Saturday, December 22, 2018

CCM YAKEMEA BAADHI YA WANACHAMA KUANZA KAMPENI ZA UBUNGE NJE YA UTARATIBU, KANUNI NA KATIBA YA CCM

22 Desemba 2018

Katika Mkutano Mkuu wa Jimbo la Peramiho, Wilaya ya Songea Vijijini Mkoa wa Ruvuma, Ndg. Humphrey Polepole Katibu wa NEC, Itikadi na Uenezi amesema CCM haikubaliani na tabia za baadhi ya wanachama wa CCM kuanza kampeni za ubunge mapema nje ya utaratibu, kanuni na katiba ya CCM.

Akieleza jambo hilo kwa undani, Ndg. Polepole amesema CCM inahimiza sana nidhamu ya Viongozi na wanachama na hivyo kufanya kampeni za ubunge kabla ya wakati, nikuanza kukigawa Chama, kujenga makundi, kudhoofisha juhudi za Mbunge aliyekuwepo katika nafasi hiyo na ni utovu wa nidhamu, jambo ambalo CCM haikubaliani nalo.

"Tupo macho sana tunajua wapo ambao wameanza kupitapita kwenye majimbo, nawaambia Chama kitawakata, hatukubaliani na vitendo vya utovu wa nidhamu vya kutafuta uongozi nje ya utaratibu ndani ya CCM". amesema Ndg. Polepole

Aidha Ndg. Polepole amepokea na kukabidhi vifaa vya kiutendaji vya Chama kwa niaba ya Ndg. Jenista Mhagama Mbunge wa Jimbo la Peramiho ikiwemo pikipiki 16 kwa makatibu wa CCM wa Kata zote za Jimbo la Peramiho, Baskeli 132 kwa Makatibu wa CCM wa  Matawi yote ya Jimbo la Peramiho, mabati 835 na Mifuko  1230 ya saruji kwaajili ya ujenzi wa ofisi za Matawi ya CCM Jimbo la Peramiho, rim za karatasi  kwa watendaji wa Kata, Wilaya na Mkoa na daftari kubwa kwa watendaji wa matawi yote ya Jimbo la Peramiho.

Ambapo Ndg. Polepole amewaasa Viongozi na watendaji waliokabidhiwa vifaa vya kiutendaji kuvitunza na  kuvitumia kwa manufaa ya Chama na siyo vinginevyo.

Kikao cha Mkutano Mkuu wa Jimbo kimehudhuriwa na Wajumbe wa Kikao hicho, Viongozi wa Chama Wilaya na Mkoa pamoja na Viongozi wa Serikali wakiongozwa na  Ndg. Oddo Killian Mwisho Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Ruvuma.

Imetolewa na,
IDARA YA ITIKADI NA UENEZI
CHAMA CHA MAPINDUZI

No comments:

Post a Comment