Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) mara baada ya kutembelea Ofisi za Bodi ya Pamba ili kukagua maabara ya Pamba wakati akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Shinyanga, Leo Tarehe 27 Februari 2019. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) akizungumza kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan ambaye yupo mkoani Shinyanga kwa ajili ya ziara ya kikazi, Tarehe 27 Februari 2019.
Naibu Waziri wa Kilimo Mhe Innocent Bashungwa (Mb) akikagua maabara ya Pamba wakati alipotembelea Ofisi za Bodi ya Pamba Mkoani Shinyanga, Tarehe 27 Februari 2019.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan akikagua maabara ya Pamba wakati alipotembelea Ofisi za Bodi ya Pamba akiwa katika ziara ya kikazi Mkoani Shinyanga, Tarehe 27 Februari 2019.
Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Shinyanga
Naibu waziri wa Kilimo ameiagiza Tume ya
Maendeleo ya Ushirika kusimamia zoezi la ulipaji wa madai ya watumishi wa Chama
Kikuu cha Ushirika Shinyanga (SHIRECU).
Mhe Bashungwa ameyasema hayo leo tarehe 27
Februari 2019 kwenye mkutano wa hadhara mbele ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe Mama Samia Suluhu Hassan wakati akijibu swali la
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini Mhe Steven Masele aliyetaka kufahamu
watumishi hao watalipwa lini fedha zao za madai.
Katika agizo hilo ameitaka Tume ya Maendeleo
ya Ushirika nchini kuhakikisha kuwa malipo hayo yanalipwa haraka iwezekanavyo
kwani tayari tume hiyo ilikwisha elekezwa na Waziri Mkuu Mhe Kassim Majaliwa
kuthaminisha vyuma chakavu vya SHIRECU ili kuwalipa haraka watumishi hao.
Bashungwa aliongeza kuwa Adhma ya serikali ya
awamu ya Tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli ni kuleta
mageuzi ya kiuchumi na kuwafanya wananchi kuwa na maisha bora kupitia kilimo
ambacho kinafungamanishwa na viwanda ambapo mkakati huo utaimarika kwa kupitia
Ushirika kwani wakulima wanapojiunga na ushirika serikali ni rahisi kuwahudumia
kwa kuwa itakuwa inawatambua.
Alisema kupitia dhana ya ushirika itakuwa ni
njia rahisi kuwapatia wakulima pembejeo kwa wakati na za bei nafuu huku mara
baada ya kuvuna mazao yao serikali itawarahisishia upatikanaji wa masoko.
Kuhusu zao la Pamba Naibu Waziri Bashungwa amesema
kuwa katika kuongeza thamani ya zao hilo na kufungamanisha kilimo hicho na
viwanda wananchi wengi wamelima Pamba kwa kiasi kikubwa jambo litakalowapatia
fedha nyingi na kuinua uchumi wao.
Alisema kuwa katika zao la Pamba kumekuwa na
changamoto mbalimbali za upatikanaji wa Viuatililifu lakini serikali imeendelea
na mkakati wa kwenda moja kwa moja kwenye viwanda vinavyozalisha Viuatilifu nje
ya nchi ili kuondokana na mfumo wa madalali.
“Kwa kuwa utafiti unaonyesha kuwa viwanda
vingi vya kutengeneza viuatilifu vipo China hivyo nasi kama wizara kuaznia
msimu unaokuja wa kilimo wa mwaka 2019/2020 tutaenda wenyewe kunua viuatilifu
na kuhakikisha tunavileta nchini na kufanya hivyo tutakuwa tumefuta kabisa
changamoto hiyo” Alikaririwa Mhe Bashungwa na kuongeza kuwa
Endapo serikali itaenda yenyewe kununua
viuatilifu itarahisisha makali ya bei kwani itakuwa inanunua mzigo mkubwa hivyo
ni rahisi kupunguziwa bei.
MWISHO
No comments:
Post a Comment