Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kulia) akisalimiana na mmoja wa wanakikundi cha Wanawake cha Tupendane kinachojishughulisha na utengenezaji wa mabatiki kilichopokea hundi ya Shilingi Milioni 3.
Halmashauri ya manispaa ya Sumbawanga imetoa shilingi milioni 70.5 kwa
vikundi 21 vya vijana, wanawake na walemavu ikiwa ni utekelezaji wa Sera
ya Taifa ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi ya Mwaka 2004 yenye adhima ya
kuwainua wananchi kiuchumi ili kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Manispaa ya Sumbawanga imedhamiria kutekeleza maelekezo ya serikali kwa
kutenga asilimia 10 ya mapato ya ndani na kuwezesha vikundi hivyo ambapo tangu
mwaka wa fedha 2018/2019 uanze mwezi Julai hadi mwezi Novemba Halmashauri
tayari imeshakusanya Shilingi bilioni 1.1 ambayo ni nusu ya makusanyo ya
malengo waliyojiwekea kwa mwaka huu.
Fedha hizo zilitolewa katika hafla fupi ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu
wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo aliyekabidhi hundi kwa vikundi hivyo na
kuhudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Sumbawanga Dkt. Khalfan Haule, Meya wa
Manispaa ya Sumbawanga Mh. Justin Malisawa na viongozi mbalimbali wa vyama vya
siasa na vikundi husika.
Akisoma taarifa ya kukabidhi fedha hizo kwa vikundi
Mkurugenzi wa Manispaa ya Sumbawanga Jacob Mtalitinya alisisitiza kuwa Ili
dhamira ya Serikali ya kufikia uchumi wa kati na Tanzania yenye Viwanda itimie
shughuli utoaji wa mikopo lazima iwe endelevu na kuwa halmashauri imejiimarisha
katika kukusanya mapato yake ya ndani ili kuleta matunda kwa kutoa mikopo.
“Vikundi hivi vinajishughulisha na Usindikaji
mafuta, chakula,vinywaji, Useremala, Utengenezaji wa Chaki na ushonaji, ufumaji
na utengenezaji wa Mabatiki na Ufugaji wa kuku na ngombe wa maziwa. Pia
Halmashauri inatarajia kutoka kiasi cha mkopo kilichobakia kwa mwezi Januari,
2019 kitakachokuwa kimekusanywa kutokana na makusanyo ya ndani.” Alisema.
Aliongeza kuwa ili kuona vikundi hivyo vinakuwa
kiuchumi maafisa maendeleo ya jamii ngazi ya kata na halmashauri
kuhakikisha wanakuwa na orodha ya vikundi vilivyokopeshwa, kwaajili kufuatilia
shughuli za vikundi na kuwajengea uwezo pamoja na kubaini mwendo wa urejeshaji
wa mikopo kwa vikundi na kufanya ufuatiliaji wa marejesho ya mikopo.
KWa upande wake Mh. Wangabo aliipongeza Manispaa ya
Sumbawanga na kwaagiza wakurugenzi wote wa halmashauri zizlizopo Mkoa wa Rukwa
kuhakikisha wanatekeleza agizo hilo ili kuweza kukuza kipato cha mwananchi wa
Mkoa kwa kuwawezesha kiuchumi na hatimae kuongeza ajira pamoja na kukuza uchumi
wa viwanda.
Pi aliwapongeza wale waliofanikiwa kupata mikopo
hiyo na kuwasihi waweze kurudisha kwa wakati ili na wengine wapate fursa ya
kukopeshwa na kujikwamua na kuwaonya kutotumia fedha hizo kwa matumizi ambayo
yako tofauti na walichoombea.
“Serikali haitafurahishwa kuona fedha zilizokopwa zinatumika kwa malengo
ambayo hayakukusudiwa kama vile anasa, aidha, nitoe wito kwa Wakurugenzi wa
Halmashauri zote ndani ya Mkoa wetu kupitia hafla hii, kuweka mipango na
mikakati ya kuhakikisha wananchi wanawezeshwa kiuchumi ikiwa ni pamoja na
kuwaunganisha na wadau mbalimbali wa maendeleo ndani na nje ya Mkoa kwa
kadiri itakavyowezekana.”Alisisitiza.
Kuanzia mwaka 2013/2014 hadi 2017/2018 fedha
zilizopaswa kuchangiwa na Halmashauri yetu kama asilimia 10 ya mapato ya ndani
ni shilingi 684,055,823. Hata hivyo hadi kufikia Juni 2018 jumla ya shilingi
50,000,000 zilitolewa kwa vikundi 43 sawa na asilimia 7.3 ya lengo. kiasi cha
shilingi 634,055,823 hakikutolewa kutokana na mwenendo wa makusanyo.
No comments:
Post a Comment