Mkurugenzi
wa Halmashauri ya Wilaya ya Msalala Bw. Simon Berege (kushoto)
akimwonesha Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein
Mwinyi eneo la ujenzi wa Makao Makuu ya Halmashauri hiyo mapema leo
tarehe 30 Agosti, 2019 katika kata ya Ntobo.
Kaimu Mkurugenzi wa SUMA JKT
Kaptain Fabian Buberwa (kulia) akimuelezea Waziri wa Ujenzi na Jeshi la
kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi namna wanavyotekeleza mradi wa
kujenga makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala. Kulia ni Mkuu
wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Mhe. Zainab Telack wakiangalia ujenzi wa Makao Makuu ya
Halmashauri ya Wilaya ya Msalala leo tarehe 30 Agosti, 2019.
Sehemu ya ujenzi wa majengo ya Makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala inavyoonekana.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi pamoja na Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga Mhe. Zainab Telacl na viongozi wengine wakiendelea kukagua
ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi akizungumza na viongozi na
watendaji katika eneo la ujenzi wa makao makuu ya Halmashauri ya Wilaya
ya Msalala.
****************
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la
Kujenga Taifa, Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi amesema anaridhishwa na kazi
nzuri inayofanywa na miradi inayotekelezwa na SUMA JKT kanda ya Ziwa.
Dkt. Mwinyi akiwa kwenye ziara
yake ya kukagua miradi inayotekelezwa na SUMA JKT pamoja na makampuni
mengine yaliyo chini ya Wizara hiyo kanda ya Ziwa mapema leo tarehe
30/08/2019 katika Wilaya ya Kahama, Mkoa wa Shinyanga amesema kwa
kiwango kikubwa ameridhishwa na kazi zinazofanywa na sehemu kubwa kazi
zimekwenda kwa kiwango kinachotarajiwa na kuwa changamoto zilizopo
zitafanyiwa kazi.
“Niwahakikishie Mikoa na
Halmashauri zinazohusika na miradi inayotekelezwa na SUMA JKT changamoto
zote zitafanyiwa kazi” amesema Dkt. Mwinyi.
Aidha, amemshukuru Mhe. Rais John
Magufuli kwa kuiamini kampuni hiyo iliyo chini ya Wizara yake na ndiyo
sababu ya yeye kufanya ziara hiyo ili kuhakikisha imani hiyo inadumu
pamoja na kuwaomba viongozi wote wa Mikoa na Halmashauri kuendelea
kuiamini.
Aidha, amewataka SUMA JKT kuongeza
kazi ya ziada mara watakapopata fedha ili kukamilisha jengo la Makao
Makuu ya Halmashauri ya Wilaya ya Msalala ambalo ujenzi wake umesimama
kutokana na changamoto ya fedha.
Naye Mkurugenzi wa SUMA JKT Kanali
Rajab Mabele amesema kuwa, kampuni hiyo imepiga hatua kubwa hasa katika
nyanja ya ujenzi lakini pia inajihusisha na kazi nyingine mbalimbali
ikiwemo kilimo na ufugaji.
Awali, akimkaribisha Dkt. Mwinyi
Mkoani hapa, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Zainab Telack amemuomba
kupitia kampuni ya SUMA JKT kuangalia jinsi ya kuwa na miradi ya kuvuna
maji ili wananchi waweze kujishughulisha na kilimo cha umwagiliaji.
“Pamoja na kiangazi kilichopo,
tunapata mvua nyingi sana na tunavuna mpunga unaoweza kulisha nchi yote,
sasa tuone namna bora ya kuvuna hayo maji na tayari baadhi ya wananchi
wameshaanza kuchimba mashimo makubwa ya kuvuna maji, tumeona kama Mkoa
tufanye hilo ili wananchi wetu waweze kupata mpunga” amesema Telack.
No comments:
Post a Comment