SERA YA VIWANDA YASAIDIA KUPUNGUZA TATIZO LA AJIRA
MKAZI wa kijiji cha Kabanga wilayani
Kasulu mkoani Kigoma, Leonard Nkamba anayejishughulisha na uchongaji wa
vyombo mbalimbali vya jikoni ameishukuru Serikali kwa kuanzisha sera ya
viwanda kwa kuwa imesaidia kupunguza tatizo la ajira nchini.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Julai 14,
2019) baada ya kukabidhiwa kiasi cha sh. milioni 2.5 na Waziri Mkuu,
Kassim Majaliwa ili aweze kuongeza mashine itakayomuwezesha kuchonga
bidhaa zenye ubora zaidi. Makabidhiano hayo yamefanyika mjini Kigoma.
Bidhaa anazochonga ni vikombe, chupa za
chai, hot pot kwa kutumia mti aina ya jakalanda. Mbali na kutengeneza
vyombo hivyo, pia mjasiriamali huyo ambaye ameajiri vijana watatu
anachonga vibao na kuandika ujumbe mbalimbali kwa kutumia unga wa ngano.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa fedha
hizo na Waziri Mkuu, mjasiliamali huyo amesema anaushukuru Umoja wa
Wanawake Tanzania (UWT) ambao uliona kazi zake na kumuagiza atengeneze
seti za vyombo kwa ajili ya zawadi za kumpelekea Rais Dkt. John
Magufuli.
“Uongozi wa UWT mkoa wa Kigoma Taifa
ulivutiwa na kazi zangu na kuniagiza nitengeneze chupa ya chai, vikombe
na hot pot kwa ajili ya kumpa zawadi Mheshimiwa Rais pamoja na Waziri
Mkuu ndipo Waziri Mkuu jana aliona kazi zangu na akavutiwa na bidhaa
ninazotengeneza ndipo akaniuliza kama kuna changamoto zinazonikabili
nikamwabia nahitaji mashine moja yenye thamani ya sh. milioni mbili na
nusu akasema umepata na leo sijaamini alivyoniita na kunikabidhi.
Namshukuru sana.”
Nkamata ametumia fursa hiyo kuwashauri
wananchi wengine hususani vijana waache kulalamikia suala la ukosefu wa
ajira na badala yake wajiunge katika vikundi vya ujasiriamali na
kuzalisha bidhaa mbalimbali ambazo wataziuza na kujipatia kipato.
Pia amewaomba Watanzania wajenge
utamaduni wa kutumia bidhaa mbalimbali zinazozalishwa na viwanda vya
ndani kwa kuwa vina ubora wa kutosha na pia watakuwa wanachangia kukuza
uchumi wa wajasiriamali na Taifa kwa ujumla. Amesema bidhaa
anazotengeneza ni rafiki wa mazingira kutokana na malighafi anazotumia.
Kwa upande wake Waziri Mkuu ametumia
fursa hiyo kuwasihi wananchi kujishughulisha na shughuli mbalimbali za
ujasiriamali ili waweze kujipatia kipato na kuondokana na umasikini. Pia
amesema Serikali ipo tayari wakati wowote watakapohitaji msaada.
Waziri Mkuu amempongeza mjasiriamali huyo
kwa bidhaa mbalimbali anazotengeneza ambazo ni nzuri na za kipekee.
Amesemma amefurahi kuona vikombe, chupa za chai pamoja na hot pot
zilizotengenezwa na Mtanzania kwa kutumia miti.
No comments:
Post a Comment