Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akipokea kitabu cha Utekelezaji wa Ilani ya
Uchaguzi cha jimbo la Manonga kutoka kwa mbunge wa jimbo hilo Mhe. Seif
Gulamali wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa mikutano
Simbo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Mheshimiwa Makamu wa Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan leo ameanza ziara
ya kikazi katika Mkoa wa Tabora ambapo atatembelea Wilaya zote saba (7)
za Igunga, Nzega, Uyui, Sikonge, Kaliua, Urambo na Tabora .
Akiwa wilayani Igunga
Makamu wa Rais alipokea taarifa ya utekelezaji ya mkoa liyosomwa na Mkuu wa
mkoa huo Mhe. Aggrey Mwanri katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya ya Igunga,
na kukagua maendeleo ya ujenzi wa tanki kubwa la masi ikiwa sehemu ya
utekelezaji wa mradi wa maji wa shilingi bilioni 600 ambao utekelezaji wake
umefikia asilimia 58% kisha kutembelea maendeleo ya ujenzi wa kituo cha afya
Simbo ambapo alipanda mti wa kumbukumbu na kuhutubia wananchi wa Simbo.
Ziara za Makamu wa Rais
zina lengo la kuhamasisha na kukagua shughuli za maendeleo kama ilivyoahidiwa
kwenye ilani ya uchaguzi ya 2015.
Akizungumza na wakazi wa
kijiji cha Simbo katika jimbo la Manonga wilayani Igunga Makamu wa Rais
aliwaambia wananchi hao kuwa tatizo kubwa la wilaya ya Igunga ni ukosefu wa
vyanzo vya maji.
“Serikali
itafanya kila linalowezekana kuhakikisha maji ya kutosha yanapatikana Igunga”alisema Makamu wa Rais.
Katika suala la afya wilaya
ya Igunga ina Vituo 66 vya afya kati ya hivyo 55 vinamilikiwa na Serikali.
Makamu wa Rais amehimiza
Elimu ya kutosha kwa wananchi juu ya umuhimu wa bima ya afya ambapo Serikali
inajiandaa na mpango wa Bima kwa wote.
Makamu wa Rais pia
amewataka Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya kutoa elimu ya kutosha kwa wafanya
biashara wadogo wadogo na kuhakikisha wale wenye sifa ndio wanapata
vitambulisho.
Katika ziara
yake mkoani Tabora Makamu wa Rais ameambatana na Waziri wa Madini Mhe. Doto
Biteko, Naibu Waziri Maji Mhe. Juma Aweso, Naibu Waziri Ujenzi Mhe. Elias
Kwandikwa na Naibu Waziri TAMISEMI Mhe. Mwita Waitara .
No comments:
Post a Comment