NA : Mwandishi Wetu
Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo kwa
kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu imewataka wapenzi na wadau wa soka nchini
kushiriki maandalizi ya mashindano ya Shirikisho la Mpira wa Miguu kwa
watu wenye ulemavu Afrika Mashariki (CECAAF) yanayotarajiwa kufanyika nchini
Mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari leo
Mei 16, 2019 Jijini Dodoma,katika mkutano uliolenga kuitambulisha kamati ya
wabunge watano waliojitolea kuhamasisha Watanzania,kushiriki kwa hali na mali
katika mashindano hayo, Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.
Harrison Mwakyembe, amesema kuwa mashindano hayo yatashirikisha nchi za
Tanzania Bara, Zanzibar, Uganda, Kenya na Rwanda.
“Mashindano haya yatakayokuwa ya kwanza kufanyika
katika ukanda huu wa Afrika yameanzishwa kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa
Mataifa wa haki za Walemavu wa mwaka 2006, unaotaka haki ya Walemavu kushiriki
katika mambo kadhaa ikiwemo michezo”
Akifafanua zaidi, Dkt. Mwakyembe amesema kuwa lengo
la kuhamasisha umma wa watanzania ni kuunga mkono mashindano hayo kwa hali na
mali.
Kwa upande wake Naibu Waziri Ofisi ya Waziri
mkuu anayeshughulikia watu wenye ulemavu Mhe. Stella Ikupa amesema kuwa
mashindano hayo yatasaidia kuibua vipaji vya watu wenye ulemavu na hivyo
kushiriki katika kukuza sekta ya michezo.
Pia ameiomba jamii kwa upana kujitokeza kuchangia
na kushiriki mashindano hayo kwa kuzingatia kuwa watu wenye ulemavu wana nia ya
kushiriki vyema katika mashindano hayo.
Naye mbunge wa Sengerema mhe. William
Ngeleja,ambaye pia ni mwenyekiti wa klabu ya michezo ya Bunge, akizungumza kwa
niaba ya Spika wa Bunge, amesema kuwa watashiriki kikamilifu katika
kuhakikisha kuwa mashindano hayo yanafanikiwa kwa kuzingatia malengo yake.
Mheshimiwa Ngeleja,aliongeza kusema kuwa
watashiriki kwa vitendo kwa kuzingatia kuwa Bunge ni wasimamizi
wa sheria za sekta ya michezo ,mikataba ya kimataifa, sheria na
kanuni katika sekta hii.
Wizara ya Habari kwa kushirikiana na Ofisi ya
Waziri Mkuu, inawaomba wananchi kuipa Kamati hii ya wabunge ushirikiano
wakutosha katika maandalizi ya michuano hiyo ambayo inahitaji fedha ya kutosha
na vifaa.
Wabunge wanaounda kamati hiyo ni Mheshimiwa William
Ngeleja,Mheshimiwa Venance Mwamoto,Mheshimiwa Margareth Sitta, Mheshimiwa Amina
Mollel na Mheshimiwa Riziki Said Lulida.
No comments:
Post a Comment