Na. Paschal Dotto-MAELEZO
Serikali Kupitia Wizara ya
Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, imesema kuwa itaendelea kuwajengea
uwezo na uzoefu mafundi sanifu na mafundi Michundo, ili waendelee
kutekeleza kazi zao kwa ufanisi na kuongeza wataalam katika kada hiyo
kwani fani hizo zina watu wachache.
Akizungumza Jijini Dar es
Salaam katika Mkutano wa Wasanifu Majengo na mafundi Michundo, Katibu
Mkuu Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano,Dkt. Elius Mwakalinga
alisema kuwa Serikali kupitia Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano
imejikita katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa miundombinu unafanikiwa kwa
kiasi kikubwa.
“Serikali imedhamiria kujenga
miundombinu ili kuwezesha ukuaji wa Sekta ya Viwanda nchini, hivyo
Mafundi sanifu wanategemewa sana katika kuwezesha miundombinu hii, ili
Tanzania iweze kufikia ndoto ya kuwa kwenye uchumi wa kati kupitia
viwanda, na katika kutekeleza hilo mwaka wa Fedha 2019/2020, Wizara ya
Ujenzi imejikita katika ajenda tatu ikiwemo kuwajengea uwezo wasanifu na
wahandisi wote nchini”, Alisema Dkt. Mwakalinga.
Dkt. Mwakalinga alisema kuwa
Serikali inahakikisha watalaam chini ya Taaluma ya Uhandisi, Usanifu
Majengo, Ukadiriaji Majenzi na kada zingine katika sekta ya ujenzi
wanaongezeka kiidadi na kujengewa ujuzi mahsusi ili kuwa na uwezo na
kumudu mahitaji ya nchi ya wataalam hao.
Aidha, Dkt. Mwakalinga
aliwathibitishia kuwa serikali inaendelea kushirikiana na bodi
mbalimbali za taaluma za kihandisi kwa kutoa miradi inayotekelezwa
nchini ili kuwawezesha watalaam hao kupata uzoefu na kufanya kazi kwa
ufanisi mkubwa na kazi hiyo itaanza rasmi mwaka wa fedha 2019/2020,
Julai Mosi.
“Napenda niwadhihirishie kuwa,
Serikali ya Awamu ya Tano, chini ya uongozi wa Rais Magufuli, inayo
dhamira ya dhati ya kuendeleza fani ya usanifu kwa kutumia miradi yake
inayotekelezwa, kama vile ujenzi wa Reli ya kisasa, SGR, Ujenzi wa
Interchange Ubungo, Ujenzi wa Bwawa kubwa la kuzalisha umeme mto Rufiji,
na ujenzi wa Daraja la Selander, kwa hiyo miradi hii itaweza kutoa
uzoefu mkubwa kwa wataalum wetu”, alisema Dkt. Mwakalinga.
Katika kuongeza uzoefu wa
watalaam hao, Dkt Mwakalinga amesema ni lazima kuwepo na maarifa na
vitendea kazi ambavyo kwa sasa ni uwepo wa miradi ya kimaendeleo ambayo
inatekelezwa na Serikali na sasa mafundi sanifu wanahitajika ili
kuiwezesha miradi hii kutekelezwa pasipo gharama kubwa.
Akaongeza kuwa Serikali
inapoendelea na zoezi la kuwapa uwezo watalaam hao inawaomba wawe
waadilifu, wenye kujituma na wenye weledi mkubwa maana kazi yao hiyo ni
kubwa sana kuliko kazi zingine za kihandisi.
“ Kama nilivyosema hapo awali
tutaendelea kuwajengea uwezo watalaam wetu kwa kutumia miradi
tuliyonayo, lakini kujenga uwezo kuna uhusiano mkubwa na masuala ya
kujituma, kuijitoa kwa moyo kwa taifa, kufanya kazi kwa bidii na weledi
mkubwa, hii ndiyo itakuwa tiketi ya kupata kazi na tutachagua watalaam
kulingana na vigezo hivyo,”Alisisitiza Mwakalinga.
Akizungumzia kuhusu changamoto za
uhaba wa wataalam hao, Dkt. Mwaklinga aliainisha kuwa, kwa takwimu za
Shirika la kazi duniani, ILO, zinabaini kuwa Mhandisi mmoja anapaswa
kufanya kazi na Mafundi Sanifu watano, na Mafundi Stadi 25, na kuongeza
kuwa hiyo inaonyesha umuhimu wa wasanifu na mafundi stadi katika sekta
ya ujenzi.
Kwa Upande wake Mwenyekiti wa
Bodi ya Usajili Wahandisi (ERB), Prof. Ninatubu Lema, alisema kuwa
Wasanafi wanahitajika kijituma ili kuanzisha viwanda vidogovidogo vya
kutengeneza vitu mbalimbali ambavyo vinaweza kuuzwa nchini.
“Mnatakiwa Mafundi Sanifu kuwa
wabunifu katika kujenga na kutengeneza uwezo kwa kufanya wajasiriamali
wa kujenga viwanda vidogovidogo, ili mtu mmoja aajiri watu watano, watu
sita au watu 10 na kutengeneza vitu vidogovidogo vya kuuzwa hapa nchini,
… tuko tayari kuratibu na kwenda kwenye nchi za wenzetu kama India,
China kutazama hivyo viwanda vidogovidogo.”, Alisema, Prof.Lema.
No comments:
Post a Comment