Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi, Taifa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan akizungumza na wajumbe wa kamati
ya Siasa ya Mkoa wa Pwani mara baada ya kujitambulisha rasmi kama Mlezi wa
Chama Cha Mapinduzi mkoa wa Pwani, hafla hiyo imefanyika kwenye ukumbi wa
Halmashauri ya mji Kibaha. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Ndugu Ramadhani Maneno (kulia) akimtambulisha
Mlezi wa CCM mkoa huo Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa, Makamu wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa wajumbe wa Kamati
ya Siasa ya Mkoa wa Pwani, kushoto ni Mkuu wa Mkoa huo Mhandisi Evarist
Ndikilo. (Picha na Ofisi ya Makamu wa Rais)
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi Taifa,
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan
amesema Serikali ya Awamu ya Tano imedhamiria kutumia fedha za ndani zaidi
kwenye shughuli za kimaendeleo kuliko kutegemea misaada.
Mhe. Samia ameyasema hayo leo mbele ya Wajumbe wa
Kamati ya Siasa ya Halmashauri Kuu ya CCM mkoa wa Pwani kwenye ukumbi wa
Halmashauri ya mji wa Kibaha.
Mjumbe huyo wa Kamati Kuu ambaye pia ni Makamu wa
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alijitambulisha rasmi kama mlezi wa CCM
mkoa wa Pwani na kuahidi kutoa ushirikiano wa kutosha .
Akizungumza na Wajumbe hao Mhe. Samia Suluhu Hassan
amewataka Viongozi wa Chama mkoani hapo kuhakikisha mali zote za Chama zinaleta
tija kwa Chama.
“Sasa ni wakati umefika kuangalia
mali zetu ndani ya Chama labda Wilaya ilikuwa inamiliki vitu gani? Viwanja vya
kujenga nyumba au vya michezo mali zozote ni kuziweka vizuri na kuhakikisha
zinazalisha kwa manufaa ya Chama.”
Mhe. Samia amesema kuwa Chama Cha Mapinduzi
kimejipanga kutoa mafunzo ya Uongozi katika ngazi mbali mbali ambapo yeye
binafsi amepangiwa mkoa wa Dar es Salaam, Pwani na Morogoro ambapo
atashirikiana na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara Ndugu Rodrick Mpogolo.
Pamoja na mambo mengine Mhe. Samia amewataka
Viongozi wa Chama cha Mapinduzi mkoa wa Pwani kufanya kazi kwa Umoja na
Ushirikiano ndani ya Chama pamoja na Serikali.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Pwani
Ndugu Ramadhani Maneno amemshukuru Mjumbe huyo wa Kamati Kuu kwa kuja
kujitambulisha na kutoa muongozo mzuri uliokubalika na kila mjumbe na kuahidi
kutoa ushirikiano mzuri kwa manufaa ya Chama Cha Mapinduzi.
No comments:
Post a Comment