Friday, November 30, 2018

Vijana Wahamasishwa Kujiepusha na Tabia Hatarishi Zinazopelekea Kupata Maambukizi ya VVU





Na; Mwandishi Wetu

Vijana Nchini Wameaswa kushirikiana na Serikalini pamoja na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya mambukizi ya virusi vya UKIMWI na kwa kuepuka Tabia hatarishi.

Akizungumza wakati wa kilele cha wiki ya Vijna kilichofanyika leo Jijini Dodoma ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya UKIMWI  Duniani itakayoadhimishwa kesho  Novemba Mosi 2018, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi Vijana Ajira Mhe. Antony  Mavunde amesema kuwa  Vijana ni zaidi ya asilimia 68 ya nguvu kazi ya Taifa hivyo ni vyema kundi hilo likachukua tahadhari katika kujikinga na maambukizi ya mapya ya VVU.

" Takwimu zinaonesha kuwa takribani watu elfu 81,000 huambukizwa Virusi vya UKIMWI kila mwaka hapa nchini, hii ni sawa na takribani watu 6750 kwa mwezi na kwa siku ni wastani wa watu 225 na katika maambukizi mapya kila mwaka asilimia 40 ni Vijana wenye umri miaka 15-24"; Alisisitiza Mhe. Mavunde

Akifafanua Mavunde amesema kuwa vijana kote nchini wanalo jukumu la kujikinga dhidi ya maambukizi ya Virusi vya UKIMWI kwa kuwa wanaomchango mkubwa  katika ujenzi wa Taifa hasa katika kujenga uchumi wa Viwanda.

Aliongeza kuwa  Nchi yetu imeridhia malengo ya Dunia ya SIFURI TATU ifikapo mwaka 2030, maana yake ni kuwa ifikapo 2030 tuwe na sifuri ya maambukizo mapya, sifuri ya vifo vitokanavyo na UKIMWI  na Sifuri ya vifo vitokanavyo na UKIMWI,Sifuri ya  unyanyapaa na ubaguzi kwa WAVIU.

Akizungumzia mwitikio wa wananchi, Mh. Mavunde amesema kuwa anawapongeza Vijana Jijini Dodoma kwa kujitokeza kwa wingi kushiriki katika maadhimisho ya wiki ya Vijana na kushiriki kuzungumzia masuala ya UKIMWI.

Aidha, Mhe. Mavunde alibainisha kuwa Kaulimbiu ya Maadhimisho ya Siku ya UKIMWI kwa hapa nchini inasema" PIMA VVU,JITAMBUE, ISHI'' kauli mbiu inatoa msukumo kwa watanzania kujitokeza kupima VVU kwa hiari baada ya ushauri nasaha.

Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania  (TACAIDS) kwa kushirikina na wadau wanaotekeleza shughuli za Mwitikio wa UKIMWI, imeratibu maadhimisho ya wiki ya Vijana kuelekea kilelele cha siku ya UKIMWI Duniani Desemba Mosi 2018 yanayotarajiwa kufanyika Jijini Dodoma.

No comments:

Post a Comment