Upanuzi Chuo cha Ualimu Patandi Kupunguza Changamoto ya Walimu wa Elimu Maalum
Na Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imekamilisha upanuzi wa Chuo cha
Ualimu Patandi ili kukiongezea uwezo wa kudahili walimu wenye taaluma
ya elimu maalum wanaohitajika nchini ili kupunguza changamoto ya walimu
hao.
Hayo yameelezwa leo Bungeni, Jijini
Dodoma na Mhandisi Stella Manyanya alipokuwa akijibu swali la Mhe. Grace
Victor Tendega Mbunge wa Viti Maalum kwa niaba ya Waziri wa Elimu
Sayansi na Teknolojia Prof. Joyce Ndalichako juu ya mpango wa Serikali
katika kuhakikisha walimu wenye weledi wa watu wenye ulemavu
wanatosheleza nchini.
“Serikali imekuwa ikichukua hatua
mbalimbali katika kukabiliana na changamoto ya upungufu wa walimu wenye
Taaluma ya Elimu Maalum. Changamoto hii inasababishwa na ongezeko la
uandikishaji wa wanafunzi wenye ulemavu kutokana na mabadiliko chanya ya
kimtazamo na uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa elimu kwa watu wenye
ulemavu,” amesema Mhandisi Manyanya.
Ameendelea kusema, mahitaji ya walimu wa
elimu maalum nchini ni walimu 8,882 katika shule maalum na vitengo
vinavyopokea wanafunzi wenye mahitaji maalum 706, ambapo hadi kufikia
Disemba 2018 walimu 5,556 wenye Taaluma ya Elimu Maalum ngazi ya
Astashahasa, Stashahada na Shahada walihitimu katika vyuo mbalimbali
nchini vikiwemo Chuo cha Ualimu Patandi na Chuo Kikuu Dodoma.
Aidha amesema, hatua ya Serikali ya
kuanzisha kozi ya elimu maalum katika ngazi ya Astashahada Chuo cha
Ualimu Patandi kwa walimu tarajali kwa mwaka wa masomo 2018/19 itaongeza
idadi wa walimu wanaojiunga na mafunzo ya Ualimu wa Elimu Maalum ili
kupunguza changamoto ya walimu wenye elimu hiyo wanaohitajika nchini.
No comments:
Post a Comment