Watumishi wa
Wizara ya Madini wakimkaribisha Waziri wa Madini Doto Biteko katika wizara hiyo
mara baada ya kuwasili kutoka kuapishwa Ikulu jijini Dar es Salaam. Sambamba ni
Naibu Waziri wa Madini, Stanslaus Nyongo.
Waziri
wa Madini Doto Biteko amewasili Makao Makuu ya Wizara jijini Dodoma na
kupokelewa na Watumishi wa Wizara ya Madini na baadhi ya Taasisi zake.
Biteko
aliteuliwa kuwa Waziri wa Madini Januari 8 baada ya Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kufanya mabadiliko madogo katika Baraza la
Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi.
Akizungumza
na watumishi hao, amewataka kujipanga na kushirikiana pamoja na viongozi wa
wizara na kuongeza kuwa, wao kama viongozi wanawategemea sana watumishi kuweza
kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
“Mimi
sio mgeni ni mwenyeji, wote tunafahamiana.
Nawashuru kwa kutupokea mimi na mwenzangu Nyongo. Ninyi ndiyo wenye wizara
sisi hatuwezi kuwa hapa kama ninyi hamjatupa ushirikiano,” amesema Biteko.
Ameongeza
kuwa, anataka kuona watumishi wa wizara hiyo wakiwa na furaha na kufanya kazi
kwa furaha katika kutekeleza wajibu na majukumu ya wizara husika na kueleza
kuwa, “Nataka nione wafanyakazi wanafurahi kufanya kazi. Kuna mtu unaweza
kumlazimisha kufika kazini lakini si kufanya kazi,” amesema.
Naye,
Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo amesema mabadiliko yaliyotokea ni kwa
ajili ya kuongeza ufanisi zaidi katika utekelezaji wa majukumu ya wizara na
kuongeza kuwa, Rais Dkt. Magufuli wakati akimwapisha Waziri Biteko Januari 9,
alitoa maagizo kwa viongozi hao, ambao wao waliyapokea kwa niaba ya watumishi
wote wa wizara na taasisi zake.
Awali,
Waziri Biteko alikuwa ni Naibu Waziri katika wizara hiyo ambayo ilikuwa
ikiongozwa na Waziri Angellah Kairuki ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Nchi,
Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.
No comments:
Post a Comment