Waziri Mkuu Kassim Majaliwa,
akizungumza na Wanachama na wapenzi wa Yanga katika hafla ya kuchangia
klabu ya Yanga, iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es
Salaam, Juni 15.2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).
.......................
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa
amevitaka vilabu vya soka nchini kutumia vema fursa ya kuwa na mashabiki
wengi katika kuvifanya viweze kujitegemea kiuchumi.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo
(Jumamosi, Juni 15, 2019) katika hafla ya kuchangia klabu ya Yanga,
iliyofanyika kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.Ameichangia
klabu hiyo sh. milioni 10.
“Natambua kwamba Yanga ni klabu
kubwa na kongwe nchini ikiwemo Simba Sport Club ambazo ndizo zina
wanachama na mashabiki wasiopungua milioni 20 au zaidi.”
Hivyo, Waziri Mkuu ametumia fursa
hiyo kuvitaka vilabu vya soka nchini kutafuta njia nzuri na endelevu ya
kupata mapato ili kuendesha timu zao na kujiimarisha kiuchumi.
Amesema kwamba, kuimarika kwa
vilabu hivyo vyenye ushawishi mkubwa katika soka nchini ni muhimu kwa
mustakabali wa soka la Taifa letu.
Waziri Mkuu amesema kufanya vizuri
kwa vilabu hivyo kuna uhusiano wa mkubwa na wa moja kwa moja na
mafanikio ya timu ya soka ya Taifa.
“Nampongeza kocha wa Yanga, Mwinyi
Zahera kwa kazi nzuri aliyoifanya msimu ulioisha na kuiwezesha timu ya
Yanga kufanya vizuri ingawa haikupata ubingwa.”
Pia, Waziri Mkuu amesema yeye ni
mpenzi wa timu zote zinazoshinda na zinazoshindwa. “Kama kuna timu
naipenda sana ni siri yangu, hata nyie hamuijui.”
Waziri Mkuu amesema soka ni mchezo
maarufu na una wapenzi wengi duniani na hapa nchini na umejipambanua
kwa fursa nyingi ikiwemo biashara, uwekezaji na ajira.
Amesema Serikali imeendelea
kusimamia maendeleo ya michezo, ukiwemo mchezo wa soka ikiwa ni
utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi ya Mwaka 2015-2020.
“Mhe. Rais Dkt. John Magufuli
amekuwa akiungana na wanamichezo kuhamasisha kuendeleza michezo na
anatamani kuona mkishinda hadi katika ngazi ya Afrika.”
Kadhalika, Waziri Mkuu
amezipongeza timu zote za soka zinazofanya vizuri katika ngazi
mbalimbali. “Tumeshuhudia Polisi na Namungo FC zikipanda hadi ligi kuu.”
Ameipongeza timu ya Simba kuwa
klabu bingwa, Azam kuwa bingwa wa FA, Serengeti boys na Twiga
kuliwakilisha Taifa na Taifa Stars inashiriki AFCON – Misri.
“Kitendo cha Azam kushinda FA na
Simba kushiriki vizuri AFCON sasa kumewezesha timu zetu mbili zaidi,
Yanga na KMC kupata nafasi ya kushiriki mashindano ya CAF.”
Kuhusu harambee ya Kubwa Kuliko,
Waziri Mkuu amesema ni mwanzo mzuri kuelekea kwenye mabadiliko
yatakayoiwezesha Yanga kujitegemea na kujiendesha bila kutarajia
michango kama ilivyo sasa.
Naye, Rais Mstaafu wa Awamu ya
Nne, Dkt. Jakaya Kikwete amewataka wanachama wa Yanga warudishe hisia na
mapenzi kwa timu yao kama ilivyo kwa timu ya Simba, pia wawe na ubunifu
wa kutengeneza mfumo mzuri wa mapato.” Siku hizi Yanga imekuwa baridi
sana, viongozi wa Yanga lazima mbadishe hali hii.”
Amesema viongozi wa sasa wa klabu
ya Yanga chini ya Uwenyekiti wa Dkt. Mshindo Msolla ni wazuri na
wanaujua mpira vizuri, hivyo watengeze mifumo mizuri itakayoinufaisha
klabu. Wahakikishe wanawekeza kwenye timu ya watoto badala ya kuangalia
wachezaji wa kutoka nje ya nchi pekee.
Amesema wasipowekeza kwenye timu
ya watoto siku zote watakua mafahari wa kuwa na wachezaji kutoka nchi za
nje jambo ambalo ni sawa na kuwafundishia wenzao. “Leo mnajisifia na
akina Makambo, Kagere siku ikicheza timu ya Taifa inakuwaje. Oneni
fahari ya kuwa na wachezaji wa ndani hivyo waendelezeni Tanzania kuna
vijana wana vipaji.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa
klabu ya Yanga, Dkt. Mosolla amesema yeye pamoja na viongozi wenzake
watahakikisha wanajenga umoja ndani ya klabu na kuipeleka jirani na
wananchi kwa kufufua matawi na kuwa na wanachama wapya wengi.
Pia watawatumia wachezaji wa
zamani katika kupata wanachama wengi na pia watakuwa na wiki ya klabu
hiyo ambayo wataitumia kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii na
kurudisha utaratibu wa kwenda mikoani baada ya ligi kuisha kwa ajili ya
kutembelea wananchi na kujiongezea wsanachama.
Kuhusu suala la mabadiliko ya
katiba amesema watalifanya kwa kufuata utaratibu wa kisheria. Pia Dkt.
Msolla amesema uongozi wake utahakikisha unazingatia utawala bora na
tayari wametoa matangazo ya nafasi za ajira.
Akizungumza kuhusu hali ya usajili
kwa ajili ya msimu ujao wa ligi kuu, amesema hadi sasa tayari
wamekamilisha kwa asilimia 90 kuwasajili wachezaji wote aliowataka kocha
wa timu hiyo Mwinyi Zahera kutoka nje ya nchi na wa ndani ya nchi.
Dkt. Msolla ametumia fursa hiyo
kumuomba Waziri Mkuu awasaidie ili Serikali iweze kuwapunguzia
changamoto mbalimbali zinazoikabili klabu hiyo ya Yanga ikiwemo ya
madeni.
Awali,Mwenyekiti wa Kamati ya
Hamasa wa klabu ya Yanga, Anthony Mavunde, alisema kamati hiyo ilikuwa
na wajumbe 27 waliofanikisha kupatikana kwa fedha ambazo zimetumika
katika kusajili wachezaji wapya kwa ajili ya msimu ujao wa ligi.
Mavunde ambaye pia ni Naibu Waziri
wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Uratibu, Bunge, Ajira na Vijana
alisema walisambaza kadi kwa ajili ya kukusanya fedha za kuimarisha
klabu yao ili iweze kujiendesha na kutatua changamoto za wachezaji.
Alisema mbali na kukusanya
michango pia kamati yao imependekeza kufanyika kwa mabadiliko ya katiba
ili kutengeneza mfumo mzuri utakaoisaidia timu hiyo kuweza kujiendesha
na kuweka mfumo mzuri wa kutumia vifaa vya klabu kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Mjumbe wa Baraza
la Wadhamini la klabu ya Yanga na Mke wa Rais wa Kwanza wa Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar, Mama Fatma Karume amewataka wananchi wasitumie
vilabu vya soka kama njia ya kutaka kujipatia nafasi za kisiasa. Pia
amewataka wanachama wampe ushirikiano Mwenyekiti wao mpya.
Naye, Waziri wa Habari, Utamaduni,
Sanaa na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe alisema hakuna kipindi kigumu
kilichompa tabu katika kuongoza wizara hiyo kama kipindi ambacho timu
ya Yanga ilipokuwa katika mgogoro wa kiuongozi.
Pia, Dkt. Mwakyembe alionesha
kutoridhishwa na upangwaji wa ratiba za michezo mbalimbali ya ligi kuu
msimu uliopita, hivyo alitumia fursa hiyo kuwahakikishia wapenzi wa soka
nchini kwamba mambo hayo hayatajirudia tena katika msimu ujao.
No comments:
Post a Comment