Na Dennis Buyekwa
Katika kuboresha Sekta ya Sheria
na Taifa kwa ujumla, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli, aliona umuhimu wa kuirudisha tena Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali iliyohamishiwa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali
hapo mnano mwaka 1965.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
imeanzishwa kwa Mamlaka aliyo nayo Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, chini ya Ibara ya 36 (1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania.
Kwa kuzingatia ibara hiyo, Mhe,
Rais alitoa amri ya kuboresha muundo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali kwa tangazo la Serikali Na. 48 la mwaka 2018 kwa lengo la
kuboresha huduma za kisheria katika Sekta ya Umma.
Kufuatia maboresho hayo ya muundo
wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, mnamo tarehe 13 Februari,
2018, Mhe, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliona upo umuhimu wa
kuirudisha Ofisi hiyo tena na alisaini Amri ya kuanzishwa kwake, kwa
tangazo la Serikali Na. 50 la mwaka 2018.
Aidha Mhe, Rais mnamo tarehe 15
April, 2018 alimteua Dkt. Clement Julius Mashamba kuwa Wakili Mkuu wa
Serikali na Dkt. Ally Saleh Possi kuwa Naibu Wakili Mkuu wa Serikali.
Akizungumzia malengo mahususi ya
kuirejesha tena Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Dkt. Mashamba, alisema
urejeshwaji wa Ofisi hii umelenga zaidi katika kuimarisha namna bora ya
kuimarisha na kusimamia mashauri mbalimbali yanayoihusu Serikali yaliyo
funguliwa na wadau wa ndani na wale wa nje ya nchi.
‘Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
inao wajibu mkubwa wa kuimarisha na kusimamia kikamilifu kesi zote za
madai Mahakamani, katika Mabaraza ya Usuluhishi pamoja na kesi zote
zinazohusu haki za binadamu na zile za kikatiba’.
Malengo mengine ya kuanzishwa kwa
Ofisi hii ni pamoja na kuratibu shughuli zote zinazohusu kesi za madai
na mwenendo wa usuluhishi kwa niaba ya Serikali Kuu, Mamlaka ya Serikali
za Mitaa, Idara mbalimbali zinazojitegemea, na Mashirika ya Serikali,
pamoja na kesi zote zinazohusu masuala ya haki za binadamu pamoja na
zile za kikatiba.
Aidha pamoja na malengo hayo
mahususi, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inaowajibu wa kutekeleza
majukumu mbalimbali, ikiwa ni pamoja na kuchukua na kuendesha kesi zote
za madai na usuluhishi kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, pamoja na kuwaelekeza Maafisa sheria na Mawakili wa Serikali
namna bora ya kusimamia uendeshaji wa kesi hizo.
Dkt. Mashamba aliongeza kuwa
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali inao wajibu wa kuratibu mashauri yote
ya madai, haki za binadamu, kesi za kikatiba na usuluhishi katika
Mahakama na Mabaraza ya Usuluhishi yanayoihusu Serikali kuu, Idara
mbalimbali na Mashirika ya Umma.
Aidha majukumu mengine ya
uanzishwaji wa Ofisi hii ni pamoja na kuandaa na kufungua mashauri
mbalimbali kwenye Mahakama za chini, Mahakama Kuu, Mahakama ya Rufaa, na
Mabaraza ya Usuluhishi kwa niaba ya Serikali ikiwa ni pamoja na kutoa
miongozo kwa wanasheria, mawakili wa Serikali, maafisa na watumishi
wengine walioajiriwa katika Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali.
Katika kutekeleza majukumu yake
ipasavyo Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, imedhamiria kuweka utaratibu
mzuri kwa kushirikiana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali utakao
wezesha Wizara, Idara na Taasisi za Umma, kutunza na kutoa taarifa au
kumbukumbu ya kesi za Madai na Usuluhishi zinazosimamiwa katika Wizara,
Idara na Taasisi husika ya Umma.
Wakili Mkuu wa Serikali pia
alisema tangu kuanzishwa kwa Ofisi hiyo, tayari mashauri 2169
yamesikilizwa katika Mahakama mbalimbali nchini ambapo mashauri 402 ni
yale yaliyosajiliwa, 42 ni yaliyosikilizwa katika mabaraza ya ndani na
nje ya nchi.
Kwa mujibu wa Wakili Mkuu wa
Serikali, mashauri 24 yalihusu masuala ya Katiba na haki za binadamu na
mashauri 12 yalihusu maswala mbalimbali ya uchaguzi wakati mashauri 58
yalikuwa ni marejeo na mapitio ya kesi mbalimbali (Reviews).
Katika kipindi hicho pia Ofisi ya
Wakili Mkuu wa Serikali ilifanya mazungumzo na Taasisi mbalimbali zenye
migogoro na taasisi nyingine za Setikali kwa pamoja waliweza kutatua
migogoro hiyo kwa kila pande kuridhika na suluhu iliyopatikana.
Naye Naibu Wakili Mkuu wa
Serikali Dkt. Ally Possi, akizungumza katika mahojiano yaliyofanyika
Ofisi kwake Jijini Dar es Salaam, alimshukuru Mhe. Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kwa uamuzi wake wa kuirejesha ofisi ya Wakili Mkuu
wa Serikali tangu ilipounganishwa na ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa
Serikali mwaka 1965.
Dkt. Possi alisema, kuanzishwa
kwa Ofisi hii kumeisaidia Serikali kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo
awali zilitumika kuwalipa Mawakili kwa kuwa Serikali ililazimika
kutumia Mawakili wengi binafsi hasa katika kesi za kimataifa kitendo
kilichoisababishia hasara kutokana na kuwalipa mawakili hao fedha nyingi
tofauti na sasa ambapo Serikali kupitia Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali imekuwa ikiwatumia Mawakili wa serikali hatua iliyosaidia
kuokoa Fedha za Umma.
“Uanzishwaji wa Ofisi ya Wakili
Mkuu wa Serikali umetimiza azma ya Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha Serikali yake
haitumii fedha nyingi katika uendeshaji wa kesi mbalimbali
zilizofunguliwa dhidi ya Serikali ya Tanzania” alisema Dkt. Possi.
Akizungumzia namna ofisi yake
ilivyojipanga kushughulikia Mashauri yote kwa wakati, Dkt. Possi alisema
kwa sasa wameweka mikakati madhubuti ya ufuatiliaji wa mashauri hayo
ikiwa ni pamoja na kushirikiana na Mahakama ili kuweka kipindi maalum
cha uendeshaji wa kesi hasa zile zilizokaa muda mrefu kitendo
kitakachosaidia kumaliza Mashauri hayo ndani ya muda mfupi.
Katika kuhakikisha wanatoa huduma
zenye viwango na ubora Dkt. Possi alisema Ofisi ya Wakili Mkuu wa
Serikali kwa sasa ina Idara inayosimamia ubora na viwango vya kesi zote
zinazoendeshwa na kusimamiwa na Ofisi yake ili kuhakikisha uendeshaji wa
Mashauri hayo unakidhi ubora unaotakiwa.
“Idara hii ina kazi ya
kushughulikia na kufuatilia ubora wa Mashauri kitendo kitakachosaidia
Mashauri yote yanayoihusu Serikali kusikilizwa muda mfupi ikiwa ni
pamoja na kuwasaidia Mawakili kuendesha kesi hizi kwa kuzingatia viwango
na ubora unaokubalika” alisema Dkt.Possi.
Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali
ilifunguliwa rasmi mkoani Dodoma mnamo Agosti 15, 2018 ambapo hafla hiyo
ya ufunguzi ilihudhuriwa na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Majaliwa Kasim Majaliwa pamoja na viongozi waandamizi wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
No comments:
Post a Comment