wa kutoka Japan pamoja na
kampuni ya Toshiba, watambue kwamba Serikali ya Awamu ya Tano imeboresha
mazingira ya uwekezaji na kuyafanya yawe rafiki, nina uhakika
wawekezaji watakaoamua kuwekeza Tanzania hawatajutia uamuzi wao huo”.
Waziri Mkuu
amesema ujio wa kampuni kubwa kutoka nchini Japan utawapa Watanzania
fursa ya kujifunza tekinolojia mpya na namna bora ya uendeshaji wa
biahsara unaozingatia viwango vya Kimataifa.
Kwa upande
wake, Mkurugenzi wa Makumbusho ya Sayansi ya Toshiba, Takano Lwakiri
amemwambia Waziri Mkuu kuwa Kampuni yake iko tayari kupanua ofisi yake
ya Tanzania na kufungua biashara, ambapo ameomba yafanyike mazungumzo
yatakayotoa dira sahihi ya kufanikisha jambo hilo.
Wakati huo
huo, Waziri Mkuu amezungumzia kuhusu Mkutano wa Saba wa Tokyo
International Conference on Africa Development (TICAD 7) utakaoanza
kesho Yokohama, nchini Japan, amesema anaamini kuwa utakuwa na mafanikio
makubwa kutokana na ajenda zilizoandaliwa.
Waziri Mkuu
amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni pamoja na kuhusu namna
ya kuunganisha kibiashara shughuli za Serikali na sekta binafsi.
Amesema kwa
kutumia mkutano huo wa TICAD 7 wafanyabiashara wa Tanzania wanayo fursa
ya kunufaika kwa kuunganisha nguvu zao na makampuni makubwa ya nchini
Japan kama Toshiba ili kupata uzoefu na teknolojia muafaka.
Hivyo, Waziri
Mkuu amewasihi wafanyabiashara kutoka Tanzania ambao watashiriki
mkutano huo wafanye mazungumzo na wenzao wa Japan, wawashawishi ili
waweze kushirikiana nao kwa ajili ya kuwekeza kwenye sekta mbalimbali.
Waziri Mkuu
yuko nchini Japan akimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli kwenye mkutano
wa TICAD 7 utakaoanza kesho, ambapo ameambatana na Waziri wa Mambo ya
Nje na Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Profesa Paramagamba Kabudi na
viongozi wengene wa Serikali na Taasisi za Umma.
No comments:
Post a Comment