Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(wa pili kushoto)akiwa na baadhi ya wanafunzi wa kike wa kidato cha sita mkoani humo, wakipokea sehemu ya msaada wa taulo za kike zilizotolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na kuwasilishwa na Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa, Bi. Nuru Mwasulama (wa tatu kulia), katika kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita mwaka 2019 inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa mkoani Simiyu.
PICHA 3:-Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa, Bi. Nuru Mwasulama (wa pili kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka(kushoto) na baadhi ya viongozi wa Mkoa wa Simiyu na baadhi ya wanafunzi sehemu ya maboksi ya taulo za kike ambazo zimetolewa msaada kwa wanafunzi kike walio kwenye kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa kidato cha sita mwaka 2019 inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya Wasichana Maswa mkoani Simiyu.
Na Stella Kalinga,
Simiyu
Mamlaka ya Chakula na Dawa(TFDA)
imetoa msaada wa katoni 111 za taulo za kike zenye thamani ya shilingi milioni
tano, kwa wanafunzi wa kike 538 walio katika kambi ya kitaaluma ya wanafunzi wa
kidato cha sita mwaka 2019, inayoendelea katika Shule ya Sekondari ya wasichana
Maswa Mkoani hapa.
Akikabidhi msaada huo Aprili 05, 2019
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) Kanda ya Ziwa,
Bi. Nuru Mwasulama, amesema Mamlaka hiyo imetoa msaada huo kuunga mkono juhudi
za Serikali katika kuinua elimu mkoani Simiyu, ili kuwasaidia watoto wa kike
wasome kwa uhuru na utulivu kambini hapo hususani wakati wa hedhi.
Amesema TFDA kama wadau wa mkoa
wataendelea kushirikiana na Serikali mkoani Simiyu katika sekta ya elimu na
masuala mengine ya Maendeleo, huku akiwasisitiza wanafunzi walio kambini
kusoma kwa bidii na kutumia vizuri muda walionao ili waweze kufikia
malengo yao.
Akipokea msaada huo, Mkuu wa Mkoa wa
Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka ameishukuru Mamlaka hiyo kwa msaada uliotolewa
kwa wanafunzi wa kike, huku akiwasisitiza wanafunzi wote walio katika
kambi ya kitaaluma kusoma kwa bidii.
Aidha, Mtaka amewashukuru wadau
mbalimbali ambao wameendelea kutoa michango kwa ajili ya kufaninisha
kambi ya kitaaluma inayoendelea mkoani humo, huku akiahidi kuwa wadau
wote waliochangia watatambuliwa na kupewa vyeti.
Katika hatua nyingine Mtaka ametoa
ufafanuzi kwa wadau na wananchi kuhusu utaratibu wa kambi za kitaaluma mkoani
Simiyu, kwamba kambi hizi hufanyika katika ngazi za shule na baadaye huundwa kambi
moja ya mkoa kuwakutanisha wanafunzi kwa ajili ya kambi ya mkoa.
“Kambi za Kitaaluma kwenye mkoa
zilianza muda mrefu lakini kama mkoa tumeweka utaratibu wa kuwa na kambi moja
ya kimkoa inayounganisha shule zote za kidato cha sita; kambi za kidato cha nne
nazo zinaendelea kwa hiyo tutakapofika mwezi wa saba tutaanza kuunganisha
shule, kama tulivyofanya mwaka jana tuliunganisha shule 24 pale Simiyu
Sekondari” alisema.
Nao wanafunzi wa kike wa Kidato cha
Sita walio katika Kambi hiyo ya Kitaaluma wameishukuru Mamlaka ya Chakula na
Dawa kwa msaada huo ambao wamesema utawasaidia sana kusoma kwa uhuru na
kujiamini zaidi wakati wa hedhi.
“Tulikuwa tunakumbana na changamoto
ya kutokuwa na amani na kushindwa kujiamini wakati wa hedhi kwa hiyo hata
kusoma tulikuwa tunasoma lakini tunakuwa na wasiwasi, kupitia msaada huu
‘tutakuwa comfortable ‘ (tutakuwa na amani) kabisa tunaishukuru sana
TFDA”Mwanaidi Halfan.
“Huu msaada tuliopata utanisaidia
kufikia ndoto zangu maana wasichana wengi wanapokosa taulo hizi za kike
wanashindwa kusoma, wanakuwa na hofu wengine hata darasani hawaendi, lakini kwa
kuwa wote tumepata msaada huu najua muda tutakao kuwa hapa tutakuwa huru
kujisomea hatutaogopa tena maana zinatuhakikishia usalama tunapokuwa hedhi”
alisema Hidaya Simba
Jumla ya wanafunzi 1166 wa kidato cha
Sita mwaka 2019 kutoka shule 12 mkoani Simiyu wako katika kambi ya kitaaluma
kwa siku 28 katika shule ya sekondari Maswa, kwa ajili ya maandalizi ya Mtihani
wa Taifa unaotarajia kufanyika mwezi Mei, 2019.
MWISHO
No comments:
Post a Comment