TFDA Yaja na Mfumo Mpya wa Udhibiti wa Vyakula
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa TFDA, Adam Fimbo akizungumza na Waandishi wa
Habari(hawapo pichani) katika Semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo
Wahariri na Waandishi wa Habari katika kuelimisha jamii juu ya masuala
ya usalama wa Chakula inayoendelea Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Chakula na Dawa TFDA, Adam Fimbo, akiwa kwenye picha ya Pamoja na
Waandishi wa Habari, mara baada ya kufungua Semina ya siku mbili ya
kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi wa Habari katika kuelimisha jamii
juu ya masuala ya usalama wa Chakula inayoendelea Wilayani Bagamoyo
Mkoani Pwani.
Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa chakula wa
TFDA Bw. Moses Mbambe, akiwasilisha Maada kuhusu majukumu ya TFDA
katika Semina ya siku mbili ya kuwajengea uwezo Wahariri na Waandishi
wa Habari katika kuelimisha jamii juu ya masuala ya usalama wa Chakula
inayoendelea Wilayani Bagamoyo Mkoani Pwani.
(Picha na Paschal Dotto-MAELEZO)
……………………
Na Grace Semfuko,MAELEZO.
Mamlaka ya Chakula na Dawa Tanzania TFDA
imeweka mfumo maalum wa udhibiti wa usalama wa chakula kinachozalishwa
ndani ya nchi na kile kinachoingizwa kutoka nje ili kuwahakikishia afya
bora kwa walaji.
Mfumo huo ni kufanya tathmini ya vyakula
vilivyofungashwa,kusajili maeneo na kutoa vibali vya biashara za
vyakula, kufanya ukaguzi wa vyakula katika soko pamoja na ukaguzi wa
maeneo ya kusindikia, kuhifadhia na kuuzia vyakula.
Akizungumza wakati akifungua Semina ya
siku mbili kwa waandishi wa Habari iliyofanyika Wilayani Bagamoyo Mkoani
Pwani Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TFDA Adam Fimbo alisema mfumo huo pia
unalenga kuchunguza sampuli za vyakula katika maabara.
“Ndugu zangu Waandishi wa Habari, naomba
muufahamishe Umma kuwa mfumo huu unahakikisha kila Mtanzania anatumia
chakula salama, na tunaanzia mipakani na kwenye maeneo mbalimbali hapa
nchini” alisema Fimbo.
Nae Kaimu Mkurugenzi wa Usalama wa
chakula wa TFDA Bw. Moses Mbambe alisema umuhimu wa usalama wa chakula
Nchini Tanzania unapewa kipaumbele kwa kushirikiana na Baraza Kuu la
umoja wa mataifa ambapo kupitia kikao chake cha Desemba 28 2018
ilipitisha siku ya usalama wa Chakula Duniani kuwa Juni 7 ya kila
mwaka ambapo kwa mara ya kwanza Duniani kote siku hiyo ilianza mwaka huu
wa 2019.
“Tanzania tunaungana na Umoja wa Mataifa
katika kuhakikisha tunakuwa na kiwango cha hali ya juu cha usalama wa
chakula,tunawaomba wananchi wazingatie uzalishaji bora wa vyakula na
hii itaongeza ufanisi na kuimarisha afya za wananchi wetu” alisema
Mbambe.
Kwa mujibu wa shirika la Afya Duniani WHO
takribani Watu Milioni 600 Duniani sawa na Mtu mmoja kati ya watu 10
huugua kila mwaka kutokana na kula chakula kisicho salama na kati yao
watu 420,000 hufariki na huku watoto wakiwa 125,000 wenye umri wa
chini ya miaka mitano ambapo kwa Bara la Afrika zaidi ya watu milioni 91
wanakadiriwa kuugua huku watu 137,000 hufariki dunia kila mwaka.
No comments:
Post a Comment