Na Mwandishi Wetu, Morogoro
Chama cha Mapinduzi (CCM ) Mkoa Morogoro kimesema utendaji wa Serikali ya Rais Dk John Magufuli utawatia kiwewe na kuwapa wakati mgumu wapinzani huku kiongozi huyo akipasua anga na kutajwa katika orodha ya viongozi bora waliowahi kutokea Barani Afrika akishika nafasi ya pili ya kiongozi bora mwaka 2018.
Pia kimeeleza wakati wapinzani wakijifanya hawaoni yanayofanyika nchini kimikakati na kimaendeleo ni aibu pale taasisi mbalimbali za kimataifa zinaposifu juhudi za kisera zinazochukuliwa na utawala wa awamu ya tano.
Matamshi hayo yametamkwa leo na Mwenyekiti wa CCM Mkoa Morogoro Innocent Kalogeris wakati akizungumza na wanachama wa CCM kata ya Sanje jimbo la Kilombero mara baada ya kuwapokea viongozi 20 wa CHADEMA kutoka kata hiyo.
Kalogeris alisema ni aibu kwa baadhi ya watu, wanasiasa na wanaharakati wanaojaribu kumpinga Rais huyo, kuichafua serikali yake, kufanya uchochezi wa kisiasa na kidiplomasia huku wengine wakitaka kuvuruga Umoja, amani na utulivu .
Alisema ni mambo ya kusikitikisha kuona wapo wanasiasa ambao wana ufahamu mpana, uelewa wa kutosha pia wameelimika na kuwa viranja wa wanaopotosha ukweli, kuipaka matope serikali na wengine wakisahau hata shutuma, lawama na tuhuma walizotoa miaka mitano iliopita.
"Nakiri wakati kuna baadhi ya wanasiasa wakibeza utendaji wa serikali ya awamu ya tano.upinzani huo umepata pigo pale Afrika ilipomtangaza Rais Dk Magufuli akishika nafasi ya pili kwa kuwa kiongozi bora Afrika "Alisema Kalogeris .
Aidha Mwenyekiti huyo wa CCM aliwataka wanasiasa, viongozi wa upinzani na wanaharakati kuacha tabia za ukuwadi wa kisiasa kwani yanayofanywa na serikali ilio madarakani ni manufaa ya sasa na wakati ujao kwa Tanzania na watu wake.
"Tunatakiwa kuwa na utamaduni wa kukiri, kusifu na kupongeza kwa mema yanayofanyika. Kujifanya haoni wakati huna upofu wa macho huko ni kama kumkebehi mungu. Kupongeza si kitendo cha mtu kujidhalilisha bali ni kielelezo cha werevu na kustaarabika kwake "Alieeza Mwenyekiti huyo.
Alisema ikiwa miaka mitano iliopita wapinzani wa CCM walikuwa wakishutumu na kudai rushwa imekithiri, kuna ubadhirifu wa mali za umma, ufisadi huku watendaji dhamana wakiingia mikataba michafu bila kujali maslahi ya umma, hivyo wapinzani walitakiwa wawe wa kwanza kupongeza juhudi na ufanisi uliopo.
" leo mumerudi CCM nataka mtambue kuwa hapa nchini naamini kuna upinzani njaa unaoongozwa na wanasiasa waganga njaa. Kama dhana na msingi wa upinzani wa Tanzania ni kupinga hata mema yanayofanyika. Mantiki ya kuwepo kwake haionekani na wasitarajie kama watauungwa mkono wajiandae kukimbiwa zaidi "Alisisitiza
Katika orodha iliotajwa ya viongozi bora Afrika , aliyekuwa Rais wa Botswana, Ian Khama ameshika namba moja, ambapo enzi za uongozi wake, serikali yake imesifika kwa kutengeneza ajira, miundombinu, usawa na mageuzi katika nyanja mbalimbali ambazo kwa kiasi kikubwa zimeibadilisha nchi hiyo na kuwa taifa imara.
Kiongozi bora namba tatu, imekwenda kwa Waziri Mkuu Abiy Ahmed wa Ethiopia, ambapo yeye anatajwa kuwa mstari wa mbele katika kuleta mapatano ya kitaifa na kuweka usawa kwenye jamii ya nchi hiyo akikuza misingi ya demokrasia.
Ethiopia ilikuwa ikitajwa ni moja ya nchi hatari kwa wanasiasa kutokana na vifo vya utatanishi kwa viongozi wake, huku ikielezwa toka alipochukua madaraka , mtawala wa sasa amekuwa kiongozi bora mwenye usimamizi madhubuti aliyelifikisha mbali taifa hilo.
Rais wa Mauritius Ameena Ghulib Fakim ameshika nafasiya nne huku akitajwa kwa juhudi za kupigania kwake usawa na haki za raia na kulifanya taifa hilo kupiga hatua kubwa kwenye kilimo na usimamizi madhubuti wa rasilimali ya nchi hiyo.
Hata hivyo katika orodha hiyo, Rais wa Rwanda, Paul Kagame ameshika nafasi ya tano, ambapo anasifika kwa kuijenga Rwanda mpya baada ya mauaji ya Kimbari mwaka 1994 na kuifanya kuwa nchi tishio kiuchumi.
No comments:
Post a Comment