WAZIRI KIGWANGALLA AITAKA BODI YA UTALII TANZANIA KUTUMIA NJIA ZA KISASA ZA MAWASILIANO
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt.
Hamisi Kigwangalla akizindua rasmi Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) jijini
Dodoma. Bodi hiyo imeongezewa muda wa miaka 3 na Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Aprili 23 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Bodi ya Utalii
Tanzania(TTB) Jaji (Mst) Thomas Mihayo akizungumza wakati wa hafla fupi
ya uzinduzi wa Bodi ya Utalii Tanzania jijini Dodoma.
Viongozi wa Wizara ya Maliasili na Utalii
wakiongozwa na Waziri wa Maliasili na Utalii Dkt. Hamisi Kigwangalla
wakiwa katika picha ya pamoja na Wajumbe wa Bodi ya Utalii Tanzania mara
baada ya uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dodoma.
………………….
WMU – Dodoma
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt.
Hamisi Kigwangalla ameitaka Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) iwekeze zaidi
katika matumizi ya njia za kisasa za mawasiliano na mbinu rahisi zenye
gharama nafuu kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo hapa nchini.
Dkt. Kigwangalla ameyasema hayo jijini
Dodoma wakati akizindua rasmi Bodi hiyo iliyongezewa muda wa miaka 3 na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli Aprili
23 mwaka huu.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi
hiyo amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe
Magufuli kwa kuiongezea kipindi kingine cha miaka 3 na kuitaka bodi
hiyo iendelee kubuni na kuongeza mbinu mpya za kutangaza utalii
zitakazoleta tija na matokeo ya haraka.
Amewataka wajumbe wa Bodi hiyo kufanya
kazi pamoja na kushirikiana na taasisi nyingine za Wizara ili kuongezea
idadi ya watalii wanaoitembelea Tanzania akiweka msisitizo katika
matumizi ya mifumo ya kisasa ya mawasiliano ili kupanua wigo wa
kutangaza vivutio vya utalii kuliko ilivyo sasa.
“Bodi ya utalii mnapaswa kuona fursa
zilizopo na kutimiza majukumu mliyopewa kwa tija na ufanisi zaidi, namna
pekee ya kufikia malengo hayo ni lazima mtumie teknolojia na mbinu
rahisi za mawasiliano zenye gharama nafuu kutimiza majukumu yaleyale ya
kutangaza vivutio vya utalii kisasa zaidi” Amesisitiza.
Ameipongeza bodi hiyo kwa kazi nzuri
inayofanya ya kuendelea kuhamasisha shughuli za Utalii nchini na
kuongeza kuwa kati ya vitu vilivyo iletea heshima sekta ya utalii
Tanzania ni uwepo wa Kaulimbiu ya “TANZANIA UNFORGETTABLE” ambayo imekua
chachu kwa taifa hasa katika kuitangaza sekta hiyo kitaifa na
kimataifa.
Amesema kupitia kaulimbiu hiyo watalii
wengi wanaoitembelea Tanzania wataendelea kukumbuka mambo mazuri na
vivutio vizuri walivyoviona na kuendelea kuichagua Tanzania kuwa mahali
pao pa kufanyia utalii.
Aidha, ametoa wito kwa Bodi hiyo
kuendelea kuweka mazingira na kuongeza soko la bidhaa za utalii za
Tanzania nje ya nchi kupitia maonesho ya kimataifa na kuwa na mkakati wa
kulenga soko husika pamoja na kuonana na watu watakaouziwa bidhaa moja
kwa lengo la kukamata soko katika maeneo kadhaa.
Pia ameitaka Bodi hiyo kuweka mkakati
mahususi ya kukamata masoko mapya ya watalii kutoka nje ya nchi kutoka
nchi za Marekani, Hispania, Urusi na nchi za Falme za Kiarabu zikiwemo
za Dubai na Oman ambazo watu wake wakiwemo wasomi, wafanyabiashara,
wanamichezo na watu maarufu wanapenda kwenda mapumziko ya muda mrefu na
kutumia fedha nyingi kwa shughuli za utalii.
Katika hatua nyingine ameishauri Bodi
hiyo kuwatumia watu maarufu na mashuhuri wakiwemo wasanii na wanamichezo
watakaoalikwa mahususi kwa kazi maalum ya kutangaza utalii wa Tanzania.
“Licha ya changamoto ya ufinyu wa bajeti
tunaweza kuweka mikakati ya kutangaza vivutio vyetu kwa tija na rahisi
zaidi na kuifanya nchi yetu ijulikane na kuonekana na watu wengi , kuna
mikakati tunaweza kuifanya mara moja tu ikadumu kwa muda mrefu, kama
tukiwatumia watu mashuhuri wenye wafuasi wengi wakatembelea vivutio
vyetu tuna uhakika watu wengi zaidi watafuatilia ziara zao na kufuata
walichokichagua, lazima tuweke mikakati ya kuwaleta watu mashuhuri walau
5 kwa mwaka ambao sisi tutawaalika, tutapata mafanikio makubwa sana
ndani ya muda mfupi” Amesisitiza Dkt. Kigwangalla.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Maliasili
na Utalii, Mhe. Constatine Kanyasu akizungumza wakati wa uzinduzi wa
Bodi hiyo amemshukuru Rais kwa kuiongezea kipindi kingine cha miaka cha
miaka 3.
Amesema kuwa katika kipindi cha miaka 3
imefanya kazi kubwa licha ya changamoto mbalimbali inazokabiliana nazo
akisisitiza kwamba uwepo wa changamoto hizo ni uhalali wa kuwepo kwa
bodi hiyo.
Amesema kuzinduliwa rasmi kwa bodi hiyo
kutaifanya itekeleze majukumu yake kwa kasi kubwa zaidi akisisitiza
kwamba kupitia bodi hiyo sekta ya Utalii Tanzania itasonga mbele kwa
kasi kubwa zaidi.
Mhe. Kanyasu ameitaka bodi hiyo iongeze
juhudu ya kutangaza utalii na kupanua wigo wa kutangaza soko la utalii
ndani na nje ya nchi akisitiza akisisitiza kwamba bado kuna mazao mengi
ya utalii ambayo hayajavunwa na endapo bodi itafanya kazi yake ipasavyo
Tanzania itapata mafanikio makubwa kiuchumi.
Naye Mwenyekiti wa Mwenyekiti wa Bodi ya
Utalii Tanzania Jaji (Mst) Thomas Mihayo akizungumza mara baada ya
kuzinduliwa kwa Bodi hiyo amemshukuru Rais hiyo nafasi nyingine akiahidi
kwamba bodi yake itafanya kazi kwa kasi na bidii zaidi ili kutimiza
malengo ya kuitangaza Sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.
Jaji Mihayo amesema kuwa Bodi hiyo
itaendelea kutekeleza majukumu yake chini ya uongozi wa Wizara na
kuitangaza kikamilifu sekta ya utalii ndani na nje ya nchi.
Bodi hiyo yenye wajumbe 6 iliongezewa
muda wa kuhudumu wa miaka 3 na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli Aprili 23, 2019.
No comments:
Post a Comment