Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim
Wangabo (kushoto) akimkabidhi hati za viwanja viwili vya Baraza Kuu la
Waislamu Tanzania vilivyopo Manispaa ya Sumbawanga Shekhe wa Mkoa Shekh
Rashid Akilimali wakati wa hafla fupi ya Makabidiano hayo.
Picha ya pamoja ya Mkuu wa mkoa
wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (waliokaa katikati) pamoja na Katibu Tawala
Mkoa wa Rukwa Bernard Makali (wa pili Kutoka kulia) na Shekhe wa Mkoa
Shekh Rashid Akilimali (wa pili toka Kushoto) Kamati ya Ulinzi na Usalam
ya mkoa pamoja na viongozi wengine wa Wilaya na Halmashauri.
……………………………………………………………………….
Shekhe wa Mkoa wa Rukwa Shekhe
Rashid Akilimali amepongeza juhudi za serikali ya mkoa wa Rukwa chini ya
mkuu wa mkoa huo Mh. Joachim Wangabo kwa kuweza kufanikisha kupatiwa
viwanja viwili vyenye jumla ya ekari 18 vilivyopo katika Manispaa ya
Sumbawanga baada ya kupita miaka 13 ya mgogoro baina ya Taasisi hiyo na
uongozi wa serikali ya mkoa.
Amesema kuwa Serikali hii ya
awamu ya tano ndio inayotakiwa kwani inawajali wanyonge na kuwapa haki
wale wanaostahiki kupewa haki hiyo na kuongeza kuwa Rais Dkt. John Pombe
Magufuli kweli anajua kuwateua watu wake na hakukosea kumteua Mh.
Wangabo kuuongoza mkoa wa Rukwa
“Kwahiyo mheshimiwa nikushukuru
kwa niaba ya waislamu wa mkoa wa Sumbawanga, hili linatoka Moyoni kwangu
rasmi, miaka 13 leo tunakabidhiwa hati hizi, imetugonga mioyo, imeleta
farka ya jamii, unapomchangisha sadaka mtu halafu isionekane imefanya
kazi fulani anabaki anajenga hoja ambayo haipo, wewe ni mfano wa kuigwa
kwa wakuu wa mikoa wengine kwa jambo hili, lakini nitakuwa mnyimi wa
fadhila kutokumshukuru Mkurugenzi wa Manispaa, kijana Madhubuti kabisa
huyu, amejitoa muhanga akasema ardhi hii ipo na mtapata lakini kwa
usimamizia wako,” Alisisitiza
Aidha, Shekhe Akilimali alitumia
nafasi hiyo kuiomba radhi serikali ya mkoa kwa niaba ya waislam wa mkoa
huo katika eneo ambalo uongozi wa taasisi uliwakwaza katika kufuatilia
hati hizo na kuonekana ni tatizo katika ofisi za serikali.
Kwa upande wake Mh. Wangabo
alisema kuwa ni dhamana ya viongozi katika maeneo mbalimbali ya
kiutawala kuhakikisha kuwa hakuna migogoro baina ya serikali na wananchi
wanaoongozwa na kuongeza kuwa viongozi kwa namna yoyote ile ni lazima
wawe tayari kuitatua migogoro hiyo kwasababu madhara yake ni makubwa na
isiposhughulikiwa kwa wakati itapelekea kukosekana kwa utulivu na amani
na hatimae maendeleo yanadumaa.
“Tnapotatua migogoro ya namna hii
tunawezesha serikali kupita hatua za kimaendeleo pamoja na wananchi kwa
ujumla wanapiga hatua za kimaendeleo, mgogoro huu wa viwanja umekuwepo
tangu miaka hiyo ya 2006, miaka mingi sana lakini sasa leo tumekata
mizizi ya fitina, tunaamini kabisa kwamba kuanzia sasa hivi tutakwenda
kwa amani na utulivu na madhehebu ya dini zote sit u waislamu hata
wakristo ambapo nao kulikuwa na mgogoro mzito tangu 1985 ambapo nao
tumekwishautatua,” Alieleza.
Halikadhalika, Mh. Wangabo
alimuagiza Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga kufanya haraka katika
kuwafikisha viongozi hao wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania
(BAKWATA)katika maeneo hayo ambayo wamepatiwa hati ili waweze kutambua
mipaka yao huku kukiwa na muwakilishi kutoka ofisi ya Mkuu wa mkoa
pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga.
Awali akitoa taarifa ya mgogoro
huo Katibu wa BAKWATA Mkoa wa Rukwa Ust. Mohamed Adam alisema kuwa kuna
wakuu wa mikoa kadhaa ambao wamepita katika mkoa huo lakini hawakuweza
kujaaliwa kuumaliza mgogoro huo ambao umemalizika leo tarehe 30.8.2019
na kusisitiza kuwa jambo hilo litabaki kuwa historia kwa waislamu wa
Mkoa wa Rukwa.
“Sisi Waislamu wa Mkoa huu kwa
jambo hili ulilolifanya tutaendelea kukumbuka katika maisha yetu yote na
Mwenyezi Mungu akujaalie sana Mheshimiwa mkuu wa mkoa kwa alama hii
uliyoiweka katika mji wetu,” Alisema.
Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mhe.
Joachim Wangabo kwa niaba ya Serikali amekabidhi hati za Viwanja viwili
vyenye namba 50074 na 50075 kwa Shekhe wa Mkoa Shekhe Rashid Akilimali
kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA).
No comments:
Post a Comment