Friday, December 28, 2018

Baada ya maafa RC Wangabo aunga mkono juhudi za wananchi kukarabati shule





Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amechangia shilingi milioni tatu ili kuharakisha ukarabati wa ujenzi wa shule ya msingi Msia pamoja na shule ya sekondari Kipeta zote za bonde la ziwa rukwa, Wilayani Sumbawanga ikiwa ni kuunga mkono juhudi za wananchi katika kurudisha miundombinu ya shule hizo zilizoharibika baada ya upepo na mvua kali iliyonyehs amwanzoni mwa mwezi huu.

Kati ya fedha hizo shilingi milioni mbili zitatumika katika shule ya msingi Msia na shilingi milioni moja zitatumika kuikarabati shule ya sekondari kipeta ambapo zimebaki wiki mbili shule hizo kufunguliwa na wanafunzi kutakiwa kuendelea na masomo.

Mh. Wangabo aliwashukuru wananchi waliojitokeza kuchangisha fedha kwaajili ya ukarabati wa shule ya msingi Msia zilizofikia kiasi cha shilingi 5,595,000/= ambapo wananchi wa kawaida walichangia shilingi 5000/=, wafanyabiashara wadogo shilingi 20000/=, mfangabiashara wa kati shilingi 50000/= na wafugaji shilingi 100000/= ambapo fedha hizo zinatarajiwa kufanya ukarabati na ujenzi wa madarasa manane.

Awali akisoma taarifa ya harambee ya ukarabati wa shule Mtendaji wa kijiji cha Msia Andrew Sanga alieleza mikakati ya kijiji kuwa ni kuongeza vyumba vya madarasa vitatu, na ofisi moja ya walimu na msingi umeshaaza kujengwa, kukusanya michango kwa wananchi ambao bado kuchangia na hivyo kutimiza lengo la kujenga madarasa nane, ofisi mbili ndani kabla ya shule kufunguliwa mwanzoni mwa mwezi wa kwanza.

“Mheshimiwa mkuu wa mkoa mapungufu yaliyopo ni kama ifuatavyo, bati, madirisha, nondo, misumari, madirisha, milango na rangi, ili kukamilisha majengo tunayoendelea kuyajenga kwani shule hiyo yenye wanafunzi 866 ina uhitaji wa madarasa 22,” Alibainisha.

Katika kuunga Mkono juhudi hizo Mh. Wangabo alisema,”Pamoja na pongezi ambazo nilizitoa kwa wadau wote ambao wamechangia, na mimi nipende kushirikiana nanyi, nitachangia vifaa ambavyo inaweza ikawa mabati, au inaweza ikawa saruji, kulingana na hesabu zitakazokuwa zinapigwa na Mkurugenzi pale, nitachangia hivyo vifaa kwa shilingi milioni mbili.”

Pia aliwasihi mafundi wa madarasa hayo kujiahidi kuzingatia ubora katika ujenzi kuliko ilivyokuwa imejengwa hapo awali na kuwaomba wachukulie kazi hiyo ni kama ya kujitolea mchango wao katika kuunga juhudi za wananchi kumaliza shule hiyo.

Pia kwa upande wa shule ya sekondari ya Kipeta alichangia shilingi milioni moja kama mwanzo wa harambee itakayofanyika mwanzoni mwa mwezi wa kwanza mwaka 2019 ili kuhamasisha wananchi wa kijiji cha kipeta kuweza kuiboresha shule hiyo ambayo iliezuliwa mapaa yote pamoja na baadhi ya nyumba 4 za walimu ikiwemo ya mwalimu Mkuu.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga Sebastina Mwilima alisema kuwa tayari halmashauri imeshaagiza vifaa vyenya thamani ya shilingi milioni 23 kwaajili ya kufanikisha zoezi la kukarabati shule hizo ambapo shule ya msingi Msia madarasa manne yalianguka na shule ya sekondari Kipeta, madarasa, mabweni pamoja na nyumba za waalimu kuezuliwa mapaa. 

Maelezo ya Picha 
IMG_5456 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa pili toka kulia) pamoja na Mkuu wa Wilauya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule (wa kwanza Kulia) wakipita mbele ya madarasa ya Shule ya Msingi Msia kuona uharibifu uliofanywa na mvua ya tarehe 8.12.2018.

IMG_5462 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (wa kwanza kushoto)akionyeshwa maendeleo ya ujenzi wa madarasa unaoendelea ili kuhakikisha shule inapofunguliwa mwezi wa kwanza wanafunzi wanapata fursa ya kuendelea na masomo. 
IMG_5474 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akishiriki msingi wa ujenzi wa madarasa ya shule ya msingi Msia alipokwenda kuangalia ujenzi unaoendelea. 

IMG_5496 - Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo. 
Kipeta Sekondari - Jengo la Utawala la shule ya Sekondari Kipeta likiwa limeezuliwa paa.


No comments:

Post a Comment