SEVILLA YAICHAPA 5-4 SIMBA SC UWANJA WA TAIFA,BOCCO MCHEZAJI BORA WA MECHI
Na Mwandishi Wetu
TIMU ya Sevilla ya Hispania imefanikiwa kutwaa Kombe la
SportPesaChallenge baada ya kuwafunga wenyeji, Simba SC mabao 5-4 katika
mchezo maalum wa kirafiki Uwanja wa Taifa mjini Dar es Salaam usiku wa
leo.
Lakini haukuwa ushindi mwepesi, kwani Sevilla waliomaliza nafasi ya sita
kwenye La Liga msimu walilazimika kutoka nyuma kwa mabao 3-1 hadi
mapumziko ili kushinda 5-4.
Nahodha wa klabu, John Raphael Bocco alianza kuifungia Simba SC dakika
ya nane kabla ya mshambuliaji mwenzake, Mnyarwanda Meddie Kagere kufunga
la pili dakika ya 14.
Sevilla ikazinduka na kupata bao lake la
kwanza dakika ya 24 kupitia kwa Jesus Escudero, lakini mshambuliaji wa
kimataifa wa Tanzania, Bocco akaifungia Simba SC bao la tatu dakika ya
32.
Sevilla ikakianza vyema kipindi cha pili baada ya kufanikiwa kupata bao
la pili kupitia kwa Bryan Gil dakika ya 48, lakini kiungo Mzambia,
Clatous Chama akaifungia Simba SC bao la nne dakika ya 61.
Sevilla wakacharuka kuanzia dakika ya 85 wakipata mabao matatu na
kuibuka na ushindi huo, kabla ya kukabidhiwa Kombe na Waziri wa Habari,
Utamaduni Sanaa na Michezo, Dk. Harrisons Mwakyembe.
Alianza winga Mholanzi, Quincy Promes kufunga mabao mawili dakika ya 85
na 89 kabla ya Manuel Agudo DurĂ¡n maarufu kama Nolito kufunga la ushindi
dakika ya tano ya muda wa nyongeza baada ya kutimia dakika 90.
Pamoja na kuchapwa, Simba SC ikajifariji baada ya Nahodha wake, John Bocco kukabidhiwa tuzo ya Mchezaji Bora wa Mechi hiyo.
Kikosi cha Simba SC kilikuwa; Aishi Manila, Zana Coulibaly, Mohammed
Hussein ‘Tshabalala’, Pascal Wawa, Jonas Mkude/Muzamil Yassin, Emmanuel
Okwi, Clatous Chama, John Bocco na Haruna Niyonzima/Hassan Dilunga.
Sevilla: Juan Soriano, Jesus Escudero, Simon Kuaer, Ever Banega, Quincy
Promes, Roque Sema, Wissam Ben Yedder, Emmanuel Agudo Nolito na Franco
Vazquez.
No comments:
Post a Comment