Waziri wa kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga (Mb)
Naibu Waziri wa Wizara ya kilimo Mhe Innocent Lugha Bashungwa
Na Mathias
Canal-WK, Dar es salaam
SERIKALI kupitia
Wizara ya Kilimo inatekeleza Programu ya Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu
ya Pili (ASDP II) ambayo ni utekelezaji wa Mpango wa Uwekezaji katika Sekta ya
Kilimo Nchini (TASFIP) unaolenga kukuza kilimo kwa asilimia 6 kwa mwaka.
Kwa kuzingatia
hatua hizo, Wizara ya Kilimo imekusudia kuleta mageuzi ya kilimo kutoka mtazamo
uliopo wa kilimo cha kujikimu hadi kufikia uendeshaji wa kilimo kwa mfumo wa
kibiashara.
Hayo yamebainishwa
leo Tarehe 12 Novemba 2018 na Waziri wa kilimo Mhe Japhet Ngailonga Hasunga
(Mb) wakati akifanya mahojiano na Televisheni ya Taifa (TBC 1) Mara baada ya
kuapishwa kuongoza Wizara hiyo Ikulu Jijini Dar es salaam.
Mhe Hasunga
ameyataja maeneo matatu ambayo yanahitaji utekelezaji wa haraka. Mosi,
Utekelezaji wa adhma ya serikali kuendeleza kilimo kupitia Programu ya
Kuendeleza Sekta ya kilimo Awamu ya Pili (ASDP II) kwa kusimamia thabiti nguzo
ya programu hiyo ikiwemo Usimamizi endelevu wa matumizi ya maji na ardhi.
Alisema kuwa Lengo
la ASDP II ni kuleta mageuzi katika Sekta ya kilimo ili kuongeza
uzalishaji na tija, kilimo cha kibiashara, kuongeza pato kwa wakulima hivyo
nilazima kuwekwa mkakati madhubuti wa utekelezaji ili kufikia nalengo
yaliyokusudiwa.
Pili, Hasunga
alisema kuwa atashirikiana na wataalamu wote Wizarani ili Kuongeza tija na
faida kwenye mazao na kuendeleza kilimo cha biashara na kuongeza thamani ya
mazao.
Vilevile, alisema
kuwa serikali imekusudia Kuboresha mazingira wezeshi, uratibu, ufatiliaji na
tathmini katika sekta ya kilimo hivyo wataalamu katika Wizara ya kilimo
wanapaswa kuongeza kasi ya uwajibikaji ili kutimizi adhma hiyo.
Alisema Wizara ya
kilimo itaweka mkakati madhubuti wa kuhakikisha kuwa bei ya Mazao inaimarika
huku akisisitiza kuwa kwa ushirikiano na Wizara ya Viwanda, Biashara na
Uwekezaji atahakikisha wakulima wanapata masoko ya mazao yao.
Jambo la tatu
alilolieleza Waziri Hasunga kuhusu utendaji wake katika Wizara ya kilimo ni
pamoja na kusimamia kwa weledi upatikanaji wa pembejeo za kilimo na ili ziweze kuwafikia
wakulima kwa wakati kote mchini.
Kwa upande wake
Naibu Waziri wa Wizara ya kilimo Mhe Innocent Lugha Bashungwa alisema kuwa
anatambua kuwa asilimia zaidi ya 70 ya wananchi wanajishughulisha na kilimo
hivyo Wizara itaweka mkakati madhubuti kuhakikisha kuwa kilimo kina imarika na
kuwa na tija kwa wakulima wote.
Aliongeza
kuwa upotevu wa mazao baada ya mavuno ni suala linalohitaji kuzingatiwa
kwa kiasi kikubwa ili kunusuru hasara inayowakumba wakulima.
Alisema, Changamoto
hiyo inadumaza uzalishaji hivyo kufifisha ndoto ya kufikia uchumi wa viwanda
kwa wakati kama ilivyokusudiwa. Licha ya changamoto hiyo, Tanzania imeendelea
kuzalisha chakula kwa wingi kupita mahitaji yaliyopo.
Bashungwa
alisisitiza kuwa Upotevu huo una uhusiano na uchumi wa viwanda kwani mazao
yanayopotea au kuharibika yalipaswa kusindikwa lakini kwa kutokupelekwa kwake,
yanaharibika kabla ya kumfikia mlaji hivyo kusababisha hasara kwa wakulima
waliowekeza nguvu na rasilimali nyinginezo kwa muda mrefu.
Sambamba na hayo
alisema kuwa Kitaasisi Serikali inalenga kuleta muafaka na mlingano kati ya
kazi za Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji hasa
kwenye kazi zinazohusu miundombinu ya uhifadhi na utawala, kupunguza upotevu wa
mazao kwa kuongeza thamani na uchakataji wa mazao ya kilimo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment