Thursday, November 15, 2018

Baada ya miaka 6 bila ya kutumika soko la samaki Kasanga laundiwa timu kuchuguza ubadhirifu


Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh.Joachim Wangabo akipita katika sehemu ya kukaushia samaki ambayo haijawahi kutumika tangu soko hilo lizinduliwe mwaka 2012

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amwemuagiza katibu tawala wa Mkoa wa Rukwa kuhakikisha anaunda timu kwaajili ya kufanya uchunguzi juu ya matumizi ya fedha iliyotumika kwenye ujenzi wa soko hilo uliokamilika mwezi Novemba mwaka 2011 na kuzinduliwa mwaka 2012 na aliyekuwa makamu wa rais Dkt. Gharib Bilal.

Mh. Wangabo amesema kuwa hali ya soko ilivyo ni tofauti na thamani inayotajwa ambayo ilitumika kwaajili ya ujenzi wa soko hilo na tangu kuzinduliwa kwake halijaanza kutumika kama ilivyotarajiwa ambapo walengwa ni wakazi wapatao 35,205 waishio mwambao wa ziwa Tanganyika.

“Bilioni moja nukta imekwisha lala hapa, RAS unda timu ije ifanye tathmini ya fedha iliyotumika hapa, hiyo ni fedha ya serikali na tunakatisha tamaa wenzetu wanaotusaidia Jumuiya ya Ulaya wametoa zaidi ya milioni 700 na wengine MIVRAF wametoa milioni karibui 300, hawa wawili tu ni bilioni moja jumlisha milioni 100 za halmashauri bado hapa mahali hapajakamilika na mapungufu yapo,” Alifafanua.

Halikadhalika alieleza kuwa mfumo wa meko yaliyopo katika soko hilo sio rafiki wa mazingira hivyo aliwataka watakaotumia soko hilo wafikirie namna ya kutengeneza mkaa mbadala kwa kutumia makaa ya mawe yanayopatikana kwa wingi katika kijiji cha Nkomolotu, Wilayani nkasi mkoani humo.

Wakati akisoma taarifa ya soko hilo afisa uvuvi wa halmashauri ya Wilaya ya Kalambo Nicholas Mrango alisema kuwa wananchi wa mwambao huo wana fursa ya kuvua samaki kwa wastani wa tani 167,000 kwa mwaka na kuongeza pato la halmashauri na serikali kuu na kutaja malengo ya mradi huo na changamoto zake.

“Malengo ya mradi ni kuboresha hali ya uchumi wa wananchi, kupata wanunuzi wa samaki wa uhakika ndani nan je ya nchi lakini ili soko lianze kutumika linahitaji miundombinu ya umeme, chumba cha kukaushia samaki, mtambo wa kugandisha barafu, meza za kuuzia samaki na chanja za kuanikia ili kukidhi kiwango cha kimataifa,”Alibainisha.

Soko kuu la samaki hao ni pamoja na ndani ya wilaya ya Kalambo, mkoa wa Rukwa kwa ujumla, Mikoa ya Mbeya, Iringa,Njombe na Ruvuma na pia nchi za jirani za Zambia, Demokrasia ya Watu wa Congo, Rwanda na Burundi.  

No comments:

Post a Comment