Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu (kulia), akiongoza kikao cha majumuisho kwa
wataalamu kutoka Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kuwasilisha
taarifa ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika la Maendeleo ya
Petroli Tanzania (TPDC) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA)
kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dodoma, Agosti 21,
2019. Kushoto ni Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara, Haji Janabi.
Naibu Waziri wa
Nishati, Subira Mgalu, akiongoza kikao cha majumuisho kwa wataalamu
kutoka Taasisi zilizo chini yake, mara baada ya kuwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dodoma, Agosti 21, 2019.
Wataalamu
mbalimbali kutoka Wizara ya Nishati na Taasisi zilizo chini yake, wakiwa
katika kikao cha majumuisho mara baada ya kuwasilisha taarifa ya
utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Shirika la Maendeleo ya Petroli
Tanzania (TPDC) na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa Pamoja (PBPA) kwa
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Dodoma, Agosti 21, 2019.
………………………………
Na Veronica Simba – Dodoma
Naibu Waziri wa Nishati, Subira
Mgalu, leo Agosti 21, 2019 aliongoza Ujumbe wa wataalamu kutoka wizarani
na taasisi zilizo chini yake, kuwasilisha taarifa za utekelezaji wa
miradi mbalimbali kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini.
Taarifa zilizowasilishwa katika
kikao hicho ni zinazohusu miradi inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo
ya Petroli Tanzania (TPDC) pamoja na Wakala wa Uagizaji Mafuta kwa
Pamoja (PBPA).
Akiwasilisha taarifa ya shirika
lake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Dkt James Mataragio, aliiambia Kamati
husika kuwa usambazaji wa gesi asilia majumbani na viwandani umeanza
katika maeneo ambayo tayari kuna miundombinu wezeshi. Ametaja maeneo
hayo kuwa ni Mtwara, Lindi, Pwani na Dar es Salaam.
“Uunganishwaji wa wateja
mbalimbali umefanyika ikiwemo wa viwandani na majumbani ambao wote
hutumia gesi kama nishati mbadala,” alieleza.
Dkt. Mataragio, alitaja viwanda
ambavyo vimesambaziwa gesi katika mikoa mbalimbali pamoja na vilivyo
mbioni kupatiwa huduma hiyo kuwa ni pamoja na Lodhia Steel, kiwanda cha
vigae cha Goodwill, Knauf Gypsum, Shreeji Silicates Tanzania Ltd, LN
Future Building Material Co. Ltd, Wuzhoe pamoja na Balstian Group of
Companies vya Mkuranga mkoani Pwani.
Alisema kwa Mkoa wa Dar es Salaam
ni kiwanda cha Coca Cola, Polypety, Interchick, Chemi & Cortex,
ESTIM Construction pamoja na Hoteli zilizopo maeneo ya Mbezi Beach.
Aidha, amesema kingine ni kiwanda cha saruji cha Dangote kilichopo
mkoani Mtwara.
Akizungumzia usambazaji wa gesi
asilia majumbani, alisema zoezi hilo linaendelea katika mikoa ya Dar es
Salaam, Mtwara na Lindi na kwamba lengo ni kufikia nyumba za awali 233,
Dar es Salaam na 125 Mtwara ifikapo Oktoba mwaka huu.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa
PBPA, Erasto Simon, aliieleza Kamati hiyo ya Bunge kuwa matumizi ya gesi
ya kupikia kwa hapa nchini yameongezeka kufikia tani 8,000 kwa mwezi
kutoka tani 4,000 kwa mwaka mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Alisema serikali imeendelea
kuchukua hatua mbalimbali kuboresha biashara na matumizi ya gesi ya
kupikia hapa nchini ikiwemo hatua kubwa ya mpango wa kuagiza gesi hiyo
kupitia mfumo wa uagizaji kwa pamoja.
“Mfumo huo utasaidia sana katika
kupata gharama halisi za uagizaji hivyo kusaidia upangaji wa bei yake
nchini, Vilevile, utaongeza ufanisi katika matumizi ya miundombinu ya
kupokelea gesi hiyo. Pia, mfumo utasaidia kupungua kwa gharama kutokana
na kuagiza kwa pamoja hivyo kupunguza bei yake,” amefafanua.
Kikao hicho ni mfululizo wa vikao
vya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini vilivyoanza Agosti 20 na
kutarajiwa kukamilika Agosti 24 ambapo Wizara ya Nishati na Taasisi zake
zinawasilisha taarifa mbalimbali kuhusu miradi ambayo zinatekeleza.
No comments:
Post a Comment