Saturday, November 24, 2018

MHE HASUNGA AANZA ZIARA YA KIKAZI MKOANI MOROGORO ASISITIZA UMUHIMU WA MBEGU BORA

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga akikagua ghala la kuhifadhia mbegu la Wakala wa Mbegu (ASA) katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro tarehe 24 Novemba 2018. Kulia kwake ni Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt Sophia Kashenge.(Picha Zote Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo).
Mtendaji Mkuu wa ASA Dkt Sophia Kashenge akimuonyesha Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga mfuko wa mbegu za alizeti zinazozalishwa na ASA wakati akiwa katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro tarehe 24 Novemba 2018. 
Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga akikagua ghala la kuhifadhia mbegu la Wakala wa Mbegu (ASA) katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro tarehe 24 Novemba 2018.

Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga akikagua mbegu mbalimbali zinazozalishwa na  Wakala wa Mbegu (ASA) katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro tarehe 24 Novemba 2018. 

Na Mathias Canal-Wizara ya Kilimo-Morogoro

Imebainika kuwa malighafi nyingi zinazozalishwa kwa ajili ya viwanda nchini zinatokana na sekta ya kilimo ambayo inategemewa na watanzania kwa zaidi ya asilimia 75.

Hayo yamebainishwa tarehe 24 Novemba 2018 na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Hasunga wakati akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Mbegu (ASA) katika ziara yake ya kikazi mkoani Morogoro.

Alisema kuwa serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe Rais Dkt John Pombe Magufuli imejipambanua katika usimamizi madhubuti wa ujenzi wa viwanda hivyo wananchi wanapaswa kuzalisha kwa wingi mazao mbalimbali katika sekta ya kilimo kwani uhai wa viwanda vingi vinategemea zaidi sekta ya kilimo.

Alisema kuwa Wizara ya kilimo itasimamia kwa weledi uzalishaji wa mazao mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuzalisha mbegu bora na kwa wingi ili wakulima waweze kunufaika katika uzalishaji wenye tija ili kuondokana na uzalishaji wa mazao kwa ajili ya chakula pekee badala yake kuzalisha kwa tija kilimo cha kibiashara.

“Katika viwanda tutakavyozalisha zaidi ya asilimia 60 ya malighafi zitakazotumika zinazalishwa hapa nchini, hivyo tunawajibu wa kutoa malighafi zinazotosheleza viwanda tunavyovianzisha” Alikaririwa Mhe Hasunga

Alisema kuwa wafanyakazi wote wa Wakala wa Mbegu (ASA) wanatakiwa kufanya kazi kwa bidii, juhudi na maarifa kwani ndio silaha pekee itakayowafanya waweze kuzalisha mbegu nyingi kwa manufaa ya mkulima mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla wake.

Alisema kuwa serikali ina mpango kabambe wa kuimarisha sekta ya kilimo nchini kitakachopelekea kupata chakula cha kutosha, kuongeza tija katika uzalishaji na kuongeza thamani ya mazao hayo.

“Huwezi kuwa na viwanda mpaka uanzie kwenye kilimo na kilimo hakiwezi kustawi bila kuwa na mbegu bora za mazao hivyo wakala wa mbegu ni Taasisi muhimu nchini kwenye sekta ya kilimo” Alisisitiza Mhe Hasunga

Aidha, Mhe Hasunga alisema kuwa wakulima wengi wamekuwa wakilima bila kufuata taratibu za kilimo hivyo wataalamu mbalimbali wa kilimo nchini wanatakiwa kufanya kazi zaidi kwenye maeneo ya wakulima kwa kufika mashambani ili kuwaongezea weledi na ujuzi wakulima kote nchini.

MWISHO.

No comments:

Post a Comment