Na.Alex Mathias,Bahi
KIONGOZI wa mbio za Mwenge wa
Uhuru 2019 Mzee Mkongea Ally amezindua na kuweka mawe ya msingi miradi 6
yenye thamani ya sh bil 8.7 katika halmashauri ya Bahi huku akiwataka
viongozi na wananchi kuilinda miradi hiyo ili idumu.
Baadhi ya miradi hiyo ni ujenzi wa
maboma manne katika shule ya sekondari ya Mundemu uliowekwa jiwe la
msingi,mradi wa usambazaji maji kijiji cha Mkakatika na kuweka jiwe la
msingi katika ujenzi wa barabara ya km 2.3 katika mji wa Bahi ikiwa ni
utekelezaji wa ahadi aliyowahi kuitoa Rais dkt John Magufuli wakati wa
kampeni 2015.
Akizungumza baada ya kukagua
miradi hiyo Mkongea amesema Rais Dkt John Magufuli anatumia fedha nyingi
kupeleka kwenye miradi ili iwasaidie wananchi hivyo ni wajibu wa kila
mmoja kuilinda.
“Katika mradi huu wa maji wa
Mkakatika tumetumia muda mrefu kujiridhisha ili tuone thamani ya fedha,
na baada ya ukaguzi huo tumeridhishwa na natamka kwamba Mwenge wa Uhuru
2019 umeridhia kuweka jiwe la msingi mradi huu,”amesema Mkongea.
Pamoja na kuridhia kuweka jiwe la
msingi ametoa maelekezo ikiwemo kuhakikisha mkandarasi wa ujenzi
anapeleka vipimo katika maabara ya serikali.
“Mradi huu nimeambiwa bado
haujakamilika, hivyo nisisitize mambo mawili, moja kuhakikisha fedha
zilizobaki zinatumika kukamilisha mradi huu, pili mkandarasi ahakikishe
anapitisha vipimo vyote katika maabara ya serikali,”ameongezea Mkongea.
Akikagua ujenzi wa hospitali ya
wilaya Mkongea amewapongeza na kusema ujenzi huo umetekelezwa vizuri na
thamani ya fedha imeonekana.
Amesema ametembelea ujenzi wa
hospitali nyingi zilizopewa sh bil 1.5 lakini nyingine bado ndio
wanapaua na kusema kuwa Bahi ni hospitali ya kwanza kati ya zote
alizotembelea.
Kwa upande wake mkuu wa wilaya ya
Bahi Mwanahamisi Munkunda amewashukuru wananchi kwa ushirikiano
waliouonyesha wakati wa utekelezaji wa miradi hiyo.
“Mafanikio tunayoyapata yanatokana
na ushirikiano wa wananchi na ushirikiano uliopo baina yetu sisi
watumishi, tukuahidi kufanyia kazi maelekezo yote,”alisema Mkuu wa
wilaya huyo
Mwenge wa Uhuru pia ulitembelea
mradi wa utunzaji wa chanzo cha maji na uhifadhi wa msitu wa Chenene
uliopo kijiji cha Mayamaya, uliweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha
kokoto katika kiwanda cha kokoto cha kampuni ya KASCCO.
No comments:
Post a Comment