Tuesday, February 5, 2019

TUMIENI IPASAVYO WIKI YA SHERIA-MAJALIWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi waliyohudhuria katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, iliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square jijjini Dodoma  Februari 2, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi waliyohudhuria katika maadhimisho ya Wiki ya Sheria, iliyofanyika kwenye viwanja vya Nyerere Square jijjini Dodoma  Februari 2, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Asema uelewa mdogo wa sheria unachangia wananchi kupoteza haki

MASUALA ya kisheria si mepesi kujulikana kwa kila mwananchi na kwa sababu hiyo, wananchi wengi wamekuwa na uelewa mdogo wa masuala hayo, jambo linalochangia baadhi kukosa au kupoteza haki zao. 

Pia, wananchi wengi hawajui taratibu na mienendo ya kimahakama, hivyo wamekuwa wakipoteza haki kwa kigezo cha kutofuata taratibu ili kupata haki zao hizo na wakati mwingine unaweza kukuta ni suala dogo tu.

Kila mwaka, Mahakama ya Tanzania imekuwa ikiadhimisha Wiki ya Sheria, ambapo pamoja na mambo mengine, wiki hiyo imekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi kwa kuwa inatoa fursa ya wananchi kupata elimu kuhusu masuala ya sheria.

Maadhimisho hayo ya Wiki ya Sheria yamekuwa yakifanyika kimkoa na kitaifa kwa wadau mbalimbali wa masuala ya sheria kutoa huduma kwa wananchi, ikiwa ni pamoja na kusikiliza masuala yao na kuyapatia ufumbuzi na kwa yale ambayo huhitaji ufumbuzi zaidi, hupewa msaada.

Kwa mwaka huu, maadhimisho ya Wiki ya Sheria, yamefanyika kwa mara ya kwanza Jijini Dodoma, baada ya Serikali kuhamishia makao makuu ya nchi katika jiji hilo.

Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na watu mbalimbali, wakiwemo wadau wa sheria. Mgeni rasmi alikuwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.

Akifungua maadhimisho hayo, Waziri Mkuu aliwataka wananchi wayatumie ipasavyo maadhimisho hayo ili waweze kupata elimu na huduma mbalimbali za kisheria.

Majaliwa alisema wananchi wa mikoa mbalimbali, ukiwemo Dodoma, wanatakiwa kutumia maadhimisho hayo kwa kujitokeza kwa wingi kupata elimu na kwa wale wenye matatizo ya kisheria kuyaeleza ili yatatuliwe.

“Kwa yule ambaye hana tatizo, aje kupata elimu ya sheria, kutoa maoni au mapendekezo yake kuhusu mfumo mzima wa utoaji wa haki. Waswahili husema, elimu haina mwisho. Kwa kuwa elimu ya sheria imesogezwa hapa Dodoma, tumieni fursa hii kujifunza kadri iwezekanavyo,” alisema.

Waziri Mkuu alibainisha kuwa, Serikali imeendelea kushirikiana na mhimili wa Mahakama katika kuhakikisha huduma bora za utoaji haki zinawafikia wananchi kwenye maeneo wanayoishi kwa wakati.
“Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli ni mdau muhimu wa Mahakama na inafuatilia kwa karibu changamoto zote zinazoikabili pamoja na wadau wengine katika mfumo wa utoaji haki,” alibainisha. 

Waziri Mkuu alisema  dhamira ya Mahakama kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika kuleta mabadiliko ya utoaji haki ni hatua nzuri na itasaidia kuboresha utoaji wa haki kwa wakati.

Hivyo, Waziri Mkuu aliwasihi watumishi wa Mahakama kujikita katika matumizi ya mifumo ya TEHAMA bila kukatishwa tamaa na changamoto zitakazojitokeza kwani mara nyingi kitu kipya chochote hakikosi changamoto za hapa na pale. 

“Binafsi naunga mkono uamuzi wa Mahakama kutumia TEHAMA katika usajili wa mashauri, kwani unakwenda sanjari na azma ya Serikali kuhakikisha TEHAMA inatumika vema kwenye taasisi za umma,” alisema.

Aliongeza kuwa matumizi ya TEHAMA katika taasisi za umma yanalenga kutoa huduma bora na kuipunguzia Serikali na mihimili mingine gharama za uendeshaji, hususan katika utoaji huduma kwa wananchi.

Alisema lengo la Serikali ni kuona huduma bora zinawafikia wananchi kwa urahisi na pia zinapatikana kwa wakati.

“Nitoe wito kwa wadau, wakiwemo mawakili wa serikali na wa kujitegemea, kutumia mifumo hiyo katika kusajili mashauri na wasiwe wao wa kwanza katika kulaumu na kubeza,” alisema. 

Waziri Mkuu alisema mawakili wote wa Serikali na wa kujitegemea, wanapaswa kuwa sehemu ya kutatua changamoto zitakazoibuka katika matumizi ya mifumo hiyo kwa kuwasilisha mapendekezo kuhusu namna bora ya kuiboresha. 

Alisema  matumizi ya TEHAMA si tu yatawawezesha kutoa huduma kwa wakati, bali pia  yataweka uwazi, ambao utawapunguzia malalamiko mengi kuhusu watumishi na utoaji haki. 

Waziri Mkuu alisisitiza kuwa  Wiki ya Sheria ni muhimu kwa mfumo mzima wa utoaji haki nchini. “Endeleeni kuienzi na itumieni vizuri katika kufanikisha malengo ya Mahakama ya kumpatia haki kila mwananchi bila ubaguzi.” 

Kwa upande wake, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahimu Juma, alisema  kwa kipindi cha wiki nzima, maonyesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika Jijini Dodoma  na kwenye Mahakama zote nchini, kuanzia ngazi ya wilaya.

Profesa Juma alisema  kupitia maonyesho hayo, wananchi watakaoshiriki na kutembelea mabanda, watapata elimu na kutathmini umuhimu na hadhi ya mfumo wa kimahakama katika kustawisha maisha yao pamoja na kuwasaidia kupata haki kwa mujibu wa sheria.

“Kujikumbusha umuhimu wa Mahakama kutoa haki kwa wakati, kuzingatia misingi ya maadili na Mahakama kuendeleza programu za maboresho yanayolenga kupeleka huduma za utoaji haki karibu zaidi na wananchi,” alisisitiza.

Jaji Mkuu aliwakumbusha viongozi wa vijiji, kata, wilaya, mkoa, idara na wizara, wabunge, majaji, mahakimu na watumishi wa umma, wahudhurie maonyesho hayo ya Wiki ya Sheria bila kukosa.

Alitolea mfano banda la maonyesho la Ofisi ya Mwanasheria Mkuu kwamba, kwa wale watakaoshiriki, watakumbushwa  kuwa mamlaka ya mihimili mitatu ya dola yanatokana na nguvu ya sheria, ambayo haimuonei mwananchi yeyote.

Katika maadhimisho hayo, ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika nje ya Jiji la Dar es Salaam, Waziri Mkuu alishiriki matembezi ya kilomita tano akiwa na Jaji Mkuu, Profesa Juma na viongozi wengine, yakianzia Mahakama Kuu Dodoma hadi viwanja vya Nyerere Square na kisha alitembelea mabanda.

No comments:

Post a Comment