Na Mwandishi Wetu, NAIROBI
TANZANIA imefanikiwa kutinga hatua ya mwisho ya mchujo wa kuwania tiketi
ya Fainali za Ubingwa wa Mataifa ya Afrika (CHAN) baada ya ushindi wa
penalti 4-1 dhidi ya Kenya jioni ya leo Uwanja wa Moi Kasarani mjini
Nairobi, Kenya.
Shujaa wa Taifa Stars leo alikuwa ni kipa mkongwe, Juma Kaseja
aliyerejeshwa kikosini baada ya miaka sita ambaye aliokoa penalti ya
Michael Kibwage.
Waliofunga penalti za Tanzania ni mabeki Erasto Nyoni, Paul Godfrey ‘Boxer’, Gardiel Michael na mshambuliaji Salum Aiyee.
Kenya walipata penalti moja tu, ambayo ilifungwa na Cliffton Miheso
Ayisi, huku nyingine wakikosa Michael Kibwage na Joash Achieng Onyango.
Sasa Tanzania itakutana na Sudan katika hatua ya mwisho ya mchujo wa
kuwania tiketi ya CHAN ya mwakani nchini Cameroon, mechi ya kwanza
ikichezwa Dar es Salaam Septemba 20 na marudiano Oktoba 18 Khartoum.
Kikosi cha Tanzania kilikuwa; Juma Kaseja, Paul Godfrey, Gardiel
Michael, Erasto Nyoni, Kelvin Yondan, Jonas Mkude, Frank Domayo/Salim
Aiyee, Salum Abubakar ‘Sure Boy’, John Bocco/Ayoub Lyanga, Iddi Suleiman
‘Nado’ na Hassan Dilunga/Abdulaziz Makame.
Kenya; John Oyemba, Philemon Otieno/Ibrahim Shambi, Cliffton Miheso,
Mike Kibwage, Joash Onyango, Dennis Odhiambo, Samuel Onyango, Kenneth
Muguna, Sydney Lokale/Enosh Ochieng, Whyvone Isuza na Duke Abuya/ David
Owino.
No comments:
Post a Comment