Thursday, January 17, 2019

BENKI YA KILIMO IHARAKISHE MALIPO YA KOROSHO - WAZIRI MKUU

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  wakuu wa mikoa ya Mtwara, Lindi na Ruvuma  katika kakao alichokiitisha kwa njia ya video akiwa ofisini kwake jijini Dodoma, Januari 16, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameitaka Benki ya Kilimo Tanzania (TADB) ihakikishe inabadilisha mfumo wake ili iweze kuharakisha malipo kwa wakulima wa korosho ambao wameshahakikiwa.

Ametoa agizo hilo leo (Jumatano, 16 Januari, 2019) wakati akizungumza na Wakuu wa Mikoa ya Lindi, Mtwara na Ruvuma pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa TADB kwenye kikao alichokiendesha kwa njia ya video (video conferencing) kutokea ofisini kwake Mlimwa, Dodoma.

Wakuu wa mikoa hiyo mitatu walikuwa kwenye mikoa yao na Mkurugenzi Mkuu wa TADB, alikuwa Dar es Salaam.

“Hakikisha mnaharakisha malipo ya wakulima lakini pia suala la uhakiki linabaki palepale ili tuwalipe wakulima wanaostahili,” amemweleza Mkurugenzi Mkuu wa TADB, Bw. Japhet Justine.

Waziri Mkuu amesema Serikali bado inapokea malalamiko kutoka kwa wakulima kuhusu suala la malipo ya korosho kwani kwa kawaida malipo ya mkupuo yote huwa yamekamilishwa ifikapo Januari 10 ya kila mwaka.

“Matarajio yetu yalikuwa ni kuvuna tani 245,000 au zaidi kidogo lakini umesema hadi sasa korosho zilizo kwenye maghala ni tani 206,000 maana yake takriban tani 40,000 ziko AMCOS au majumbani kwa wakulima. Na ambazo mmezilipia hadi sasa ni tani 92,000 na pointi zake. Tuko chini ya nusu.”

“Hili zoezi la uhakiki na malipo, lilianza Novemba 27, 2018 na leo ni tarehe 16 Januari, 2019 na hatujafika hata asilimia 50, maana yake zoezi hili tutalimaliza Aprili mwanzoni. Haiwezekani! Tunapata lawama kutoka kwa wakulima wa korosho kwa sababu hii kasi ni ndogo; na haya siyo malengo ya Mheshimiwa Rais, aliyetaka korosho zinunuliwe na Serikali.”

Waziri Mkuu alihoji ni kwa nini benki hiyo haishirikiani na vyama vikuu (unions) au vyama vya msingi (AMCOS) ili kubaini idadi halisi ya wakulima na idadi kamili ya kiasi walichovuna kwa sababu kila AMCOS ina wanachama wake wanaojulikana.

“Zao la korosho lina mfumo wa ushirika. AMCOS ziko kwenye ngazi ya vijiji na unaweza kukuta AMCOS moja ina wanachama zaidi ya 200, sasa bila kupitia kwenye hizi AMCOS unawezaje kujua kila mkulima amevuna kilo ngapi na anadai kiasi gani kwa kupitia Bodi ya Mazao Mchanganyiko pekee?

“Kuna Wilaya zina AMCOS zaidi ya 50. Ni kwa nini msitumie mfumo huo lakini mkawatenga kwenye makundi mawili yaani wakulima wenye chini ya kilo 1,500 au zaidi ya 1,500 ili muweze kufanyia uhakiki kwa urahisi?” aliluliza.

Ameitaka benki hiyo izishirikishe AMCOS na UNIONS pindi malipo yanapofanyika ili nao wajue ni wanachama wao gani ambao wameshalipwa. “Mfumo unaotumika sasa unapeleka malipo moja kwa moja kwenye akaunti ya mtu binafsi, kwa hiyo AMCOS wanakuwa hawana taarifa, na wao pia wanachangia kushiriki kutoa malalamiko.”

Waziri Mkuu pia alitumia fursa hiyo kuwataka wakuu wa mikoa hiyo wahuishe taarifa zao na wamtumie ili aweze kuzitumia kuratibu zoezi zima. “Mniletee taarifa zenu mkionesha ni kiasi cha korosho mlitarajia kuzalisha; mmeshakusanya kilo ngapi hadi sasa ambazo ziko kwenye maghala; kama malipo yameanza, ni wakulima wangapi wameshalipwa; na fedha kiasi kila mkoa umeshapokea hadi sasa,” amesisitiza.

“Nimeongea na wakurugenzi wa CRDB na NMB na kuwasisitiza kuwa suala la miamala ya malipo ya korosho lifanywe mchana na usiku ili malipo yakamilike kabla ya Januari mwishoni,” amesema.

Kwa upande wao, wakielezea changamoto wanazokabiliana nazo, wakuu hao wa mikoa walisema kuwa suala kubwa ni ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, baadhi ya AMCOS na vyama vya msingi kulipwa mara nyingi zaidi ya vyama vingine, miamala ya malipo ya wakulima kukataliwa na Benki na hali ya kutoaminiana baina ya timu ya uhakiki na watendaji wa wilaya na mikoa ambao ni wajumbe wa Kamati za Ulinzi na Usalama.

Mapema, Mkurugenzi Mkuu wa TADB, alisema fedha iliyolipwa kwa wakulima wa korosho hadi sasa ni sh. bilioni 306 kwa wakulima zaidi ya 156,000. “Korosho zilizolipwa hadi sasa ni tani elfu 92.7 ambazo ni wastani wa asilimia 44,” alisema.

Hata hivyo, Bw. Justine alisema zaidi sh. bilioni 11 zimekwama kulipwa kwani taarifa za kibenki zinaonyesha kuna matatizo hasa kwenye majina.

“Majina ya waliopeleka mzigo, yanatofautiana na majina ya akaunti za benki. Majina yaliyokataliwa na mfumo wa kibenki yatabandikwa kwenye vyama vya msingi ili wakulima wakarekebishe taarifa zao,” alisema.

Alisema takriban sh. bilioni 15 zimelipwa wa watoa huduma ambao ni wasafirishaji, wapagazi na wenye maghala.

(mwisho)

No comments:

Post a Comment