Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akimkabidhi Mwenge kiongozi wa mbio za Mwenge Kitaifa kwa mwaka 2019
Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini Magharibi kuashiria kuanza kwa mbio za
Mwenge wa Uhuru 2019. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu
Hassan akiwasha Mwenge kuashiria kuzinduliwa kwa mbio za Mwenge wa Uhuru katika
uwanja wa Mlowo mkoani Songwe. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ametoa rai
kwa Wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutumia mbio za Mwenge wa
Uhuru mwaka huu 2019 kumkumbuka Baba wa Taifa kwa kupinga vitendo vya dhulma,
ufisadi, rushwa, maradhi, chuki, dharau na kuwataka kuenzi umoja na mshikamano
wetu kuchapakazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.
Makamu wa Rais
ameyasema hayo leo kwenye sherehe za uzinduzi wa mbio za Mwenge Kitaifa
zilizofanyika kwenye uwanja wa Mlowo mkoani Songwe na kuhudhuriwa na viongozi
mbalimbali wa Chama na Serikali akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa.
Kaulimbiu ya
mbio za Mwenge wa Uhuru mwaka 2019 ni “Maji ni haki ya kila mtu,
tutunze vyanzo vyake na tukumbuke kushiriki Uchaguzi wa Serikali za
Mitaa”
“Nimependezwa na kaulimbiu hii ambayo inauwiano wa moja kwa moja na
jukumu langu la kila siku la kusimamia na kutunza mazingira ya nchini. Sote
tunafahamu kuwa bila utunzaji thabiti wa mazingira basi vyanzo vya maji
hupotea”alisema Makamu wa Rais
Hali ya
upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama nchini inaendelea kuimarika ambapo
huduma ya maji vijijini imeongezeka kutoka wastani wa
asilimia 58.7 kwa mwaka 2018 hadi kufikia asilimia 64.8 mwezi februari 2019 na
miji mikuu ya mikoa kutoka asilimia 78 mwezi machi 2018 mpaka asilimia februari
2019.
“Niwahakikishie wananchi tutatekeleza kwa vitendo ilani ya Uchaguzi
ya Chama cha Mapinduzi inayotutaka kuboresha huduma ya maji vijijini kufikia
asilimia 85 na mijini kwa asilimia 95 ifikapo 2020”alisisitiza Makamu wa Rais
Aidha, Makamu
wa Rais kupitia hadhara ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka
2019 ametoa wito kwa wananchi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuacha kufanya
shughuli za kibinadamu kama vile kilimo, ufugaji, ujenzi, ukataji na uchomaji
miti kwenye vyanzo vya maji.
Makamu wa Rais
pia amewakumbusha wananchi juu ya uchaguzi wa Serikali za mitaa utakaofanyika
mwezi oktoba 2019 kuhakikisha wanachagua Viongozi wachapakazi na wenye dhamira
ya maendeleo kwa jamii.
Mbio za Mwenge
wa Uhuru mwaka 2019 zitaongozwa na Ndugu Mzee Mkongea Ali kutoka Mjini
Magharibi.
No comments:
Post a Comment