WANANCHI CHIBOLI KUFURAHIA SIKUKUU YA EID EL-FITR NA UMEME
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(kushoto) na Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde, wakifuatilia taarifa
mbalimbali zilizokuwa zikitolewa katika Kijiji cha Chiboli wilayani
Chamwino kabla ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Chiboli wilayani Chamwino
kabla ya kuwasha umeme katika Kijiji hicho.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(katikati), Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (kushoto kwa Naibu
Waziri), Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga (kulia kwa Naibu
Waziri) wakishangilia mara baada ya kuwasha umeme katika Kijiji cha
Chiboli wilayani Chamwino.
Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(katikati) akikata utepe kuashiria umeme kufika kwenye Kisima cha Maji
katika Kijiji cha Chiboli, wilayani Chamwino. Wa tatu kulia ni Mbunge wa
Mtera, Livingstone Lusinde na wa Pili kulia ni Mkuu wa Wilaya ya
Chamwino, Vumilia Nyamoga.
Zahanati katika Kijiji cha Chiboli
wilayani Chamwino ambayo imepata umeme kupitia mradi wa BTIP (kV 400)
uliosambaza umeme katika Vijiji 121 vinavyopitiwa na mradi huo kutoka
Iringa hadi Shinyanga.
Wataalam kutoka Wizara ya Nishati na
TANESCO wakifuatilia hotuba ya Naibu Waziri wa Nishati, Subira Mgalu
(hayupo pichani) wakati akizungumza na wananchi katika Kijiji cha
Chiboli wilayani Chamwino.
………………………….
Wananchi katika Kijiji cha Chiboli
wilayani Chamwino, Jimbo la Mtera, watasherehekea sikukuu ya Eid El-fitr
wakiwa na umeme kwa mara ya kwanza, baada ya Naibu Waziri wa Nishati,
Subira Mgalu kuwasha umeme katika Kijiji hicho.
Akiwa ameambatana Mbunge wa Mtera,
Livingstone Lusinde na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Vumilia Nyamoga,
Naibu Waziri wa Nishati, amewasha umeme katika Zahanati ya Kijiji hicho
pamoja na Kisima cha Maji ambapo Kijiji hicho kimepata umeme kupitia
mradi wa BTIP (kV 400) ambao umesambaza umeme katika Vijiji 121
vinavyopitiwa na mradi kutoka Iringa hadi Shinyanga.
Akizungumza na Wananchi, Mgalu alisema
kuwa, kuwashwa kwa umeme katika Kijiji hicho ni muendelezo wa
utekelezaji wa adhma ya Serikali ya Awamu ya Tano kufikisha umeme katika
Vijiji vyote nchini.
Amesema kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano
ilipoingia madarakani mwaka 2015 kulikuwa vijiji takribani 2,018 vyenye
umeme ambapo kuanzia Januari 2016, vijiji vipya vilivyoongezeka ni
takribani 5000 hivyo hadi sasa vijiji 7,290 vina umeme kati ya Vijiji
12,268.
Kuhusu usambazaji umeme katika maeneo
ambayo hayajapata umeme ingawa yamepitiwa na miundombinu alisema kuwa,
kuna mradi wa ujazilizi, mzunguko wa Pili unaolenga kuongeza wigo wa
kuunganisha umeme katika vitongoji mbalimbali na Dodoma ni kati ya Mikoa
itakayoguswa na mradi huo.
Naibu Waziri, pia alisisitiza wananchi kutumia vifaa vya Umeme Tayari (UMETA) ambavyo vitawawezesha kuondokana na gharama za wiring na kuwezesha kuunga wateja wengi katika mradi huo wa BTIP.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la
Mtera, Lusinde alishukuru Serikali kwa kupeleka umeme katika Kijiji
hicho, hata hivyo aliomba umeme huo ufike katika maeneo muhimu kama vile
shamba la umwagiliaji, nyumba za ibada, na vitongoji vya Kijiji hicho.
Aidha, aliipongeza Serikali kwa kufanya
kazi bila ubaguzi kwani idadi ya watu katika Kijiji hicho si kubwa
ukiliganisha na vijiji vingine lakini Serikali haikungalia idadi ya watu
hao ili kufikisha umeme katika Kijiji hicho wala hadhi ya nyumba.
Wilaya ya Chamwino, ina vijiji 107 na
vijiji 54 tayari vimesambaziwa umeme huku kazi ya usambazaji ikiendelea
kupitia miradi mbalimbali kama REA Awamu ya Tatu, Mzunguko wa Kwanza na
BTIP.
No comments:
Post a Comment