Friday, November 30, 2018

MHE HASUNGA AIAGIZA BODI YA KOROSHO NDANI YA SIKU 31 KUFANYA USAJILI WA WAKULIMA

Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa CBT Mjini Mtwara, Tarehe 29 Novemba 2018.(Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo)
Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) akisisitiza jambo wakati wa kikao kazi kilichofanyika kwenye ukumbi wa CBT Mjini Mtwara, Tarehe 29 Novemba 2018

Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo-Mtwara

Bodi ya Korosho Tanzania imepewa siku 31 kuwa imekamilisha zoezi la usajili wa wakulima wa Korosho nchini.

Agizo hilo limetolewa tarehe 29 Novemba 2018 na Waziri wa Kilimo Mhe Japhet Hasunga (Mb) wakati alipokuwa akizungumza na wafanyakazi wa Bodi hiyo Mjini Mtwara.

Waziri Hasunga aliwasili Mkoani Mtwara juzi kwa ajili ya safari ya kikazi kujionea mwenendo wa ununuzi wa Korosho za wakulima ambapo pamoja na mambo mengine alikutana na kufanya mazungumzo na timu ya wataalamu wa Oparesheni Korosho.

Mhe Hasunga ametoa siku 31 kuanzia kesho tarehe mosi mwezi Disemba mpaka tarehe 31 mwezi Disemba 2018 agizo hilo kuwa limekamilika na kuwasilishwa ofisini kwake.

Alisema kuwa utambuzi huo wa wakulima utarahisisha serikali kumtambua kila mkulima na eneo analolima Korosho ili unapofika wakati wa malipo ya wakulima serikali iweze kuwalipa wakulima husika na sio wafanyabiashara wanaojipenyeza katika biashara hiyo maarufu kama (Kangomba).

"Serikali imekuwa ikihangaika kufanya uhakiki wa wakulima katika kipindi cha muda mrefu jambo hili linaonyesha wazi kuwa hamjatekeleza majukumu yenu ipasavyo" Alikaririwa Mhe Hasunga

Katika hatua nyingine Waziri huyo mwenye dhamana ya kilimo nchini alisema kuwa agizo hilo litakuwa kipimo kwa watendaji hao wa Bodi ya Korosho nchini.

Vilevile amesisitiza umoja na mshikamano kazini sambamba na kuwataka watendaji hao kuongeza bidii, nidhamu, wajabikaji na uadilifu kazini.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment